KARIBU mwaka mpya 2025. Wasomaji na wapenzi wa Kijarida cha Siasa cha Nipashe pokeeni maua yenu na heri nyingi.
Ni mwaka wa jambo letu yaani uchaguzi wa marais wa Tanzania na Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani.
Lakini kwanza itakapofika Juni utakuwa mwanzo mpya kwa Tanzania baada ya kuzindua na kuanza kutekeleza Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050. Inaanza kutumika baada ya ile ya 2025 kumaliza muda wake.
Taifa lenye demokrasia ya kweli ni lazima liwe na dira ambayo ni malengo ya kufikiwa au maono ya mbali ya kutaka lifike huko kwa kipindi fulani.
Dira hiyo huonekana katika mipango, mifumo inayoandaliwa, sheria, taratibu, miongozo na mikakati mbalimbali ya kujenga uchumi na jamii imara inayolingana na wakati unaotazamwa.
Serikali imeandaa malengo au dira na kwa kuona kuwa ni lazima watu wenyewe wapange na kukubaliana na kile wanachotaka na namna ya kufikia lengo ya maono hayo. Dira 2050 imewashirikisha watu katika kuiandaa kadhalika ndiyo muhimili katika kuitekeleza.
Kwa hili la dira serikali imedhihirisha umuhimu wa demokrasia shirikishi kwa kupokea maoni ushauri na fikra kutoka karibu kila kundi ili kuwa na dira inayobeba maoni na mitazamo ya Watanzania wote.
Mwaka 2025 ni wa umuhimu wa kipekee mbali na dira umebeba jambo muhimu, ndiyo msimu wa uchaguzi mkuu wa marais wa Jamhuri ya Muungano na Zanzibar, wabunge, wawakilishi na madiwani. Unafanyika wakati Tanzania ikitimiza miaka 33 ndani ya mageuzi ya kisiasa.
Zama hizi mageuzi hayo ya kisiasa yameboreshwa zaidi na falsafa ya Rais Samia Suluhu Hassan ya R4 zenye maudhui ya “Reconciliation” au maridhiano au kupatana kwa makundi yote yanayohasimiana, “Resilience” yaani ustahimilivu, Reforms” kwa maana ya mageuzi na kuzungumzia mabadiliko ili kuwa na kesho iliyo bora zaidi na “Rebuild” ikimaanisha kujenga taifa upya.
Rais anakuja na falsafa hiyo kwa sababu licha ya kuwa na mfumo wa vyama vingi, kulikuwa na mkwamo wa kisiasa ambao ulivifungia vyama vingine vya kisiasa kushiriki kwenye masuala ya kidemokrasia katika awamu ya tano, suala lililorejesha nyuma na kuzifungia milango ya harakati za kuendeleza demokrasia vyama vya upinzani, taasisi za kiraia na ya kubinya uhuru wa vyombo vya habari.
Mwaka 2025 unapoanza na ajenda ya uchaguzi, la muhimu kuzingatia ni kwamba mfumo wa vyama vingi ni mageuzi ya kisiasa kutoka katika serikali yenye chama kimoja na kuingia kwenye vyama vingi.
Huku ndiko kuwa na wigo mpana wa demokrasia. Mara kadhaa tafsiri ya demokrasia imetolewa na kuna umuhimu wa kuikumbusha tena kuwa ni neno la Kigiriki.
‘Demos’ kwa maana ya watu na ‘Kratos au cratos’ ni uwezo au nguvu ama mamlaka. Hivyo humaanisha uwezo wa raia kujitawala wenyewe kwa manufaa yao.
Utawala wa raia wenyewe huwakilishwa na watu wenyewe lakini kwa njia tofauti kwa mfano kupitia mikutano ya hadhara na mijadala ndiyo maana R4 ya maridhiano na ile ya uhimilivu zinafungua milango ya mikutano ya wanasiasa wapinzani pamoja na harakati zote za kisiasa katika kutoa ya moyoni, kukosoa, kuelekeza ili kuboresha..
