Madereva hawana elimu kutoa huduma ya kwanza, kuwafunza sheria za usalama, kuhudumia majeruhi

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 07:57 AM Oct 01 2024
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Dinnah Mosy, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo.
PICHA: SABATO KASIKA
Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi, Dinnah Mosy, akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo.

UKOSEFU wa elimu ya usalama barabarani kwa baadhi ya watumiaji wa vyombo vya moto, ni moja ya visababishi vya ajali zinazoendelea kuripotiwa kila wakati.

Ni kwa mujibu wa Kitengo cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi kinachofafanua zaidi kuwa pamoja na ukosefu wa elimu hiyo, kupuuza na kutokufuata sheria za usalama barabarani nalo ni tatizo.
 
 Mkuu wa Mafunzo Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Dinaah Mosy, anasema jeshi hilo mara kwa mara linatoa elimu kuhusu utii wa sheria za usalama barabarani.
 
 Anafafanua kuwa pamoja na juhudi hizo wapo baadhi ya madereva wa bodaboda ambao hawana nidhamu wala hawazingatii sheria ambazo pia zinawaelekeza kwenda kusomea udereva.
 
 "Licha ya jeshi kuwaelimisha, baadhi yao hawazingatii, wapo wanaojifunza udereva usiku vichochoroni, kisha asubuhi wanaingia barabarani kubeba abiria," anasema Dinnah.
 
 Dinnah anasema hatua hiyo inahatarisha maisha yao na ya abiria kila wanapotoa huduma na kuongeza wingi wa ajali ambazo kuanzia Juni mwaka 2023 hadi Julai mwaka huu zimefikia 163,148, huku asilimia 61 ya majeruhi wakiwa ni wa bodaboda.
 
 Anasema hayo ni kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. John Jingu , wakati akizungumza katika semina na wadau wa usafirishaji inayofanyika jijini Dodoma hivi karibuni.
 
 Lakini Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyama vya Madereva wa  Bodaboda na Bajaj mkoa wa Dar es Salaam na Taifa, Said Kagoma, anasema tatizo la kukimbia mafunzo linatokana na gharama kubwa wanachama wake wanazotozwa ili kujifunza taalamu hiyo.
 
 Anasema kwa Dar es Salaam kuna madereva zaidi ya 200,000, wakati kitaifa kuna madereva zaidi 2,000,000 na kufafanua kuwa chanzo cha madereva wengi kujifunzia udereva uchochoroni ni ada kubwa inayoanzia Sh. 180,000 kwa mwezi wanayolipa vyuoni.
  
 "Kama vyuo vya udereva kama VETA Chang'ombe na Buza vyote vya Dar es Salaam, Vikindu na Kibaha mkoani Pwani, ambavyo tunasoma kwa miezi mitatu kabla ya kuingia barabarani, gharama zake ni hizo ambazo hatuwezi kumudu  tutasemaje sisi wanyonge," anasema.
 
 Anafafanua kuwa, kwa siku dereva anaweza kupata Shilingi 25,000 hadi 30,000 na kupeleka kwa bosi Shilingi 10,000 au 12,000 kisha anatoa pesa ya mafuta 7,000 na kubakiwa na kiasi kidogo.
 
 "Kinachobaki hakiwezi kutosha matumizi ya nyumbani na kulipia ada ya kujifunza udereva, ndio maana tunaomba tupunguziwe, ili wengi wasome na waweze kufanya kazi yao kwa weledi," anasema.
 Kagoma anasema, wao hawawezi kujilinganisha na madereva wa Bolt au Farasi, kwa maelezo kuwa wenzao hao wanafanya kazi kwa mtandao, tofauti na wao (bodaboda), wanaoshinda sehemu moja wakisubiri abiria.
 "Kwanza wenzetu hao hawakamatwi kama sisi, lakini pia wanazunguka jiji zima bila usumbufu, kwani wanaweza kufikisha abiria sehemu fulani wakaitwa sehemu. Hivyo nzima wanakuwa na abiria ingawa sijui wanaingiza kiasi gani cha fedha kwa kutwa," anasema.
 
