ZIKIWA zimesalia siku 20 kufikia uchaguzi wa viongozi wa kitaifa wa CHADEMA, mwenyekiti Freeman Mbowe na Makamu Tundu Lissu, anayetaka kumrithi, agenda zao kuu ni tatu.
Kudai katiba mpya, mifumo huru ya uchaguzi na sheria rafiki za kusimamia uchaguzi, ndiyo madai yanayobebwa na Mwenyekiti Taifa, Mbowe na Makamu Lissu.
Wote wamebeba agenda hizo lakini kila mmoja ana mipango ya namna ya kuyadai kwa watawala.
Lissu anayetaka kuwa bosi namba moja kutoka namba mbili aliko hivi sasa, haamini sana katika maridhiano bali anategemea kuona agenda hizo zinapata majibu kwa njia anayoeleza ni ya mazingira ya sasa ya kisiasa.
Mbali na mambo hayo matatu, Lissu anataka aifumue katiba ya CHADEMA ili kuweka kikomo cha uongozi ndani ya chama na ule wa ubunge wa viti maalum na udiwani.
Anasema anataka aanze kufanya mabadiliko kuanzia ndani ya chama kwenye mifumo ya uchaguzi, ili madai ya uchaguzi huru wa nchi yawe na tija zaidi.
“Kipindi cha siasa ngumu kinahitaji watu wagumu. Wanaoweza kusimama hadharani wakasema maneno yanayostahili. Wenye msimamo wa kuaminika, uadilifu usiokuwa na shaka. Huu ni muda sahihi kwangu kugombea nafasi ya Mwenyekiti,” anasema Lissu.
Msimamo wa Lissu kutoamini katika maridhiano ni kile anachosema kwamba CCM, kwa upande mmoja na serikali kwa upande mwingine, hawako tayari kupata muafaka wa kitaifa kwa kile anachoona, mifumo na katiba iliyopo inakinufaisha zaidi chama hicho.
Hiyo ndiyo sababu inayomfanya tangu mwanzo, kupinga mazungumzo ya maridhiano kati ya CHADEMA, CCM na serikali, anasema Lissu.
“Nilimpinga Mbowe, kwenye maridhiano na baadaye akasema mwenyewe wenzake waliompinga, walikuwa sahihi. Tungeimba wote wimbo wa maridhiano, tungekuwa wapi leo. Tuwe na ujasiri wa kusema hii haiko sawa hata kama inasemwa na wakubwa zetu,” anasisitiza.
MWENYEKITI MBOWE
Anaamini katika maridhiano na kwamba njia hiyo itasaidia kuunganisha makundi yote katika jamii.
Hata hivyo, anatofautiana na Lissu kuhusu marekebisho ya katiba ya CHADEMA ili iendane na mazingira ya sasa, akieleza kuwa hilo linaweza kujadiliwa ndani ya vikao vya chama na si kwenye majukwaa ya kisiasa.
Mbowe anasema ili hoja tatu kuu za chama hicho zipate muafaka wa kitaifa, zinahitaji ushirikiano wa wanasiasa, asasi za kiraia, wanazuoni, viongozi wa dini, wasomi na mwananchi mmoja mmoja.
Msimamo wake anauweka kwa kauli yake alipokwenda kuchukua fomu akisema:
“Tunahitaji katiba kwa kucheza miguu yote, ya diplomasia, ushirikishwaji, barabara na kila silaha itumike. Na hii ni ajenda ya msingi katika chama chetu.”
Katika kujenga msingi wa msimamo wake, ananukuu kauli 10 za viongozi mashuhuri duniani, akiwamo Hayati Nelson Mandela aliyekuwa mpigania uhuru na rais wa Afrika Kusini, Makatibu Wakuu wastaafu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-Moon na Koffi Anan, marais wa Marekani, Jonh Kennedy na Barack Obama, Kansela mstaafu wa Ujerumani, Angela Markel, Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Winston Churchil na Waziri Mkuu wa India, Mahatma Gandhi, ambao kwa nyakati mbalimbali walihimiza umuhimu wa meza ya maridhiano hasa kunapotokea tofauti kubwa za kisiasa.
Raia hao wa dunia, walinukuliwa kwa nyakati tofauti wakieleza kuwa mazungumzo yanafanywa na watu jasiri walio tayari kupoteza kidogo ili wapate kikubwa chenye maslahi ya umma.
Anaona kwamba licha ya mazungumzo kati ya CHADEMA na CCM kukwama, chama hicho kikuu cha upinzani kilipata mafanikio makubwa ikiwamo kufunguliwa kwa mikutano iliyokiwezesha kusajili wanachama nchi nzima, kufanya uchaguzi wa ngazi zote na kufutwa kwa kesi zaidi ya 400 zilizokuwa zimebambikiwa kwa viongozi na makada wake, maeneo mbalimbali, kurejea nchini kwa viongozi waliokuwa wamekimbilia ughaibuni na kulipwa haki yao ya ruzuku ya chama iliyokuwa imezuiwa kwa miaka miwili.
Anaamini kwamba hata sasa, chama hicho kimefanikiwa kufanya uchaguzi katika ngazi mbalimbali, kutokana na maridhiano, ambayo yalifanikisha kufuta katazo haramu la miaka saba la kuzuia mikutano ya vyama vya siasa.
“Maridhiano si jambo jepesi, lakini ni kitu kisichoepukika kwenye siasa duniani kote. Makundi mbalimbali yanachukua upande wa maridhiano kutokana kile inachotamani,” anasema.
“Ninajivunia sana mazungumzo na uamuzi wetu wa kuingia kwenye maridhiano.”
KURA MITANDAONI
Wakati viongozi hao wakichuana, hali ni hiyo hiyo mitandaoni kila upande ukieleza sababu za kumuunga Lissu au Mbowe mkono.
Kwenye jukwaa la Jamii Forums, Lissu anaongoza kwa asilimia 83.3 ya kura zilizoanza kupigwa wiki iliyopita huku Mbowe akiwa na asilimia 16.7. upigaji wa kura hizo utahitimishwa Jumatatu ijayo.
Hata hivyo, maamuzi rasmi ya nani atakiongoza chama hicho yatafanywa na wajumbe 1,200 wa mkutano mkuu wa CHADEMA.
“Lissu anapendwa na wapiga kura na hili ndilo lengo la chama cha siasa. Mbowe anaweza kupendwa na wajumbe wa Mkutano Mkuu lakini bila wananchi, chama ni mufilisi. Kitabaki tu kuwa chama cha kuitwa Ikulu kunywa chai na kupiga picha,” anaeleza mmoja wa wachangiaji kwenye ukurasa wa kura za maoni kwenye jukwaa la Jamii Forums.
Msimamo wa CHADEMA ni 'no reforms, no election' na ndiyo inayowafanya Mbowe na Lissu kuzibeba agenda tatu za chama hicho.
HERI YA MWAKA MPYA 2025
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED