Kambi Makonda ilivyompigia makofi Rais Samia

By Beatrice Shayo , Nipashe
Published at 07:51 AM Jul 04 2024
Umati uliokusanyika katika ‘Kambi ya Makonda’ iliyotoa tiba za kibingwa bure, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.
PICHA: BEATRECE SHAYO
Umati uliokusanyika katika ‘Kambi ya Makonda’ iliyotoa tiba za kibingwa bure, katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, jijini Arusha.

BAADHI ya wananchi waliojitokeza katika kambi maalum ya matibabu bure mkoani Arusha, wamesimulia awali walivyokata tamaa ya maisha, kwa kukosa fedha za kufanya vipimo katika vituo vya afya.

Juni 24 mwaka huu, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, akatangaza kuanza kambi hiyo ya matibabu ya kibingwa bure katika viwanja vya michezo vya Sheikh Amri Abeid.

Wananchi walijitokeza kwa wingi, hata kusababisha kuwapo foleni kubwa za kwenda kumuona daktari kwa ajili ya kufanyiwa vipimo.

Vurugu zilijitokeza  kutokana na umati wa watu , huku wagonjwa wakieleza walivyokaa miaka mingi nyumbani wanaugua kutokana na kukosa fedha za tiba.

Katika kambi hiyo, wapo wagonjwa waliotoka katika mikoa mingine ikiwamo Mbeya, Manyara, Kilimanjaro, Singida na Dodoma, kwa ajili ya kutaka kutibiwa.

Hapo ndipo ilipogundulika umati, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, akaamua kuziba pengo, akitumia Wizara ya Afya, kuelekeza dawa zenye thamani zaidi ya Sh. milioni 100 katika kambi hiyo ya madaktari bingwa na wabobezi. 

Pia, serikali ikaongeza safu ya madaktari 20 waliotoka Marekani wakijitolea, kuungana na kundi lingine liliongezwa kwa madaktari wa Kitanzania kuanzia Juni 25, katika kazi iliyokuwapo kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid.

"Kipekee ninaomba tumshukuru Rais Samia Suluhu Hassan, hivi tunavyoongea kuna gari linakuja, lina dawa zenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 100. Dawa hizo ambazo Rais Samia amezitoa kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD), ziko njiani…" akatamka Makonda.

Makonda anasema wamepatiwa vijana wa kujitolea wanaotoka Marekani wanaosomea udaktari na uuguzi, wapo zaidi ya 20, hivyo wanaendelea kuongeza nguvu ili kuhakikisha foleni inakuwa fupi. 

ALIYETOKA MBEYA

Joyce Mwaipopo anayeishi mkoani Mbeya, anasimulia imemlazimu kufika  kambi hapo, kutokana na kukosa fedha za kumtibu mwanawe mwenye miaka saba, akisumbuliwa na matatizo ya kuoza viungo vya mwili.

Anasema, mifupa ya mtoto huyo inatoka na kusababisha harufu, hali anayoteseka nayo kwa miaka saba bila ya kupata suluhu.

Mama huyo anasimulia tangu alivyojifungua mtoto huyo, siku ya nne alianza kulia na hakujua kilichomsumbua na alipofika umri miezi saba akaanza kutambaa, akavunjika mkono.

“Madaktari walikuwa wananifokea, niwe makini na mtoto. Inawezekana eti mimi ni mlevi au sitaki kumlea mtoto au ni mzembe,” anatamka mama wa mtoto huyo.

Anaendelea mtoto alivyofika hatua ya kwanza kutembea katika umri wa miezi tisa, akavunjika tena mguu na ndipo safari ya mateso ilivyoanza maishani mwake.

Joyce anasema, akapatiwa rufani kwenda Hospitali ya Rufani Mbeya, akashindwa kupata matibabu, kwa kukosa Sh. Milioni 1.7, hakuwa nazo.

“Ilishindikana, kwa sababu baba yangu aliweka mji wake bondi kwa Sh. 800,000 akapatiwa Sh. 400,000. Bado ule mji ukawa umepotea ikashindikana kupatiwa matibabu nikarudi nyumbani.

“Nilivyoona mwanangu anazidi kuteseka, nikirudi tena katika hiyo hospitali, sipati msaada naambiwa mpaka niwe na hizo (pesa),” anasimulia, huku akilia

“Nikarudi nyumbani, nikaona mguu unazidi kuoza, nikajipa moyo ngoja nirudi tena Hospitali ya Rufani Mbeya, lakini sipatiwi msaada, maana mifupa haipo kwenye nyonga, imetoka akapasuka na goti na kuanza kuoza,” anafafanua.

Anasema, kila alipoenda hospitali hakupatiwa matibabu kwa kukosa fedha za malipo alizotakiwa, akarudi nyumbani viungo vya mwili wa mtoto vikizidi kuvunjika na mifupa kutoka.

Joyce anaeleza, hata alivyokuwa anahitaji msaada wa kusafishwa vidonda vya mtoto wake na hakuweza kupatiwa huduma hiyo, ilimlazimu kumchukua kukatwa nyama zilizooza.

“Bahati mbaya baba yangu ambaye alikuwa akinisaidia, akaugua, ambaye mpaka sasa hivi yupo kitandani. Giza likazidi kuwa nene. Namshukuru Mungu nilisikia hili tangazo la matibabu katika radio, nikaongea na watu wanaonipa msaada wa nguo na fedha, nikawaambia natamani ningefika huko, nasikia kuna mkombozi amejitokeza Makonda.

“Saa nane kuna ‘mkaka’ mmoja alinipigia simu, akaniambia unaweza kwenda na huyo mtoto tukikusaidia? Nikamuambia ‘naweza kwenda’. Akaniambia nijiandae. Nikaenda kwa mama kuomba unga na mchele, ili tuweze kupata chakula tunavyosafiri,” anasimulia 

Joyce anaeleza taarifa zake zinajulikana kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, kuhusiana na tatizo lake na wasaidizi wake walimjulisha aandike barua ili serikali imsaidie tiba, lakini mpaka sasa hajatibiwa.

Anasimulia kwamba vipimo alivyofanyiwa mtoto wake, kipo kilichobaini uti wa mgongo umeathirika, jambo ambalo hakujua.

 “Nyumba zote nilizopanga nafukuzwa, kwa sababu mtoto ananuka na nzi wanamfuata. Sasa nimeona nuru, mwanangu hajawahi kupimwa kwenye hiki kipimo kikubwa ni kwa mara ya kwanza, Mungu ameniona,” anasimulia, huku akitokwa na machozi.

WAKAZI ARUSHA 

Dorah Mollel, ni mkazi wa Arusha anasimulia alikuwa na shida ya macho na nyonga tangu mwaka jana, akiwa ameanza matibabu hakupata nafuu. 

“Nimejikuta sina uwezo wa kuendelea kujitibu tangu Disemba mwaka jana. Ninaugua na huu mguu ulikufa ganzi, natembea kwa kuchechemea.

“Ninashukuru kwa msaada huu kwa kuwa sijawahi kupata msaada wa aina hii ninamshukuru Makonda kutuletea haya matibabu,” anasema.

“Hatukuwa na uwezo wa kumkaribia mkuu wa mkoa na kueleza kero, lakini sasa hivi tumefunguliwa, tunaenda kuongea naye na hata kwa Mkuu wa Wilaya na kueleza shida zako na kusaidiwa,” anaeleza.

“Hawa watu wote tumekuja kufurika hapa uwanjani ni kwamba hatuna fedha kwa ajili ya kujitibu. Unaambiwa unatakiwa kutibiwa kwa Sh milioni 1.5. Kama mimi nisingeweza kipimo cha mwisho, niliambiwa nitoe Sh 100,000 nilikosa nikarudi nyumbani.

“Nilivyosikia hii kambi nikaja mbio, huu umati wanaugua, hawana sehemu ya kwenda kuomba msaada na hospitali zetu zinahitaji fedha,” anasema

Mollel anaeleza kwamba mhusika kafanyiwa kipimo cha macho na kupatiwa miwani, ameenda kupimwa nyonga ana amepatiwa matibabu.

“Tunakutana na madaktari wazuri ambao wanatusikiliza vizuri. Nimefanyiwa kipimo cha X-Ray bila ya malipo na dawa nimepatiwa. Ninamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa jitihada anazozifanya za kutetea wananchi wanyonge,” anasema.

Mwingine ni Mary Lyakurya, anayesimulia changamoto yake ya tumbo tangu mwaka 2021, akiambiwa anatakiwa kufanyiwa kipimo  kwa gharama Sh. 600,000 na hakuwa nazo.

Anasema hakuwa vizuri kifedha, hata ikamlazimu kubaki nyumbani akiugua maumivu, mpaka alipopata taarifa ya kuwapo kambi yenye matibabu bure.

Anaikumbuka siku ya tarehe 25 mwezi uliopita, majira ya saa 11.00 alfajiri akahudhuiria na kupewa namba 39, ila alishindwa kupata matibabu siku hiyo kutokana na foleni, licha ya kuwahi.

“Sikukata tamaa, Jumanne nikafika nikaonana na madaktari husika walinifanyia matibabu na kunipatia rufani niende hospitali ya Mount Meru, wakanifanyia uchunguzi na kunipangia Juni 28 nirudi wanifanyie kipimo,” anasema.

Anasema, vipimo vya awali vilionyesha kuwapo uvimbe kwenye utumbo, akajulishwa anachukuliwa nyama za kupelekwa maabara kuchunguzwa zaidi.

“Nimeambiwa Julai 1 nikachukue majibu. Kwa kweli ninamshukuru Mungu na Rais Samia, kwa sababu wengi ni wagonjwa tunakosa huduma kutokana na gharama za matibabu kuwa kubwa,” anasema  

Mkazi wa Arusha, Raymond Gabriel, anasema, alikuwa kazini wakivunja ukuta, ukamuangukia akawa amekatika mguu wa kulia na mgongo kuvunjika pingili tatu.

Anasema, alikaa Hospitali ya Rufani Mount Meru kwa siku tano akisubiri fedha za kupelekwa katika Hospitali ya Rufani ya Kanda KCMC, huku mguu ukiharibika.

Gabriel anasema, bosi wake alitoa Sh. 500,000 za gari la wagonjwa kumsafirisha na alivyofika hospitalini KCMC mguu wake ulikuwa tayari umeoza, wakaanza kumfanyia oparesheni.

Anasema tiba y uti wa mgongo kufanyiwa upasuaji ilishindikana kwa kukosa fedha Sh. Milioni 10, hata mguu wake alitibiwa baada ya kuuza kiwanja chake, kwani  bosi wake baada ya kumpatia usafiri, hakurejea tena kunihudumia,”anasema.

Gabriel anaeleza kuwa baada ya kufika katika kambi hiyo, daktari alimfanyia vipimo, pia akakutwa na shida nyingine ya kupata choo kikubwa na kidogo, kutokana na tatizo la uti wa mgongo lililompata.

Anasimulia alikofikia ni kwamba, ameshafanyiwa kipimo cha gharama ya Sh. milioni 1.5, iliyokuwa inamsumbua tangu mwaka juzi akikosa fedha nza tiba na dawa.

Ni aina ya mfumo unaoacha salamu za nafasi ya Bima ya Afya kwa Wote.