 RED CROSS KAZINI
 
 Kutokana na upungufu na hatari hiyo inayojitokeza, Chama cha Msalaba Mwekundi Tanzania (Red Cross), kinakusudia kuwaelimisha madereva wa bodaboda wa  Dar es Salaam katika jitihada za kupunguza ajali hizo.
 
 Mkurugenzi wa Maendeleo ya Matawi ya Red Cross Tanzania, Reginald Muhango , anasema na kuongeza kuwa chama kitaanza kutoa elimu itakayoambatana na mafunzo ya huduma ya kwanza.
 
 Anasema ni jukumu linaloanza mwezi huu hadi Desemba, wakishrikiana na wadau mbalimbali, wakiwamo polisi na kiwanda cha bia cha TBL wanaofadhili mradi huo.
 
 Muhongo anaeleza hayo wakati wa uzinduzi wa mpango wa kutoa mafunzo kwa madereva hao wiki iliyopita. Kwamba watajikita zaidi kwenye mafunzo ya kutoa huduma ya kwanza huku kikosi cha usalama barabarani wakifundisha udereva na sheria ya usalama barabarani.
 
 Anaeleza kuwa pamoja na madereva wengi kutozingatia sheria za usalama barabarani, wamegundua kuwa kuna tatizo kwenye kusaidia wanaojeruhiwa kwenye huduma ya kwanza inapotokea ajali na sasa wanakwenda kulifanyia kazi kupitia elimu watakayotoa.
 
 "Tunakwenda kuwaelimisha ili wanapopata ajali au wakikuta mtu amepata ajali wajue jinsi ya kumhudumia kabla ya kumfikisha hospitalini. Wengi wakifika eneo la ajali  hushangaa  badala ya kutoa huduma kwa majeruhi," anasema Muhango.
 
    RED CROSS WANACHOLENGA
 
 Anasema, elimu hiyo itaanza kutolewa wakati wowote kuanzia mwezi huu kwa kushirikisha madereva wa bodaboda, viongozi  wa serikali za mitaa, kata tarafa, wilaya hadi mkoa, kupitia mikutano.
 
 "Tutafika wilaya zote tano za Dar es Salaam na kuitisha mikutano kwa ajili ya kutoa elimu kwa madereva huku viongozi wao na wa serikali wakishiriki, kwani nao wanatakiwa kupata elimu hii," anasema Muhango.
 
 Mkufunzi wa Huduma ya Kwanza wa Msalaba Mwekundu, Peter Bongo, anasema, chama hicho kimegundua kuwa madereva wa boda na abiria wao hawafahamu jinsi ya kutoa huduma ya kwanza wakati wa ajali.
 
 Anasema kabla ya kutoa huduma cha kwanza ni kujali usalama wa wote mtoa huduma na majeruhi na wengine walio katika tukio na kwamba mara nyingi unapotokea ajali, watu hukusanyika bila tahadhari.
 
 Bongo anasema hakikishi mazingira yako salama, huku akiongeza kuwa katika mazingira hayo, inaweza kutokea ajali nyingine, hivyo, mtoa huduma anatakiwa kuwaelekeza watu wawe makini wasije kuumia tena.
 
 "Baada ya kujihakikishia usalama, ataomba msaada wa usafiri kisha mtoa huduma ya kwanza atamfanyia tathmini majeruhi kujua ana tatizo gani kwani ni muhimu kutoa huduma baada ya kujua ukubwa wa tatizo  ili iwe rahisi kumhudumia," anasema Bongo.
 
 Mkufunzi huyo anasema kinachofuata ni kuanza kutoa huduma ya kwanza na kwamba ni lazima ifanyike haraka  kuokoa maisha ya majeruhi.
 
 "Madereva wengi hawana elimu mfano  kumbeba majeruhi asiumie zaidi. Hivyo, Red Cross tunakwenda kuwaelimisha, wajue jinsi ya kutoa huduma ya kwanza," anasema.