Mbinu asili zinavyoepusha kemikali kwenye kilimo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:05 AM Feb 25 2025
Mbinu asili zinavyoepusha kemikali kwenye kilimo
Picha: Mtandao
Mbinu asili zinavyoepusha kemikali kwenye kilimo

TEKNOLOJIA asilia ni muhimu zama hizi ili kukabiliana na matumizi makubwa ya kemikali ambazo zinaelezwa kuwa zinaathiri kwenye bayoanui au viumbe hai.

Licha ya kwamba pengine hazipewi kipaumbele teknolojia asilia zina uwezo wa kuzalisha bidhaa zinazohuisha ardhi, kuboresha hali ya mazao na kuongeza uzalishaji na tija kwa mkulima.

Wakulima wengi wanaolima kwa ajili ya chakula wanategemea zaidi mbolea na viuatilifu asilia kutokana na gharama kubwa za bidhaa hizo, hivyo kuwa na umuhimu kwenye kuendeleza teknolojia asilia.

Kwa mfano, mkoani Singida wakulima wa kijijini Ilongero wanatumia teknolojia za asili kutengeneza mbolea na viuatilifu.

Wanatumia majani ya mapapai dume ambayo wanayatwanga na kuyaponda kikamilifu kisha kuweka vijiko kadhaa vya majivu ya kuni. 

Majivu hayo yanachekechwa kuondoa taka ambayo baada ya kuchanganywa na majani ya papai hulowekwa kwenye dumu la lita 20 kwa siku 21 au zaidi.

“Baada ya hapo tunachuja mchanganyiko na mfuko wa kiroba au nguo na kunyunyuzia mimea,” anasema Maria Mbura mkulima kutoka kijiji cha Ilongero.

Anasema wananyunyuzia mboga na mahindi kudhibiti visumbufu, aidha, wanalima mazao mbalimbali kama mahindi, maharage na mboga kwa kutumia teknolojia za asili.

Visumbufu wanavyo viangamiza ni pamoja na ‘katapila, funza au bora na kuvu, akisema wanaweza kunyunyuzi dawa hizo mara mbili kwa mwezi lakini wakati wa msimu wa mvua hutumika mara kwa mara.

Kadhalika wanalima kilimo mseto wakipanda mazao mbalimbali kwenye eneo moja kama mahindi, kunde, mbaazi na maboga.

Isitoshe, wanalima mboga za asili kama mnafu, matembele na mchicha.

Wanazalisha viazi vitamu pia, vyote vikitumia teknolojia ya asili mfano kurejeleza (regenerative technologies), mbinu asilia kuendeleza kilimo ambazo wakulima wanazitumia kuboresha uzalishaji.

Wanalima mboga za asili kama salada zinazooteshwa ndani ya maji au kando ya mito, au kwenye mifereji. Kadhalika hupanda mchicha wa kienyeji, kunde, jamii za mboga pori kama mashona nguo.

Wakulima hawa wanatumia mbinu nyingine ya kuchimba mitaro kuzuia mmomonyoko wa udongo kwenye miteremko ya milima. Wanatengeneza pia matuta (terraces) ya ulalo (horizontal) kuzuia mmomonyoko huo. 

Kwa upande wa mitaro wanayochimba wanaitumia kupitisha maji au kuchota maji kumwagilia mimea.

Aidha, hutumia mbinu za kuweka mazao yanayofunika udongo mfano maboga, jamii za maharage kitaalamu huitwa ‘cover cropping’.

Kadhalika wanatumia nyasi zenye harufu zinazofukuza wadudu waharibifu.

Huku matumizi ya dawa zenye kemikali kukabiliana na wadudu yakiwa kero kwa udongo na mazingira, wakulima hutumia teknolojia kukabili visumbufu.

Mchanganyiko wa pilipili kichaa zinazo changanywa na tura au ndulele zilizokomaa na kuwa na rangi ya njano ni dawa asili ya kuua wadudu ndani ya nafaka.

Wakulima kutoka kijiji cha Ngulu wilayani Mwanga mkoa wa Kilimanjaro wanasema viuatilifu hivyo huandaliwa kwa kukata vipande vidogo vya pilipili na tura, kuzianika ndani kusiko na mwanga wa jua na baada ya kukauka kuzitwanga, kuchekecha na kutumia unga wake kuhifadhi mahindi.

Wakulima hao huchanganya unga huo na mahindi, mtama au maharage na kuhifadhi kwenye mifuko kuzuia usibungue na pekecha au funza.

Mkulima anakadiria kiwango cha viuatilifu kulingana na kiasi cha mazao alicho nacho. Wanatumia majani ya mimea mingine kuua visimbufu mfano ‘Sesbania’ ambayo majani yake pia ni mbolea hai au ya kijani na pia husaidia kuongeza rutuba ya ardhi.

Pia wanatumia virutubisho vya majani kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi. 

Katika kijiji hicho wakulima wanatumia mbolea au samadi mbichi ya ng’ombe ambayo hujazwa kwenye kiroba na kufungwa kisha kutumbukizwa kwenye pipa la maji kwa siku 28.

Mkulima akiloweka mboleo hiyo inajichuja kutoka kwenye kiroba na kuingia kwenye maji ndani ya pipa ikitoa virutubisho vinavyohitajika.

Mtafiti Dk. Josaphat Ndakidemi, aliyehitimu kutoka Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela Arusha, anasema wanawahimiza wakulima kutwanga majani na kuloweka mchanganyiko wa dawa za asili kwenye maji kwa muda mrefu ili kuachilia dawa iliyoko kwenye mimea hiyo.

Anasema kadri majani au mimea inavyolowekwa kwenye maji ndivyo inavyomeng’enywa na kutoa kemikali asilia ya kuua visumbufu.

Aidha, anasema ni lazima kuponda au kutwanga majani mfano ya papai kikamilifu ili kuharakisha kumeng’enywa.

Anakumbusha kuwa mbolea na viuatilifu asilia vina faida kwa walaji na mazingira kwa sababu havidhuru bayoanuwai na pia huongeza uchavushaji mfano, huchochea mimea kutoa maua mengi yanayovutia nyuki, wanaosaka chavua na kuendeleza mchakato wa kuchavusha.