Wanawake, vijana kung’ara kiuchumi, EU yawapa bil.12

By Gaudensia Mngumi , Nipashe
Published at 02:14 PM Jun 20 2024
Wafanyabiashara wadogo na wa kati ni zaidi ya milioni tatu na wanachangia zaidi ya asilimia 27 ya Pato la Taifa.
Picha: Maktaba
Wafanyabiashara wadogo na wa kati ni zaidi ya milioni tatu na wanachangia zaidi ya asilimia 27 ya Pato la Taifa.

UMOJA wa Ulaya (EU), umewapa wajasiriamali wa Tanzania Euro 4,000,000 kwa ajili ya kufanikisha miradi mbalimbali ya kiuchumi popote walipo.

Makubaliano ya kutolewa fedha hizo yalifanyika Dar es Salaam jana, kati ya Umoja wa Ulaya (EU) na Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT), kwenye mkutano ulioshirikisha wadau wakiwamo taasisi za fedha, maofisa wa serikali, wajasiriamali na sekta binafsi.

Akizungumza kwenye halfa ya kusaini mkataba, Mkuu wa Ushirikiano wa EU Cedric Mellel, alisema fedha hizo takribani Sh.bilioni 12 zimelenga kuwanufaisha wajasiriamali wadogo na wa kati wanawake na vijana.

Alisema wanufaika ni pamoja na walio kwenye kilimo, uvuvi-uchumi wa bluu, biashara  na miradi ya hifadhi mazingira.

Akizungumzia fedha hizo Dk. Peter Kingu, Mkuu wa Sera, Wajasiriamali na Huduma Jumuishi za Fedha wa mfuko wa FSDT, alisema asilimia 70 ya wanufaika wa fedha hizo watakuwa wanawake wakati vijana ni asilimia 30.

Alisema wanalenga kuwafikia wayu 200 na kuwawezesha  kuanzisha, kuendeleza miradi  na kununua vifaa au vitendea kazi.

Aliongeza kuwa msaada huo kwa walengwa utaanzia Sh. 5,000,000 hadi milioni 30 na kwamba vitendea kazi vitakavyopata fedha hizo  ni vile vinavyopunguza uharibifu wa mazingira.

Dk. Kingu alisema ni pamoja na majiko banifu, yanayotumia nishati jua, pikipiki zinazotumia gesi au betrii na vingine vinavyopunguza uzalishaji wa hewa ukaa na kuchafua mazingira.

Aliongeza kuwa fedha hizo siyo mikopo bali ni msaada kwa ajili ya kuendeleza ujasiriamali kwenye sekta mbalimbali kuanzia kilimo, viwanda vidogo, usindikaji, uvuvi  na biashara ndogo ndogo.

Alisema zitapatikana kwa kuandika andiko la mradi (business proposal) linaloeleweka na lenye kukidhi viwango na sifa za  kupewa fedha hizo.

Akizungumza kupatikana kwa fedha hizo, wakati wa mkutano huo Kamishna wa Kuendeleza Fedha na Uchumi, kutoka Wizara ya Fedha, Dk. Charles Mwamwaja, alisema ni mmoja wa wadau na mshirika wa Tanzania katika kuchang ia fedha za maendeleo na safari hii  imetoa Yuro 4,000,000 kukuza wajasiriamali wadogo na wakati hasa wanawake.

Alisema benki mbalimbali na taasisi nchini zimepokea fedha kwa ajili ya kutoa mikopo nafuu ya kusaidia wakulima, wafugaji, viwanda vidogo na wavuvi kwenye uchumi wa bluu ikilenga kuwainua wanawake na vijana.

Hata hivyo, Dk. Mwamwaja alisema fedha hazitolewi bila kukidhi viwango ikiwa ni pamoja na kuandika andiko la biashara lenye sifa na linalokopesheka.

Alitahadharisha kuwa miradi mingi inasuasua kutokana na sababu kadhaa lakini mojawapo ni kukosa elimu ya fedha, kuweka rekodi, kutunza akiba, ujuzi wa ujasiriamali na elimu ya utafutaji.

Kamishana wa Kuendeleza Fedha na Uchumi, alisema ili kukabiliana na upungufu huo benki na taasisi nyingine zinawajengea uwezo wanufaika ili miradi iwe endelevu.

Washiriki wa mkutano huo wakiwamo taasisi za fedha na benki walisema wanawake wajasiriamali  kwenye kilimo, ufugaji, viwanda vidogo, biashara na uvuvi wamenufaika na mikopo na misaada kutoka  EU.

Walisema taifa linajivunia programu mahsusi za ujumuishaji wanawake kwenye mikopo na misaada ya kifedha ambao wengi wanaweka akiba na kuongeza mitaji.

EU inatoa fedha kwa benki na taasisi za fedha kupitia programu maalum zinazolenga mikopo kwa wanawake na vijana ambao wameanzisha miradi mijini na vijijini.