KILIO UVAMIZI TEMBO KUSINI... Agizo lake Rais Septemba hitaji la ‘ndege nyuki’, TAWA wameanza nalo

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:16 AM Nov 01 2024

Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mabula Nyanda.
PICHA: MTANDAO.
Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mabula Nyanda.

MIKOA kadhaa nchini na wilaya zake zikiwamo Liwale na Nachingwea (Lindi), pia Tunduru ya Ruvuma, ambazo ziko katika ukanda mmoja, kuna historia ya suala la uvamizi wa tembo mashambani na makazi ya watu limezidi.

Inaelezwa hali hiyo yenye kipindi kirefu, mathalan Nachingwea ni mwaka wa tatu sasa, inaathiri usalama wa makazi na uzalishaji mashambani, pia kukwama.

Agosti mwaka jana ilitoa sauti ya kifo huko Nachingwea, hata kuvuta hisia za kitaifa, huku Mkuu wa Wilaya hiyo, Mohamed Moyo, akiripotiwa ahadi yake serikali ingetumia ndege za helikopta kuwafukuza.

Rais Dk. Samia Suluhu Hassan akiwa ziarani wilayani Tunduru mwezi uliopita, sauti hiyo ya kilio cha uvamizi wa wanyama waharibifu akawasilishiwa tena, hata akaielekeza Wizara ya Maliasili kuongeza ndege nyuki (drones) kutekeleza kazi hiyo.

Akizungumza na wananchi wa Tunduru kwa nyakati tofauti katika ziara yake ya siku ya nne mkoani Ruvuma, Rais Dk. Samia akataja mikakati inayofanyika inajumuisha kuongeza askari wa wanyamapori na kuwaongezea ujuzi walioko vijijini, ili washirikiane kuwadhibiti tembo.

Akasema, serikali imeweka magari ya doria katika maeneo mbalimbali wilayani, kurahisisha shughuli hiyo, pia ndege nyuki ya kufukuza tembo, hatua inayofika pia wilayani Namtumbo.

“Tunajua kuna tatizo la tembo, lakini tumeanza kuchukua jitihada hizo na mengine yanafuatia, lengo letu ni kuongeza idadi ya ndege nyuki ili kufukuza tembo na kuimarisha vituo vya askari wa maliasili,” akasema Rais Dk. Samia, mkutanoni katika uwanja wa Majimaji mjini Songea.

WATEKELEZA MAAGIZO

Ni wastani wa wiki mbili na nusu baadaye (Oktoba 15), hatua za kiserikali zikaanza kushuhudiwa, pale Kamishna wa Uhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), Mabula Nyanda, anapotangaza hatua kadhaa kukabili wanyamapori wakali na waharibifu, hususan tembo katika mikoa ya Ruvuma na Lindi. 

Hivi sasa, serikali kupitia TAWA imetenga bajeti ya kwa ajili ya kununua ndege nyuki nne aina ya DJI Mavic 3 zitakazopelekwa wilayani Namtumbo (Ruvuma) na Liwale, Nachingwea na Lindi mkoani Lindi.

Kamishna Mabula, anayasema hayo mbele ya anayeongoza Kamati ay Ulinzi na Usalama, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas Ahmed, ikiwa ni utakelezaji wa maelekezo ya Rais Dk. Samia, aliyoyatoa mkoani humo Septemba 28, 2024 kuhusu udhibiti wa wanyamapori wakali na waharibifu katika wilaya za Namtumbo na Tunduru.

Mabula anasema katika mwaka wa fedha uliopo 2024/25, TAWA inatarajia kuajiri askari 351 watakaopangiwa vituo vilivyoko kwenye maeneo yenye changamoto kubwa ya wanyamapori hao.

Pia anataja, kuna askari 20 watapangiwa katika kituo kidogo cha Songea na watafanya kazi katika wilaya za Tunduru na Namtumbo, kunakotajwa kuwa na changamoto kubwa ya wanyamapori wakali na waharibifu.

Vilevile, Kamishna Mabula anasisitiza TAWA inatarajia kununua gari moja na pikipiki mbili zitakazopelekwa katika kituo kidogo cha Songea, kutumika kudhibiti changamoto ya wanyamapori wilaya za Tunduru na Namtumbo.

Pia, anasema mamlaka tajwa itaboresha kituo kimoja cha Askari cha Kudumu katika wilaya ya Tunduru, pia vikosi viwili vya kudumu vya askari kutoka kituo kidogo cha Songea, ili kurahisisha mwitikio wa haraka wa matukio ya tembo.

Anasema, baada ya changamoto ya wanyamapori wakali na waharibifu kuwa endelevu, Wizara ya Maliasili na Utalii imeandaa mkakati wa kukabiliana na migongano hiyo, baina ya binadamu na wanyamapori wakali na waharibifu.

Ni mkakati anaoutaja kutekelezwa na taasisi za wizara zilizo chini ya Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu (TAWA, TANAPA, NCAA na TFS) kwa kugawana maeneo, halmashauri za wilaya, taasisi zisizo za kiserikali, wadau wa uhifadhi na wananchi kwa ujumla.

BUSTANI WANYAMAPORI

Aidha, Kamishna Mabula anasema, kuwapo bustani ya wanyamapori (zoo) hai inayosimamiwa, huko Ruhila katika Manispaa ya Songea, ikitajwa ni kivutio kwa wakazi mkoani humo, Kamishna Mabula amemwomba Mkuu wa Mkoa - Kanali Ahmed kusaidia ujenzi wake kiwango cha lami urefu wa kilomita tano kufika mahali hapo, kukiwa kivutio cha utalii.

Kanali Ahmed anapongeza Kamishna Mabula, kuzingatia na kutekeleza maagizo ya Rais kwenye ziara yake mkoani humo, mwezi uliopita.

Mkuu wa Mkoa, pia anasema jitihada za TAWA zinahuisha matumaini ya wananchi wa Ruvuma, kwa kuwa zinalenga kuimarisha usalama wa maisha na mali zao, dhidi ya uvamizi wa wanyamapori kwenye maeneo yao.