WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ametoa maagizo kusaidia kuongeza usalama kwa watu wenye ualbino nchini na kukomesha vitendo vya unyanyasaji na mauaji dhidi yao.
Alitoa maagizo hayo bungeni jana wakati wa kipindi cha maswali ya papo hapo kwa Waziri Mkuu.
Ni baada ya Mei 31, mwaka huu kutokea tukio la kutekwa kwa mtoto Asiimwe Novati (mwenye ualbino) aliyekuwa na umri wa miaka miwili na nusu mkazi wa kitongoji cha Mbale, kijiji cha Mulamula, Kata na Tarafa ya Kamachumu, Wilaya ya Muleba, Mkoa wa Kagera nyumbani kwao Kebyera.
“Mheshimiwa Naibu Spika, tarehe mosi Juni, 2024 Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera na Ofisi ya Rais – TAMISEMI, walithibitisha kutokea kwa tukio hilo.
“Mtoto huyo alikuwa na mama yake wakati walipovamiwa na vijana wawili majira ya saa 2:15 usiku ambapo mmoja alimkaba koo mama yake ambaye alikuwa nje ya nyumba na mwingine aliingia kwa haraka ndani na kumchukua mtoto na kutokomea naye kusikojulikana,” alisema.
Waziri Mkuu alisema, ili kuzuia unyanyasaji na mauaji ya watu wenye ualbino, mamlaka za mikoa na serikali za mitaa zinawajibika katika usimamizi, ulinzi na utoaji wa huduma kwa watu wenye ualbino.
“Hivyo basi, wakuu wa mikoa na wilaya hakikisheni kila halmashauri inaanzisha operesheni maalum za ulinzi kwa watu wenye ualbino,” alisisitiza.
Aidha, alisema operesheni hizo zihusishe vikosi vya usalama ili kuhakikisha ulinzi wa watu wenye ualbino dhidi ya mashambulizi na vitisho.
Vile vile, alisema mamlaka za mikoa na wilaya zihamasishe ushiriki wa jamii katika ulinzi na haki za watu wenye ualbino.
Alikumbusha wajibu wa wazazi kwa watoto wao ni kuwapa malezi bora yatakayowawezesha kuwa watu wema katika jamii ambayo wataweza kuitawala dunia.
Amesema viongozi wa dini wana jukumu kwenye suala la kukemea maovu yanayotendeka kwenye jamii hususan mauaji ya watu wenye ualbino nchini kunaonesha upotofu wa maadili na kukosa hofu ya Mungu.
“Vitendo hivyo vinapaswa kukemewa kwa nguvu na nitumie nafasi hii kuwaomba viongozi wetu wa dini tuungane pamoja katika kupambana na mauaji haya ya watu wasiokuwa na hatia hata kidogo.
“Hivyo, niwasihi watumie majukwaa yao ya ibada kuwahubiria waumini wao kuachana na vitendo hivyo vya ukatili ambavyo hata Mwenyezi Mungu anavikataza, watu wenye ualbino wana haki ya kuishi kama walivyo watu wengine,” alisema.
Akiwageukia waganga wa jadi, alisema wanayo nafasi kubwa ya kutoa mchango wao katika mapambano na vita hiyo ya kuwalinda wenye ualbino.
“Ni wajibu wao kushiriki kukemea vitendo hivi vya mauaji na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa kuheshimu na kuthamini maisha ya kila mtu, bila kujali hali ya maumbile yake,” alisema.
Aliagiza waganga wa jadi nchini kushiriki kikamilifu katika kampeni za kupinga mauaji ya watu wenye ualbino.
“Wakati umefika kwenu nyote kushirikiana na serikali katika kutokomeza imani potofu zinazochangia mauaji haya. Ninawasihi sana elezeni wazi kwamba hakuna tiba wala mafanikio yanayoweza kupatikana kwa kutumia viungo vya watu wenye ualbino, badala yake matendo haya yanavunja haki za binadamu na kumomonyoa utu wetu kama Taifa,” alisema.
Alisisitiza kuwa Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lifanye usajili wa waganga wa jadi na vituo vyao sambamba na aina ya huduma wanayoitoa kwa wateja wao ili kudhibiti huduma holela isiyofuata misingi ya utu na haki za binadamu.
Majaliwa alitoa wito kwa kwa Chama cha Waganga wa Tiba Asili na Tiba Mbadala Tanzania (CHAWATIATA) kiwakatae na kuwatenga waganga wanaotumia njia za imani potofu, ramli chonganishi ikiwamo kutoa masharti ya kufanya mauaji ya watu wenye ualbino ili kufanikisha mahitaji ya wateja wao.
“Vile vile, toeni taarifa kwa mamlaka husika ili hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi yao.”
Alisema kutokana na nafasi yao ya pekee, waliyonayo viongozi wa kimila amewasihi kutoka kila kona ya Tanzania, washiriki kikamilifu kukemea na kupinga mauaji ya watu wenye ualbino.
“Ninawaomba viongozi wetu wa kimila wakiwamo machifu washirikiane na serikali kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama pindi wanapopata fununu za mipango au vitendo vya mauaji ya watu wenye ualbino katika maeneo wanayoishi,” alisema.
Jeshi la Polisi pia limetakiwa kuchukua hatua za haraka linapopata fununu ya uwapo wa njama za utekaji na mauaji ya watu wenye ualbino.
“Kuendelea kufanya operesheni ya kuwakamata wote waliotajwa na watakaotajwa kuhusika kwenye matukio ya aina hii kwa lengo la kuua mtandao mzima wa wahalifu hawa na operesheni hizo ziwe endelevu, polisi jamii ishirikishwe kikamilifu ili kupata taarifa zote muhimu katika maeneo husika na watoa taarifa wote walindwe ipasavyo,” alisema Majaliwa.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED