Moto usiojulikana chanzo unavyoitikisa Marekani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:10 AM Jan 14 2025
 Moto usiojulikana chanzo unavyoitikisa Marekani.
Picha:Mtandao
Moto usiojulikana chanzo unavyoitikisa Marekani.

MOTO asilia au wa nyika usiozimika ama mgumu kudhibitika unateketeza sehemu kadhaa za jiji la Los Angeles kwenye jimbo la Calfornia nchini Marekani.

Umesababisha vifo vya takriban watu 16, kuharibu mamia ya majumba, miundombinu  na kulazimisha zaidi ya wakazi  130,000 kukimbia nyumba zao za kifahari katika jiji hilo la pili kwa ukubwa Marekani.

Licha ya jitihada za wazima moto, miale mikubwa ya moto inaelezwa kuwa inaendelea kushika kasi, huku hali ya hewa ya ukame na ukavu na athari za mabadiliko ya tabianchi zikitarajiwa kuendelea kuzidisha moto kama huo siku zijazo.

Kwa mujibu wa taarifa za CNN, watu 16 wamefariki wakati nyumba 5,000 zimeharibiwa na moto huo ambao unatajwa kuwa haujawahi kuonekana katika jimbo hilo la Calfornia.

NI NINI SABABU?

Watu wanaweza kujiuliza inakuwaje kuwe na moto wa asili ambao hakuna anayehusika kuuwasha? 

Kwa mujibu wa taarifa za kimtandao, unaweza kuwashwa na radi, inauwasha kwa kutoa moto unaoshika mimea na vitu vikavu na kuviunguza.

Radi inatoa joto la kutosha kuwasha moto miti na chochote kikavu ambacho kinaweza kuungua na kuwa moja ya vyanzo vya moto asilia. 

Milipuko ya volkano inatajwa kuwa ni chanzo pia, Lava ya moto au uji mzito au mwepesi kutoka ndani ya miamba chini ya ardhi inaweza pia kusababisha moto. Unaposhika vitu vikavu huviwasha.

Kadhalika mlipuko wa  volkano unoambatana na cheche na moto  unawasha moto eneo jirani kwa kuunguza vitu vikavu au chochote kinachoweza kushika moto. 

Lakini, katika hali ya joto, hasa katika maeneo yenye ukavu mfano jangwani, mbuga au  nyika kulikojaa mimea na vitu vingi vikavu na hewa nyingi ya kaboni, moto wa asili unaweza kuzuka moja kwa moja na kuteteza  misitu, nyumba miundombinu na kukatisha maisha ya viumbe hai.

Kwa kurejea moto unaowaka Marekani kwenye jiji la pili kwa ukubwa la Los Angeles, BBC inasema maofisa wanataja upepo mkali na ukame katika eneo hili, umeifanya mimea kuwa mikavu na rahisi kuwaka moto, lakini pia  athari za mabadiliko ya tabianchi zinatajwa.

Hata hivyo, ingawa mazingira halisi bado hayajulikana, inaelezwa kuwa zaidi ya asilimia 95 ya matukio ya moto katika eneo hilo inaanzishwa na binadamu, kulingana na David Acuna, mkuu wa kikosi cha moto cha California.

Ingawa maofisa hawajatoa maelezo kamili kuhusu chanzo cha moto huu wa sasa, kipengele muhimu kilichotajwa katika kuenea kwa moto huo ni upepo wa Santa Ana, ambao unapuliza kutoka bara kuelekea pwani.

Unasafiri kwa kasi ya zaidi ya maili 60 kwa saa sawa na kilometa 97 kwa saa, inaaminika kuwa upepo huo umekuwa ukifanya moto kuzidi kuwaka na kuteketeza kazi zote zilizofanywa na binadamu.

Mabadiliko ya tabia nchi yamechangia, ingawa upepo mkali na ukosefu wa mvua vinachochea moto, wataalamu wanasema kuwa mabadiliko hayo yanabadilisha hali ya kawaida na kuongeza uwezekano wa milipuko kama hiyo ya moto kwa miaka mingi ijayo.

Utafiti wa serikali ya Marekani hauna shaka katika kuhusisha mabadiliko ya tabianchi na milipuko mikubwa na kali ya moto upande wa magharibi wa nchi hiyo, inasema BBC.

"Mabadiliko ya tabianchi, ikiwamo joto kali, ukame mrefu, na anga linayohitaji mvua, imekuwa kichocheo katika kuongezeka kwa hatari na ukubwa wa moto katika eneo hilo," inasema Idara ya Kitaifa ya Oceanic na Hali ya Hewa.

Baada ya msimu wa joto kali na ukosefu wa mvua katika miezi ya karibuni, California iko katika hatari kubwa, msimu wa moto kusini mwa California kawaida huaminika kuanza Mei hadi Oktoba, lakini Gavana wa jimbo hilo, Gavin Newsom, anaeleza mapema kuwa milipuko ya moto imekuwa tatizo la kila mwaka.

"Hakuna msimu wa moto," anasema ni  mwaka wa moto."

Akizungumza na BBC, Acuna anasema kuwa moto wa Palisades unatokea  mara ya tatu  katika miaka 30 iliyopita ambapo moto mkubwa umeibuka Januari mwaka huu.

Moto wa asili si jambo geni kwa Tanzania na itakumbukwa kwamba mwaka 2023 ulilipuka katika Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro na kuvuruga uoto wa asili na shughuli za kitalii pia.
Japo mara nyingi moto unahusishwa na moto wa asili.