Madaktari wanawake waja kimkakati kukabili unyanyasaji kijinsia, afya akili

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:27 AM Oct 08 2024
Dk. Zeitun Bokhary (wa pili kushoto) pamoja na mwasisi wa MEWATA, Prof. Ester Mwaikambo (kushoto) na  madaktari wengine, wakati wa Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Afya, uliomalizika  Zanzibar.
PICHA: MEWATA
Dk. Zeitun Bokhary (wa pili kushoto) pamoja na mwasisi wa MEWATA, Prof. Ester Mwaikambo (kushoto) na madaktari wengine, wakati wa Mkutano Mkuu wa Kitaifa wa Afya, uliomalizika Zanzibar.

TANZANIA Bara hadi Visiwani, ukatili wa kijinsia kwa jinsi zote ni janga, serikali na wadau wanashirikiana kukabiliana na balaa hilo la mmomonyoko wa maadili linalowaumiza zaidi watoto wa kike, wakiume na wanawake wakiwamo vikongwe.

Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA), ni miongoni mwa mashiriki yanayopambana na ukatili huo, na hivi karibuni Dk. Zeitun Bokhary, rais wa MEWATA, anakiri kuwa jinsi zote zinaathirika na lazima kuchukua hatua na kusimama pamoja kuwalinda dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia. 

Ni katika mahojiano na Nipashe jijini Dar es Salaam, anapoeleza kuwa unyanyasaji unaumiza wote na MEWATA inaliona kuwa ni tatizo la kitaifa na imeanza kutoa elimu kwa umma ili watambua kuwa wamiliki na wenye mamlaka ya miili na maisha yao. Kama anavyosimulia zaidi… 

SWALI: Mnachukua hatua gani tofauti na juhudi nyingi zinazofanyika?

JIBU: Tunafika shuleni kuwafundisha wanafunzi wajitambue kuwa miili yao zikiwamo sehemu za siri ni mali yao hakuna yeyote anayeruhusiwa kuwagusa au kuziona.

Wanatakiwa kufahamu hayo kwa kuwa ndiyo mwanzo wa kuwanyanyasa. Mathalani, tunawaeleza umuhimu wa viungo hivyo, pamoja na matumizi ya miili yao mfano sehemu za siri na matiti. Tunawaambia ni wakati upi vitatumika, siyo sasa wakiwa watoto. Tunawaelimisha kuwa miili yao si ya kuchezewa na  mtu mwingine na wasiruhusu, walipinge na kutoa taarifa za wanyanyasaji.

 Tunawafundisha kuhusu kudanganywa na watu wanaowahadaa kutumia simu na  kuwarekodi na kuwapiga picha zinazosambazwa mitandaoni. Kingine ni aina za unyanyasaji kama kulazimishiwa kuolewa, kutumikishwa kwenye ajira.

 Pamoja na kuelimisha hatari za ukatili wa kijinsia, tunawekeza pia kwenye kutoa elimu ya kufahamu na kutibu matatizo ya afya ya akili kwa watoto. Tumegundua kuwa  linaathiri maendeleo darasani na ndani ya jamii.

 Kadhalika, tunawahamasisha mabinti kusoma masomo ya sayansi ili kuwa na idadi kubwa ya wataalamu wanawake kwenye sayansi na  kiteknolojia, kuanzia madaktari, wahandisi, mabingwa wa upasuaji, marubani na manahodha.

 Tunahamasisha hivyo ili kuondoa pengo la jinsia kwenye sekta ya sayansi na teknolojia kwa kuongeza wanawake kwenye kazi ambazo zinaaminika kuwa hawaziwezi.

  SWALI: Maono ya MEWATA ni kuwa na  Watanzania wenye afya bora wanaopata huduma bora, nafuu na endelevu kupitia mifumo bora inayoamini. Juhudi hizo zimefikia wapi?

JIBU: Harakati za chama tangu kilipoanzishwa  ni  kuwa na jamii yenye afya bora na kuhudumiwa kwa ubora.

Itakumbukwa kuwa miongoni mwa wataalamu wa afya walioasisi kampeni za kuelimisha jamii kutambua na kutibu saratani ya matiti na shingo ya kizazi ni sisi chama cha madaktari wanawake na sasa juhudi zinaendelea.

Tangu mwanzo kampeni na hamasa zimefanyika na kuwafikia wanawake  karibu Tanzania nzima kuelezea kuzitambua dalili na kutibu magonjwa ya saratani ya matiti na shingo ya kizazi.

Wanawake wengi wanajitokeza wanafuatilia afya ya matiti na shingo ya kizazi. Itakumbukwa kwamba kwa kufanya uchunguzi (screening), kinamama wengi wenye dalili waligundulika na kutibiwa.

Licha ya kwamba walikuwa wana dalili hawakuzifahamu lakini kampeni na uchunguzi wa MEWATA ulifanikisha kuwatambua, kutibiwa mapema na kupona.

Kampeni zinaendelea na kukumbusha kuwa saratani ikigundulika mapema inatibika na kuwashauri kujichunguza, kushiriki kampeni kila zinapotangazwa na kuwahi hospitalini.

Tunawakumbusha kuwa Oktoba ni mwezi wa kuhamasisha uelewa, kuchukua hatua na kutiba saratani ya matiti, nasi tutaendelea na jukumu hilo.

 Watanzania wafahamu kuwa changamoto kubwa ya saratani ni kuchelewa kuigundua na kuanza tiba mapema.

Pamoja na kuwaeleza na kuwachunguza saratani za matiti na shingo ya kizazi tunawafahamisha kuhusu mambo yanayochangia kupata maradhi hayo kama kutumia tumbaku, vilevi, dawa za kulevya ili kujiepusha.

SWALI: Tueleze kuhusu harakati za MEWATA Zanzibar.

JIBU: Kwa karibu miongo mitatu kazi za MEWATA zilifanyika zaidi Bara, lakini mwaka huu tumeanzisha tawi Zanzibar.

Tumefungua tawi Zanzibar wiki iliyopita tukiwa na wanachama zaidi ya 20 ambao ni pamoja na mabingwa wa watoto, wanawake, wapasuaji na kwa ujumla MEWATA sasa iko Bara na Visiwani. 

Kwa mara ya kwanza tumepokea wanachama wapya madaktari wanawake Zanzibar, ni tukio la kihistoria MEWATA mwaka 2024 imeandika rekodi, tutashirikiana nao kwenye kufikia maono yetu.

Ni matokeo ya Mkutano Mkuu wa Afya (Tanzania Healthy Summit) uliofanyika karibuni.

SWALI: Unazungumziaje wanachama na idadi ya madaktari wanawake kitaifa sasa?

JIBU: Kwa ujumla idadi ya wanachama inaongezeka kama madaktari wanavyoongezeka pia, tupo takribani wana MEWATA 500 wakiwamo wanachama hai wanaolipa michango na ada za chama, tunafikia 250. Lakini tunao  wengine wasio hai.

Idadi ya wanawake madaktari pia inaongezeka ikilinganishwa na ilivyokuwa hapo awali. Wasichana wanasoma sayansi na wanaoingia kwenye fani ya tiba siyo kama zamani miaka ya 1990 wanazidi kuongezeka.

SWALI: Ni nini ujumbe wako kwa jamii na serikali?

JIBU: Kinamama tujali afya ya uzazi na uzazi salama. Tanzania imepunguza idadi ya vifo vya wazazi kutoka 500 kwa kila vizazi hai 100,000 hadi kufikia wastani wa vifo 100.

Tunawahimiza wajawazito kuhudhuria kliniki na kupata matibabu, ushauri, maelekezo na mafundisho na kuyafuata.

Wajawazito wasijifungulie nyumbani, wafike kwenye vituo vya afya kupata matibabu, kwa kufanya hivyo itapunguza vifo vya wajawazito, na watoto wachanga.

Tunaishauri jamii kusoma taarifa mbalimbali za kiafya  aidha majarida, magazeti, vipeperushi vya kiafya na pia mabango na ujumbe unaoweka kwenye huduma za afya.

Watu wazingatie lishe bora, afya ya akili, tiba, chanjo magonjwa ya milipuko na kutafuta tiba sahihi, ikumbukwe afya ni mtaji wa kwanza kwenye kila kitu.

Kadhalika sekta ya afya imekuwa na mafanikio makubwa, serikali imejenga miundombinu bora vijijini na sehemu nyingi hata za vitongoji vya ndani zaidi, leo zina huduma za afya karibu na wananchi.

Tunampongeza Rais Dk. Samia Suluhu Hassan  kuboresha  afya ya wananchi na serikali bado inaendelea.