RIPOTI MAALUM: Nchi ina walimu 68 tu wa somo la Uraia

By Francis Kajubi , Nipashe
Published at 07:11 AM Jun 15 2024
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.
Picha: Maktaba.
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.

KATIKA shule za sekondari za serikali Tanzania Bara kuna walimu 68 pekee wenye sifa za kufundisha somo la Uraia, mwandishi wa habari hii amebaini.

Hao ndiyo wanaostahili kuwafundisha somo hilo wanafunzi wote wa kidato cha kwanza hadi cha nne katika shule za umma za sekondari nchini.

Hata hivyo, kutokana na uhaba uliopo, walimu wasio na sifa za kufundisha Uraia, ndiyo wanabeba jukumu kufundisha somo hilo katika shule hizo za umma.

Athari za uhaba huo ni kushuka ufaulu wa somo hilo kwa kasi unaoonekana kwenye matokeo ya upimaji kidato cha pili na Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne.

Uchunguzi wa kitakwimu umebaini kuwapo wanafunzi wanaopata daraja "A", "B+" au "B" katika masomo ya Hisabati, Fizikia na Kemia lakini wanaangukia daraja "C", "D" au "F" katika somo la Uraia.

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, walimu wa somo la Uraia katika shule za sekondari ni wale ambao wamehitimu shahada au stashahada ya ualimu kwa kulisoma somo la Sayansi ya Siasa vyuoni kama somo mahususi watakalofundisha shuleni.

Ripoti ya Upimaji wa Wanafunzi wa Kidato cha Pili 2022 (FTNA 2022) ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ambayo mwandishi ameiona, inabainisha kuwa hadi Aprili 2022, Tanzania ilikuwa na walimu 66 pekee waliosoma Sayansi ya Siasa kama somo mahususi la kufundisha katika shule za sekondari.

Walimu hao ndiyo wenye sifa ya kufundisha somo la Uraia waliokuwa katika shule za sekondari za serikali hadi wakati huo (Aprili 2022).

Hata hivyo, mwandishi anafahamu kwamba idadi yao iliongezeka hadi kufikia walimu 68 kufikia mwezi Februari mwaka huu.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mahitaji ya walimu waliosomea kufundisha somo la Uraia katika shule za sekondari mwaka 2022 yalikuwa walimu 15,816. Hata hivyo, mahitaji yaliongezeka kufikia walimu 16,695 Februari 2023, kwa mujibu wa FTNA 2023.

Ripoti (FTNA 2022) inaonesha wanafunzi 635,130 walisajiliwa kufanya mtihani wa upimaji wa kidato cha pili mwaka 2022, ingawa ni wanafunzi 633,095 waliofanya mtihani wa somo hilo. Kati yao, 436,094 (asilimia 68.88) walipata daraja "F" katika somo hilo.

Kwa mujibu wa Baraza la Mitihani (NECTA), wanafunzi 125,788 (asilimia 19.87) walipata daraja "D", 59,995 (asilimia 9.48) walipata daraja "C", 8,058 (asilimia 1.27) walipata daraja "B" na 3,160 (asilimia 0.5) walipata daraja "A".

Katika Shule ya Sekondari Goba Mpakani, mkoani Dar es Salaam, wanafunzi 304 walifanya mtihani huo. Kati yao, mmoja alifaulu kwa daraja "C", 41 walipata daraja "D" na wanafunzi 262 walifeli, kwa maana walipata daraja "F".

Hata hivyo, matokeo ya mtihani huo wa upimaji wa kitaifa kidato cha pili, yanaonesha asilimia 57 ya wanafuzi waliopata daraja "F" katika somo la Uraia katika shule hiyo walipata daraja "B+", "B" na "C"katika masomo ya Hisabati, Fizikia na Kemia.

Joseph Kiriri, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Goba Mpakani, anasema shule inao walimu wanne wanaofundisha somo la Uraia; mmoja ndiye amesomea kufundisha somo hilo.

"Mmoja amesomea kufundisha somo la Fasihi ya Kiingereza, mwingine somo la Kiswahili na mwingine somo la Historia, ila wote wanafundisha Uraia. Hii ndiyo sababu kuu wanafunzi kufeli somo hili," anasema Mwalimu Kiriri na kueleza kuwa shule inavyo vitabu vingi vya somo la Uraia katika maktaba yake kulinganisha na masomo mengine.

Anasema upungufu wa walimu wa Uraia unachangiwa na kutokupandishwa vyeo walimu wa somo hilo kwa muda mrefu hata kama sifa wanazo, jambo linalofanya wengi wao kuacha kufundisha na kuingia katika siasa.

Mwalimu Joyce Mbise wa Shule ya Sekondari Goba Mpakani, anasema amesomea kufundisha Historia, lakini anafundisha Uraia shuleni huko kutokana na uhaba wa walimu uliopo.

Anasema alianza kufundisha shuleni huko mwaka 2013 baada ya kuhitimu Stashahada ya Ualimu katika Chuo cha Ualimu Songea.

"Ilinichukua mwaka mzima kujifunza na kuzoea kufundisha Uraia. Ninafundisha mikondo mitano, kila mmoja ukiwa na wanafunzi kati ya 55 hadi 65," alisema Mwalimu Joyce.

Hata hivyo, Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 iliyofanyiwa mapitio mwaka jana, inaelekeza shuleni kuwe na uwiano wa 1:45 (yaani mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45). Hivyo, Mwalimu Joyce amebeba mzigo wa ziada.

Grace Mwaisabila ni mwalimu pekee aliyesomea kufundisha somo la Uraia shuleni Goba Mpakani. Alihitimu Shahada ya Elimu mwaka 2009 katika Chuo cha Ualimu Mkwawa.
 Anasema kuwa baada ya kuhitimu alipangwa kufundisha somo la Uraia kidato cha I-IV katika Shule ya Sekondari Kilakala, mkoani Morogoro.

"Pale shuleni nilikuwa mwalimu pekee aliyesomea kufundisha Uraia. Walimu wenzangu wawili; mmoja alikuwa amesomea kufundisha Historia na mwingine Jiografia, lakini wote tulikuwa tunafundisha somo hilo (Uraia)," anasema.

Mwalimu Grace anasema alihitimu chuoni Mkwawa pamoja na wenzake takribani 300 waliosomea Sayansi ya Siasa. Baadhi walichagua kuendelea na elimu ya juu zaidi huku wengine wakitafuta kazi ya kufundisha katika shule za sekondari zinazomilikiwa na watu na taasisi binafsi.

Kwa mujibu wa ripoti ya Sensa ya Watu na Makazi Mwaka 2022 ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Tanzania Bara ina jumla ya shule za sekondari 5,592. Hata hivyo, ripoti hiyo haibainishi ni shule ngapi zinamilikiwa na serikali.

Uraia si somo pekee lenye uhaba wa walimu katika shule za sekondari za umma Tanzania Bara. Ripoti ya FTNA 2022 inaonesha kuwapo uhaba wa walimu wa Kiingereza 11,337 (asilimia 47).

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mahitaji yalikuwa walimu 21,435 hadi kufikia Desemba 2022, lakini walimu wa Kiingereza waliokuwapo ni 11,337.

Ni upungufu unaotajwa kuchangia asilimia 40 ya wanafunzi wote waliofanya mtihani wa upimaji wa kidato cha pili mwaka 2022 kupata daraja "F" katika somo hilo.
 
 JEDWALI LA UHABA WA WALIMU

Somo Mahitaji Waliopo Upungufu %
 Historia 17,318 15,960 1,358 8
 Jiografia 18,181 13,755 4,426 24
 Kiswahili 16,792 15,828 964 6
 Fasili (Eng) 2,964 30 2,934 99
 Kiingereza 21,435 11,337 10,098 47
 Baiolojia 17,813 5,795 12,018 67
 Kemia 16,664 6,074 10,590 64
 Fizikia 16,334 3,758 12,576 77
 Hisabati 19,216 5,537 13,679 71
 Uraia 15,816 66 15,750 99.6
 Hali ya upungufu wa walimu katika shule za sekondari za umma kidato cha I-IV. CHANZO: FTNA 2022.

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, anathibitisha kuwapo changamoto ya upungufu wa walimu nchini, akieleza kuwa wizara imeandaa mwongozo wa walimu kujitolea ili kuziba upungufu huo.

"Tumekwishaanza kuchukua hatua kukabili changamoto ya upungufu wa walimu si tu katika shule za sekondari, bali pia katika ngazi zote za elimu. Mojawapo ya hatua hizo ni kuandaa mwongozo wa walimu wa kujitolea," anasema Prof. Mkenda.

Mwandishi wa habari hii ameona nakala ya mwongozo huo uliopewa jina la "Mwongozo wa Walimu wa Kujitolea katika Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi Tanzania Bara wa Juni 2023".

Utangulizi wa mwongozo huo unabainisha kuwa hadi mwezi Machi 2022 kulikuwa na jumla ya wanafunzi 14,853,242 katika ngazi zote za elimu Tanzania Bara. Kati yao, 1,433,779 ni elimu ya awali, 10,873,782 wa shule za msingi, 2,530,651 wa sekondari na 15,030 wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.

Mwongozo huo unabainisha kuwa katika ngazi zote tajwa kulikuwa na walimu 270,614. Kati yao, 10,134 ni wa elimu ya awali, 170,730 wa shule za msingi, 89,500 wa sekondari na 250 wa Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.

"Hata hivyo, mahitaji ya walimu katika ngazi zote tajwa za elimu ni 538,060. Hii inaashiria kuwapo upungufu wa walimu 267,446," unabainisha mwongozo huo.

Mwongozo huo unabainisha taratibu ambazo waombaji watazipitia ili kupata nafasi za kufundisha kwa kujitolea huku ukisema kuwa maslahi yao yataamuliwa na halmashauri husika.

Kwa mujibu wa mwongozo huo hadi mwezi Julai 2022, kulikuwa na walimu wa kujitolea 17,237 nchi nzima.  Kati yao, walimu 10,373 walikuwa katika shule za msingi, 6,542 walikuwa katika shule za sekondari na 322 walikuwa katika Vyuo vya Maendeleo ya Wananchi.

Kimsingi, uhaba wa walimu shuleni unakwaza utekelezaji wa Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano (2021/22-2025/26).

Mpango huo pamoja na mambo mengine umebainisha malengo muhimu katika sekta ya elimu yanayotakiwa kufikiwa ifikapo mwaka 2026, ambayo ni pamoja na kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia katika shule za msingi na sekondari na kuboresha uwiano wa walimu na wanafunzi katika ngazi zote.

Hali hiyo pia inakinzana na Katiba ya nchi, Ibara ya 11(2) inayoelekeza utoaji haki ya kujielimisha katika fani ambayo kila raia anao uhuru kufikia upeo anaotaka kulingana na stahiki na uwezo wake.

*ITAENDELEA KESHO