MZOZO unaofukuta kati ya Misri na Ethiopia kuhusu uhalali wa matumizi ya maji ya Mto Nile, umeongeza hofu ya kuibuka vita baina ya mataifa hayo.
Misri imeiwashia Ethiopia taa nyekundu baada ya kusogeza vikosi vya majeshi Somalia na kuongeza sintofahamu.
Ikumbukwe Somalia inapakana na Ethiopia upande wa kaskazini, hivyo Misri kuanza kusogeza vikosi vyake eneo hilo kunaleta taharuki ukanda wa Afrika Mashariki na Pembe ya Afrika.
Ni wasiwasi wa tishio la kuibuka kwa ushirikiano wa kijeshi kati ya Somalia na Misri unaoongeza hasira kwa Ethiopia ghadhabu inayoweza kuwa zaidi ya vita.
Mvutano huo uliongezeka karibuni baada ya kuwasili kwa ndege mbili za kijeshi za Misri aina ya C-130 katika mji mkuu wa Somalia, Mogadishu, kuashiria mwanzo wa makubaliano yaliyotiwa saini mwezi uliopita.
Mpango huo unahusu Misri kuwapeleka wanajeshi 5,000 kujiunga na kikosi kipya cha Umoja wa Afrika (AU) mwishoni mwa mwaka huu, huku wengine 5,000 wakiripotiwa kupelekwa katika mpango mwingine tofauti.
Ethiopia, ambayo huko nyuma ilikuwa mshirika muhimu wa Somalia katika kupambana na wanamgambo wenye mafungamano na al-Qaeda, iko katika mgogoro na Misri baada ya kujenga bwawa kubwa kwenye Mto Nile, jambo ambalo Misri inapinga.
ETHIOPIA MTEGONI
Somalia licha ya kumleta karibu adui wa Ethiopia ambao wako vitani kupigania maji ya Nile, pia amepigilia msumari mwingine kwa kutangaza kwamba vikosi vya Ethiopia ambavyo viko nchini humo havitakuwa sehemu ya kikosi cha AU kuanzia Januari mwakani.
Kuna wanajeshi 3,000 wa Ethiopia chini ya ujumbe wa sasa wa Umoja wa Afrika, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
Waziri Mkuu wa Somalia anasema Ethiopia italazimika kuondoa wanajeshi wake wengine kati ya 5,000 na 7,000 waliowekwa katika maeneo kadhaa chini ya makubaliano tofauti ya nchi hizo mbili, kama haitajiondoa katika mkataba wa kumiliki bandari walioafikiana na jimbo la Somaliland.
Mtafiti mwandamizi kutoka Taasisi ya Royal United Services, Christopher Hockey, anasema hatua hiyo haitakubaliwa na Ethiopia ikiamini kuondolewa kwa wanajeshi wao kutaifanya nchi yake kuwa katika hatari ya kushambuliwa.
Anaiambia BBC kuwa kupelekwa vikosi vya Misri katika mpaka wake wa upande wa mashariki pia kutaifanya Ethiopia kuwa na wasiwasi.
Mkanganyiko huo ambao sasa umeleta hofu, unatokana na wazo la Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, ambaye anataka nchi yake ambayo haina bahari kuwa na bandari yake.
Ethiopia ilipoteza bahari wakati ilipotengana na Eritrea mwanzoni mwa miaka ya 1990.
Waziri Mkuu Abiy anaitia saini mkataba wenye utata na Jamhuri ya Somaliland iliyojitangazia uhuru wake kutoka Somalia, kukodi sehemu ya kilomita 20 sawa na maili 12 ya pwani yake kwa miaka 50 ili kuanzisha kambi ya kijeshi.
Anadaiwa kwenda mbali kwa kuonyesha nia ya kuitambua rasmi Somaliland kama nchi huru, kitendo ambacho kimeikasirisha Somalia.
Somaliland ilijitenga na Somalia zaidi ya miaka 30 iliyopita, lakini Somalia inatambua kama sehemu ya eneo lake.
CHANZO BWAWA
Tatizo inalopelekea nchi hizo kutishiana lilianza 2011 baada ya Ethiopia kuamua kujenga bwawa kubwa la Grand Ethiopian Renaissance (GERD) katika mto wa Blue Nile.
Bwawa hilo linategemea kuchukua zaidi ya asilimia 85 ya maji yake katika mto huo.
Misri, ambayo inategemea maji ya mto Nile kwa asilimia 80, imekuwa na hofu kuwa bwawa hilo litaathiri mfumo wa usambazaji maji na pia kuifanya Ethiopia kuwa na mamlaka juu ya usambazaji wa maji ya Nile ambao ni mrefu kuliko yote barani Afrika ukiwa na kilometa zaidi ya 6,000.
Muda utakaotumika kujaza maji katika bwawa hilo unaweza kuleta upungufu mkubwa wa maji Nile.
Ethiopia inasisitiza ni lazima kukamilisha mradi wake wa bwawa na kueleza itajaza maji kwa miaka sita.
Misri ilipendekeza kipindi cha miaka 10 ili kutoa nafasi maji kutiririka katika hali yake ya kawaida na kuepuka athari za ukame katika maeneo yake.
Mazungumzo kati ya Misri, Sudan na Ethiopia kuhusu kuendesha mradi huo wa bwawa yamekwama kwa miaka minne na sasa, huku Marekani ikijaribu kuwapatanisha bila mafanikio.
Misri inasema Ethiopia iliendelea kujenga mradi huo kwa nguvu na kupuuza maslahi na haki za nchi nyingine kwa matumizi ya maji na usalama wao.
Pia ilidai kuwa kupunguzwa kwa asilimia mbili ya maji kutoka mto Nile kunaweza kusababisha kupotea kwa karibu hekari 200,000 za ardhi za kilimo cha umwagiliaji.
HOFU YA WENGI
Misri inaona ushirikiano wake wa kijeshi na Somalia kama kete ya kuilazimisha Ethiopia kuachana na mradi wake wa bwawa.
Rais wa Misri, Abdul Fattah al-Sisi, anaona kuweka kikosi chake cha kijeshi Somalia kutaleta suluhu ya mgogoro huo.
Dk. Hassan Khannenje, ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Mikakati ya Pembe ya Afrika anasema mgogoro huo utasababisha mapigano kati ya Ethiopia na Misri ikiwa vikosi vyao vitakutana katika mpaka wa Somalia.
Somaliland pia imeonya kuwa kuanzishwa kwa kambi za kijeshi za Misri ndani ya Somalia kunaweza kuyumbisha eneo hilo.
Dk. Khannenje anaiambia BBC kwamba iwapo mzozo utazuka, huenda ukaathiri zaidi matumizi ya Bahari ya Shamu na biashara ya kimataifa.
Misri imepewa nguvu na mkataba wa kikoloni wa mwaka 1929 ambao Uingereza ilitoa haki kwa nchi hiyo kumiliki na kukataza kazi zozote zinazoweza kuhatarisha utiririshaji wa maji ya mto Nile.
Pia Misri ilipewa haki ya matumizi ya mita za ujazo bilioni 55.5 kati ya bilioni 84 ya maji ya mto Nile.
Misri ilikuwa na haki ya kutembelea na kuchunguza kila mahali mto huo unapopita na miradi inayofanyika ili kuulinda.
Hata hivyo, mwaka 2010 nchi nne za Afrika Mashariki na Kati zilisaini mkataba mpya wa matumizi ya maji ya mto Nile, huko Uganda na kuutengua ule wa awali ulioandaliwa na mkoloni.
Nchi zilizotia saini mkataba huo mpya ni Tanzania, Uganda, Kenya Ethiopia, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, Rwanda na Burundi.
Misri na Sudan ambazo zinatumia maji ya mto huo kwa kiwango kikubwa zilishiriki katika majadiliano, lakini zilipinga vipengele vyote 15 vilivyomo katika mkataba huo mpya.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED