SIMU NI JASUSI: Unayeitumia hufichi kitu unabeba bomu mfukoni

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:23 AM Oct 08 2024
Simu inakudukua, chunga.
PICHA: MTANDAO
Simu inakudukua, chunga.

UJASUSI wa kidijitali ni jambo linalowahusu wanaotumia vifaa vya mawasiliano kama simu janja au ‘smartphones’ kuujua ukweli kwamba wanatembea na bomu linalolipuka mfukoni.

Ni kama kubeba mzinga wa nyuki wanaoweza kukung’ata na kukuangamiza. Kwa sababu majasusi wanadukua taarifa zako wanavyotaka bila wewe uliyeiweka mfukoni au kwenye pochi kujijua.

Wanaweza kutizama maandiko (text), ujumbe (SMS), picha na kutumia kamera kukupata mubashara kwenye video au vyovyote wanavyohitaji.

Kwa hiyo simu ya mkononi ni jasusi usiyelijua lakini uliyembeba. "Watu wanaonekana hawaelewi kwamba usalama wa simu za mkononi kama kitu kimoja ni jambo ambalo halipo," inasema BBC.

Inaeleza wasiwasi mkubwa kwamba hakuna  faragha kwenye  simu za mkononi kwa sababu zimebainika  kuwa na programu za kijasusi. Mojawapo ni kama ‘Pegasus’,  inayotengenezwa na kampuni ya NSO Group ya Israel. 

Programu ya ujasusi ya Pegasus kutoka kampuni ya NSO Group ilizua maswali kuhusu usalama wa simu janja.

Miaka ya karibuni imegundulika kuwa programu ya Pegasus inaweza kukuweka kwenye simu za iPhones na Android, na kuruhusu  kutoa ujumbe, picha na barua pepe, kurekodi simu na kuwasha  kipaza sauti au ‘mic’ na kamera na  kufanya kazi yake kwa siri kama majasusi wanavyotaka na kuiongoza.

Kiasi  teknolojia inavyoendelea haraka na kwa nguvu upelelezi na uchunguzi sasa hivi unawafanya wanaotumia simu ‘kuonekana mno’ au kuachwa  wazi bila kificho ama kizuizi  cha kudukuliwa.

Uchunguzi wa Kituo cha Utafiti cha Pew unaonyesha kuwa Wamarekani asilimia 72 waliripoti kuwa wanachunguzwa katika simu zao na kufuatiliwa.

Wanaowadukua ni watangazaji wa matangazo ya biashara, kampuni za teknolojia au kampuni zingine na idadi kubwa inaamini kuwa shughuli zao nyingi mtandaoni zinafuatiliwa na serikali.

Ni wazi kuwa kuna uingiliaji wa aina nyingine na kwamba hakuna ulinzi kwenye masuala ya kutumia simu janja. Ni kama kutembea bila mavazi.

Japo si kila mtu lakini wapo baadhi ambao majasusi wanawafanyia kazi kwa niaba ya serikali zao, kampuni au hata usalama wa mataifa.

Dunia leo inathibitika kuwa matumizi ya simu za mkononi yanakuja na madhara ambayo mwanzoni watu wengi hawakuyajua kuwa yanaweza kuvuruga maisha yao.

Sio tu kiafya bali pia kisaikolojia na hata kuyahatarisha maana vilipuzi vinaweza kutumiwa kwa njia ya simu na kukuangamiza.

Simu ina alama za vidole, ina picha, anuani, umri, uraia na popote unapoishika unaonekana. 

Baadhi ya matukio ya kutumia ujasusi wa vifaa vya kielektroniki zikiwamo simu za mkononi na kuua watu ni lile la kushambuliwa kiongozi wa kundi la Hezbollah la Lebanon Hassan Nasrallah.

Pamoja naye, udukuzi wa kupitia vifaa vya kielektroniki umeharibu vifaa vya mawasiliano kuanzia simu za upepo, za mkononi, kompyuta na vifaa vingine vyote vya kundi la Hezbollah. 

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) Mwanza, Dk. Kamugisha Byabato, anasema matumizi ya ujasusi kwenye vifaa vya kielektroniki yanaakisi ukweli kuwa watumiaji wa simu hizo wameanikwa zaidi.

Anakumbusha kuwa hakuna kificho cha mahali ulipo, unachofanya na kwa ujumla shughuli zako zama hizi.

Mtaalamu wa uhandisi wa nishati mbadala na teknolojia anasema ni jambo ambalo linaamsha wataalamu kubuni na kuanzisha njia nyingine zenye usalama zaidi za mawasiliano.Anaeleza kuwa zinahitajika juhudi nyingine zaidi ya kuibua na kutumia mawasiliano hayo iwapo taifa linahitaji kuwa na usalama zaidi.

Anasema japo si kila mtu anaweza kudukuliwa wala kufuatiliwa lakini, ukweli ni kwamba hakuna kificho kwenye simu janja.

Na majasusi wanafahamu wanaowalenga pote duniani hivyo tahadhari ni muhimu.

Anaeleza kuwa dunia ya sasa ujasusi unaweza kutumia simu hizo na vifaa vya kielektroniki kupata chochote wanachotaka.

Anaongeza kuwa wanaweza  kufuatilia mwenendo wa watu wanaowaona kuwa ni hatari au wanaotishia maslahi yao, popote duniani. 

Kwa mfano kupitia simu na vifaa vya mawasiliano vya kielektroniki mfano GPS, majasusi au yeyote anayehitaji taarifa za mtu fulani anavitumia kumfikia na kupata kile anachokitaka.