Kadhalika, kuna kutoa maoni mfano kwenye mitandao ya kijamii, vyombo mbalimbali vya habari, kwenye mijadala, mihadhara vyote vikitumiwa kutoa maoni ya watu kwa ajili ya faida ya kukomaza demokrasia na kuleta ustawi.
Watu wanaoweza pia kuchagua wawakilishi ndiyo maana ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu wa 2025 na pia wananchi wanakuwa na taasisi zao za kirai , ndizo AZAKI zinazojumuisha wadau, sekta na makundi mbalimbali kuzungumzia maoni na ushauri wao.
Sharti kubwa la demokrasia ni hili, hakuna kujilimbikizia madaraka bali kugawanya madaraka na kuwa na uwakilishi na ushiriki mpana unaogusa karibu kila mtu na kuwapo na taasisi mbalimbali zikifanyakazi tofauti na pia zikitumiwa kufanya ‘checks and balance’.
Katika mgawanyo huo wa madaraka kuna bunge , baraza la wawakilishi ndiyo wawakilishi wa wananchi, watunga sheria, wachambuzi na wapitisha bajeti na wasimamizi wa serikali.
Iko serikali hapa ndipo kuna viongozi kuanzia rais, baraza la mawaziri, makatibu wakuu, watendaji wakuu, maofisa, mameneja na wakuu wa vitengo, vyombo na idara za umma zinazofanyakazi kwa ajili ya wananchi. Hawa wanafanya maamuzi na kusimamia utendaji kazi wa kila siku uwe wa kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Upo muhimili wa sheria ni mahakama, ndani yake kuna majaji, mahakimu, wapo mawakili ambao ni walinzi wa sheria na katiba, waamuzi wa kesi za jinai na madai na kwa ujumla kutafsiri sheria na kusimamia haki.
Pamoja na hayo kuna taasisi nyingine za kuendelea kufuatilia mfano AZAKI, vyombo vya habari navyo ni jicho muhimu kwenye kuendeleza demokrasia.
SIFA ZA DEMOKRASIA
Kikubwa ni uchaguzi huru, halali, wa haki na unaokubalika. Taifa linapoingia 2025 ambo ni mwaka wa uchaguzi wanasiasa wakumbuke kuwa demokrasia ya kweli huonekana wakati wa uchaguzi.
Ni mchakato unaoanza na jinsi wagombea wanavyoteuliwa na vyama vyao, walivyopigiwa kura na kupitishwa, kura zilivyopigwa vituoni, zilivyohesabiwa na kutangazwa matokeo au mshindi.
UTAWALA KISHERIA
Kwenye demokrasia kanuni hii inasimama kwamba, sheria ni kipimo cha mwenendo wa taifa na raia na ili demokrasia iwepo ni lazima sheria zake ziwe za kuendeleza maisha ya watu wote na kuleta usawa katika jamii hasa kwenye kupata na kutumia huduma muhimu na za lazima na pale inapoonekana kuna upungufu ikibidi zibadilike kila wakati kulinda haki , ustawi na maendeleo ya raia.
UHURU KIFIKRA
Serikali yenye demokrasia ya kweli, watu wake wana uhuru wa fikra na kutoa maoni au mawazo bila kuogopa au kutishwa na utawala. Fikra na mawazo yao ni kwa faida yao na taifa pia.
Watu wawe na uhuru wa kuandika habari kuhusu maisha yao, changamoto, fursa bila kuogopa na wakati mwingine ni lazima kukubali upinzani kama Rais Samia anavyosema kuwa ni lazima kuukubali upinzani kwa ajili ya kujenga maana ni muhimu katika nchi.
Wakati huu kuelekea kwenye uchaguzi mkuu lazima serikali ilinde uhuru wa watu wake si kuuingilia. Uchaguzi ili uwe huru ni lazima watu walindwe si kutishiwa maana hatua kama hizo zinaleta woga na kunyong’oneza demokrasia.
HERI YA MWAKA MPYA 2025
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED