Kijiji kilichokosa daraja tangu uhuru sasa chakumbukwa

By Jumbe Ismaily , Nipashe
Published at 07:08 AM Sep 04 2024

Mto Mwandile unaotarajiwa kujengewa daraja.
PICHA: JUMBE ISMALY
Mto Mwandile unaotarajiwa kujengewa daraja.

MOJA ya sababu zinazochangia kupanda gharama za maisha ya wananchi ni uharibifu wa miundombinu ya barabara, madaraja na vivuko kila wakati wa msimu wa mvua, iwe masika au vuli.

Pamoja na kupanda gharama za maisha vile vile husababisha baadhi ya huduma za kijamii kama afya, elimu kukosekana, au kutokupatikana kwa urahisi huku wajawazito na watoto wakipoteza maisha wakati wa kujifungua.

Kijiji cha Ntumbi wilayani Manyoni Mkoa wa Singida ni miongoni mwa maeneo ambayo tangu uhuru hayajawahi kubaki salama. 

Changamoto haziishii hapo wengine wanasombwa na maji wakijaribu kuvuka  mito kuwahi hospitalini.

Hata hivyo juhudi zimeanza kuwakwamua na kuwaondoa wasiwe maeneo yasiyofikika kirahisi kutokana na kuharibika kwa daraja la Mto Mwandile. Tayari kwa  mujibu wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini (TARURA) Manyoni, serikali imetenga Shilingi milioni  415 kwa ajili ya daraja jipya litakalojengwa katika Mto Mwandile.

Taarifa za TARURA wilaya zinasema daraja hilo litakapokamilika litawanufaisha wananchi kwa kuwarahisishia upatikanaji wa huduma za kijamii.

Akiwa katika ziara za kukagua miradi ya maendeleo ya kata ya Nkonko, diwani wake Ezekiel Samwel, anashuhudia ujenzi wa daraja la Mto Mwandile unaoendelea, kuwaondolea adha wananchi wa eneo hilo.

Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Nkonko na Ntumbi, wanasema changamoto zilizokuwa zikiwakabili kwa kukosa usafiri wa uhakika kukosa fedha na kupanda gharama za maisha kutokana na bei za bidhaa kuwa juu.

Wanasema ujenzi wa daraja hilo linalojengwa na mkandarasi mzawa, utawaondolea kero ya ukosefu wa usafiri na kurahisisha usafirishaji wa mazao ya kilimo, mifugo na wananchi.

Wanavijiji hao wanaipongeza serikali kwa mradi huo wa kuwaboreshea miundombinu hasa  barabara na daraja ambao utaunganisha kata za Nkonko, Sanza, Iseke na makao makuu ya wilaya ya Manyoni.

Wanapongeza kwa kuwaangalia wakijiita kuwa ni watu wa hali ya chini ambao wanaathirika kwa kukosa barabara na madaraja yanayopitika wakati wote wa mwaka.

John Mnyama mkazi wa Kijiji cha Nkonko anasema tangu uhuru mwaka 1961 wananchi wa vijiji vya Ntumbi na Ipanduka hawakuwa na miundombinu bora ya barabara, hivyo kupata shida kufikia huduma za kijamii kama hospitali na masoko.

Mnyama anawaasa wanufaika wa daraja hilo kuendelea kutoa ushirikiano kwa serikali ambayo imetoa fedha kwenye miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao. Mhandisi mjenzi wa daraja hilo, James Malisa anasema mradi wa daraja la Nkonko -Ntumbi una awamu mbili ambazo ni  kipande cha Nkonko Ntumbi na kingine kipo upande wa Itagata, lakini kwa sasa wanaanza na ujenzi wa daraja. Anasema mradi huo uliosainiwa Mei mwaka huu utakapokamilika utagharimu Shilingi milioni 415 na unatarajiwa kukamilika Novemba mwaka huu. Anatoa wito kwa watumiaji wa daraja hilo kwamba baada ya kukamilika kwake walitunze kwa sababu serikali imewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa daraja hilo.

Diwani wa Kata ya Nkonko, Ezekieli Samweli anasema wanufaika wakubwa wa daraja hilo ni wanakijiji cha Ntumbi chenye  wakazi takribani  8,000. Anasema kutokana na kutopitika kwa barabara hiyo  gharama za vitu madukani zimepanda na kusababisha ugumu wa maisha kwa wananchi, hususani wakazi wa Ntumbi pamoja na vijiji vya kata jirani ya Iseke.

Diwani wa Viti Maalumu (CCM) Tarafa ya Nkonko, Rehema Chuji, anasema kabla ya kuanza kujengwa kwa daraja hilo, kulikuwa na changamoto kwa kinamama siku za kujifungua maji yanapokuwa yamejaa kwenye mto huo walikuwa wanahangaika kupita. Kata ya Nkonko ina kituo cha afya kinachotegemewa pia na wanakijiji cha Ntumbi kupata huduma za afya kilichopo Nkonko na inapofika masika, kina mama wanaokwenda Nkonko wanakutana na changamoto mara nyingi na hata wengine kupoteza maisha. Mwaka 2023 kuna mama alipoteza maisha akitokea Ntumbi kwa ajili ya kufuata huduma ya kujifungua katika kituo cha afya Nkonko. Aidha, mwaka 2022 kina mama wawili na baba mmoja walipofika kwenye mto huo walizama.

Pamoja na hayo maharusi wawili waliokuwa wametoka kufunga ndoa  walipozama wakati wakipita kwenye mto huo.

Wawili hao walisombwa na maji na hivyo kupoteza maisha, Rehema akitoa  wito kwa wanaotumia  barabara na daraja, hususani wakazi wa Ntumbi, Nkonko na Mwandile waendelee kutunza miundombinu hiyo.

Anawataka wafanyakazi wa kujitolea, washirikiane na mkandarasi mjenzi kwenye eneo la mradi kwa ajili ya kutengeneza daraja madhubuti.

Meneja wa Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini (TARURA) Wilaya ya Manyoni, Stephen  Nyanda,  anasema wilaya hiyo  inahitaji takribani Shilingi bilioni 18 kukamilisha changamoto za miundombinu yote ya barabara. Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Manyoni, Annastazia Tutuba, anasema ujenzi wa daraja hilo utafungua mawasiliano na kurahisisha wakulima wa mazao ya biashara katika kata hiyo kutoka na kuingia ndani na nje ya kata hiyo.