Viongozi wa dini wahimizwa kukemea ushoga, ulawiti

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:56 AM Jun 20 2024
Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Zakaria Mwansasu.
Picha: Maktaba
Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Zakaria Mwansasu.

VIONGOZI wa dini wamehimizwa kukemea vitendo vya ushoga na ulawiti dhidi ya watoto na vijana pamoja na kushirikiana na serikali kudhibiti na kumaliza hali hiyo, kwamba vitendo hivyo vinasababisha mmomonyoko wa maadili ndani ya jamii.

Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Uyui, Zakaria Mwansasu, wakati akimwakilisha Mkuu wa Mkoa Tabora, Paul Chacha, katika Baraza la Eid- Al-adha.

Alisema viongozi wa dini ni wazazi na walezi ambao wanapaswa kupaza sauti zao katika kukemea vitendo hivyo viovu. 

"Tupaze sauti zetu kwa nguvu kubwa ili kukemea vitendo hivyo viovu, vinavyosababisha vijana wetu kukosa nguvu kazi za kimaendeleo kwa kushindwa kujishughulisha na kazi halali za kujiingizia kipato, kwa sababu wameharibiwa na watu wenye roho mbaya, lakini zikiwapo nyumba za ibada katika maeneo ya vijijini kutasaidia vijana na watoto kuwa katika maadili mazuri,” alisema Mwansansu.

Alisema viongozi wa dini wasisite kuwaita viongozi wa serikali, kuwaambia ukweli kama kuna jambo wameliona ambalo haliendi sawa. 

Mjumbe wa Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA) Taifa, Shekhe Hilali Kipozeo aliwahimiza waumini hao kuipigania dini hiyo, watambue nia njema wakiwa na imani ili kuvuta baraka na sadaka.

Alisema sadaka inafungua milango ya mafanikio, huku akiwataka kuchangia ujenzi wa ofisi ya Jumuiya ya Wanawake wa kiislamu mkoani Tabora.