NI msiba mkubwa unaobeba sura ya kitaifa na kihistoria, Mkuu wa Majeshi Mstaafu, Jenerali David Musuguri anayetarajiwa kuzikwa Jumatatu wiki ijayo kijijini kwao Butiama, alikokuwa anaishi maisha yake ya ustaafu kwa miaka 36.
Uzalendo wake unatolewa mfano kila kona, ikiwamo kutoka kwa Mkuu wa Majeshi Mwasisi wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) mwaka 1964, Jenerali Mirisho Sarakikya.
Daima kabarikiwa kuishi umri miaka 104, akibaki na wasifu wake wa uzalendo na mtu wa watu, saa akishuka ngazi ya kijiji hasa.
Makazi yake ya ustaafu waliishi kijiji kimoja na baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere, yeye akimtangulia kiumri kwa miaka miwili na baada ya kustaafu walikuwa majirani kijijini, makazi yake na Nyerere wanatenganishwa na bonde fulani.
Hali ilivyo msiba wake wa leo, pia unawakumbusha wana Butiama, Mara, ugeni wa umati unaofika kwao kumuaga Mtanzania mwingine mzalendo aliyewatoka.
Ndio hali iliyotawala kwake Dar es Salaam, Mbezi kwa Msuguri, ukiwa ni ushuhuda wa Nipashe na taarifa kutoka kijijini Butiama, huku pilika za kitaifa ni nyingi, ratiba ya leo ya mazishi, Naibu Waziri Mkuu, Dotto Biteko anatarajiwa kuongoza utoaji wa heshima za mwisho kabla ya mwili kusafirisha kwenda Butiama.
Katika zama za uongozi wake 1980 hadi 1988, Jenerali Musuguri na viongozi wenzake wa juu kabisa jeshini watatu kuna wakati walijulikana kwa umaarufu wa masihara MML; kwa maana ya Musuguri, Meja Jenerali Martin Mwakalindile na Meja Jenerali James Luhanga.
KUTOKA BUTIAMA
Staili yake ya maisha kijijini inatajwa ni ileile ya mstaafu Nyerere, alivyoamua kurudi kuwa mkulima wa kawaida, miaka minne Nyerere akajikuta anamkaribisha Mkuu wa Majeshi mstaafu aliyesaidia ulinzi wake, pia kumtokomeza Adui Nduli Iddi Amin, wanaofahamiana vema, maana inaelezwa kihistoria walishahudhuria kozi za kijeshi pamoja.
Nipashe imezungumza na Katibu wa Ukoo wa Nyerere aliyejitambulisha kwa jina la Maghembe Jackton, anasema Musuguri amewahi kuwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Butiama kwa muda wa mwaka mmoja.
"Baada ya kustaafu , Musuguri, alirudi hapa Butiama, baada ya miaka michache akawa Mwenyekiti wa Kijiji kuanzia mwaka 1990 hadi 1991," anasema Jackton.
Pia, anasema, Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alimpendekeza ashike nafasi kwa muda mfupi kijijini, kabla ya uchaguzi, alipoona kijiji cha Butiama kinayumba kwa kukosa uongozi.
"Awali kijiji kilikuwa kinaongozwa na Joseph Nyerere (mdogo wa Mwalimu Nyerere) ambaye aliacha nafasi hiyo kutokana na sababu zilizo juu ya uwezo wake, hivyo kijiji kukosa mwenyekiti," anasimulia.
Katibu huyo wa Ukoo wa Nyerere, anasema mazingira hayo yalimfanya Baba wa Taifa amuombe Musuguri kushikilia nafasi hiyo na kukiweka kijiji katika mstari kwa mwaka mmoja, ndipo ukafuatia uchaguzi.
Anasema, Musuguri hakutaka kugombea nafasi hiyo, ingawa wananchi walikuwa wanamhitaji awe kiongozi wake, lakini akakataa kwa maelezo kwamba mwaka mmoja alioongoza unatosha.
Kwa muda huo, ameacha rekodi kuisaidia kufufua miradi ya kijiji ikiwamo duka la kijiji, mashamba, gereji, kiwanda cha mbao, pia akaimarisha umoja wa wananchi wa Butiama, uliokuwa umeyumba kutokana na kijiji kukosa uongozi kamili.
Anaongeza kuwa Musuguri alikuwa mtu wa karibu na wazee wenzake wa Butiama na alikuwa anashirikishwa katika mambo mbalimbali yakiwamo ya kimila ili kupata busara zake.
"Butiama wamepata pigo kubwa, kwani hapa tunapozungumza, watu wamefurika nyumbani kwake tangu wapate taarifa ya msiba, wanashinda hapo," anasema.
AMGOMEA MTOTO WA AMIN
Maghembe anaisimulia Nipashe, kwamba Musuguri alikuwa mtu mwenye msimamo usioyumba, akitoa mfano tukio la mwaka 2008, kwamba mtoto wa Rais wa zamani wa Uganda Nduli Idd Amin alipotaka kuonana naye.
"Sikumbuki jina lake, lakini alikuwa ni mtoto wa kiume ambaye alikuja Butiama nyumbani kwa Baba wa Taifa akazungumza na familia, pia alitamani kukutana na Musuguri ili wazungumze," anasema.
Katibu huyo anasimulia Musuguri alikataa kuonana na mtoto wa Amin akisema āhawezi kukaa pamoja na mtoto wa mtu ambaye aliua Watanzania kwa uvamizi wake mkoani Kagera.ā
"Nilikuwapo wakati mtoto huyo anafika kwa Baba wa Taifa, sikujua alitaka kuzungumza nini, lakini Musuguri alikataa kuonana naye akisema hataki kuonana na mtoto wa mtu aliyeua Watanzania," anasema.
Anaeleza kwamba Musuguri hakuwa mtu wa kuyumba na kwamba msimamo huo ulimfanya mtoto wa Amin aliyekaa siku moja, aondoke Butiama bila kuonana na mkuu wa huyo wa majeshi mstaafu.
Jackton anasema hilo ni miongoni mwa matukio ambayo hatayasahau katika maisha yake kuhusu Musuguri, kwa maelezo kwamba alishuhudia hatua kwa hatua jinsi ambavyo mtoto huyo aliomba waonane.
MTU WA WATU
Chifu Japhet Wanzagi, anamtaja Musuguri alikuwa mtu wa watu na mwadilifu, huku akifafanua kuwa nyumbani kwake kulikuwa kama ākituo cha kulelea watu kutoka mikoa mbalimbali.
"Nyumbani kwa Musuguri kulikuwa kama kituo cha kulelea watu, kwani kila siku walikuwa wanajaa kumwelezea shida mbalimbali ili awasaidie, kwani hakukuwa na kizuizi cha kuonana naye," anasema Chifu Wanzagi.
Anasema sio kwamba alikuwa na fedha nyingi za kuwagawia, bali ni roho ya utu aliokuwa nayo na kwamba alijitahidi kuhangaika huku na kule kumsaidia kila mmoja kadri inavyowezekana.
Chifu Wanzagi anaongeza kusema kuwa Musuguri hakuwa tayari kuona mtu anakosa fedha za kusafirisha maiti kutoka maeneo mengine kwenda Butiama badala yake alijitahidi kuhakikisha anapata gari la kubeba maiti.
"Lakini pamoja na wema wake huo, baadhi ya watu walifikia kudanganya wakawa wanaomba kiasi fulani cha fedha kwa ajili kujitibu au kununua vifaa vya shule na kumbe si kweli," anasema.
Aidha, anasema Musuguri alikuwa anaishi nje kidogo ya mji wa Butiama, na kwamba watu walikuwa huru kufika nyumbani kwake kucheza bao, na hivyo kuufanya mji wake kufurika watu kila siku.
Kwenye suala la uadilifu, anasema Musuguri alikuwa mwadilifu kama Baba wa Taifa, akifafanua kuwa hakujilimbizia mali, bali aliishi katika nyumba za kawaida alizojenga kijijini Butiama.
Anasema amejengewa nyumba nzuri wakati wa utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano na kwamba hata hivyo hakuishi muda mrefu katika nyumba hiyo kutokana na kusafiri sana kwa ajili ya matibabu.
AGAWIA MAJIRANI VIWANJA
Katika makazi yake mengine ya jijini Dar es Salaam, ambayo yapo eneo ambalo ni maarufu kwa jina la āKwa Musuguriā, Kamanda huyo mstaafu aliwahi kugawa viwanja vyake bure kwa baadhi ya majirani.
Mkazi wa Mbezi Kwa Msuguri anayejitambulisha kwa jina la Leonard Mbangile, anasema Msuguri ana eneo kubwa ambalo baadhi ya watu walikuwa wameanza ākujimegeaā kinyemela.
"Familia yake ambayo inaishi eneo hilo, ilimpa taarifa, akaja kutoka Butiama na kukuta baadhi ya watu wamejenga vibanda ambavyo si vya kudumu," anasema Mbangile.
Anaeleza baada ya mbabe huyo wa vita ya Uganda kufika, aliamua kuwamegea watu hao sehemu ya kiwanja chake, huku akisema kuwa hao ndio majira zake ambao ataishi nao.
Anasema, alifanya tukio ambalo watu wengi walibaki wana shangaa, kwa kuwa walitarajia angewafukuza au kuwachukulia hatua za kisheria kwa kuvamia kiwanja chake, lakini akaonyesha uungwana.
"Mzee Msuguri alikuwa mnyenyekevu na msikivu, hatukukosea kumpa heshima ya kutumia jina lake kuliita eneo hili Kwa Msuguri tangu mwaka 1980 hadi leo limeendelea kuwa maarufu," anasema.
SIRI YA MAISHA MAREFU
Msemaji wa Ukoo a Nyerere, anamwelezea, alikuwa ni mtu wa mazoezi, kwani alikuwa anatembea kila akitoka nyumbani kwake katika kitongoji cha Kitanga kwenda Senta au shambani.
Anaeleza alikuwa na mashamba, pia ng'ombe wengi wa kienyeji na kisasa,
na alipendelea chakula cha kabila lake la Kizanaki ambacho ni ugali wa muhogo na mboga za majani, maziwa na nyama.
"Vilevile alikuwa anapenda kunywa uji wa ulevi, kwa mtindo huo wa maisha, ninaamini umechangia kumfanya aishi miaka mingi," anasema.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED