MUHAS kufanya kongamano la 12 la kisayansi, kumuenzi Hayati Mwinyi

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 08:23 PM Jun 24 2024
news
Picha: Mtandao
Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Mzee Dk. Ali Hassan Mwinyi.

Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) kitafanya Kongamano lake la 12 la Kisayansi Juni 27 na 28 2024.

Kongamano hilo litafanyika katika Kituo cha Afrika Mashariki cha Umahiri wa Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu, MUHAS Kampasi ya Mloganzila,  nje kidogo ya jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Juni 24, 2024 jijini Dar es Salaam Makamu Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Muhimbili (MUHAS) Profesa Aporinary Kamuhabwa amesema kongamano la mwaka huu ni maalum kumuenzi Mkuu wa Chuo wa kwanza na Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati  Mzee Dk. Ali Hassan Mwinyi.

Profesa Kamuhabwa amesema Jukumu mojawapo la Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili ni kutoa mafunzo ili kujenga rasilimali watu ya fani za afya na kufanya tafiti, kushiriki kikamilifu katika utoaji huduma za afya kwa umma. 

Lengo ni kuhakikisha matokeo ya tafiti zinazofanywa yaweze kutumiwa na watekelezaji, wadau, wafanyakazi wa huduma za afya na wengine wanaofanya kazi katika maeneo husika ya kitaalamu, ambapo matokeo ya tafiti hizi hayana budi kusambazwe kwa ufanisi.

“Madhumuni ya kongamano hili la kumi na mbili ni kushirikishana, kuelezana, kujifunza na kubadilishana ujuzi unaotokana na matokeo ya tafiti kati ya watafiti mbali mbali, watoa huduma wa afya, watekelezaji wa mikakati na sera mbalimbali na wadau wengine wote ndani na nje ya Tanzania ikiwa ni pamoja na kushirikisha jamii kwa ujumla kupitia vyombo mbalimbali vya habari.” amesema Profesa Kamuhabwa. 

Katika Kongamano la 12, Chuo kitaonyesha matokeo ya tafiti za hivi karibuni ya kisayansi kutoka miradi mbali mbali ya tafiti zinazotoka ndani na nje ya nchi katika kipindi cha miaka ya nyuma. Na kwa jamii ya wanataaluma wa MUHAS watapata fursa ya kushirikishana matokeo yao na kubadilishana mawazo na wataalamu pamoja na wadau kutoka sehemu mbalimbali za nchi na duniani kote ikiwa lengo kuu ni kuboresha afya kupitia tafiti.

Ameongeza kuwa Chuo pia kitaeleza mafanikio ya tafiti na athari zake kwa upande wa kijamii na maendeleo ya uchumi wa nchi.

“Kama nilivyosema hapo awali, Kongamano la mwaka huu litatumika pia kumuenzi aliyekuwa Mkuu wa Chuo wa kwanza na Rais wa Pili wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dk. Ali Hassan Mwinyi aliyefariki tarehe 29 Februari, 2024. Katika miaka 17 alipokuwa Mkuu wa Chuo, chuo hiki cha MUHAS kilinufaika moja kwa moja kwa mchango wake katika upanuaji wa miundombinu ya kufundishia, kutoa huduma na tafiti, ikiwemo kampasi hii mpya ya Mloganzila,” amesema Profesa Kamuhabwa 

Ametanabaisha kuwa Kauli mbiu ya Kongamano hili inasema “ SAYANSI KAMA HADITHI YA MAISHA : NGUVU YA TAFITI, BUNIFU NA USHIRIKIANO KWENYE KUIMARISHA MIFUMO THABITI YA AFYA” , Kauli mbiu hii inaendana vema na maneno ya busara aliyotuachia Mzee wetu Mwinyi kwamba Maisha ni Hadithi. Hayati Mzee Mwinyi alitoa mchango mkubwa katika uboreshaji wa sekta ya afya nchini Tanzania.

Kauli mbiu hii pia imechaguliwa mahususi kwa sababu muelekeo wa magonjwa hapa nchini na duniani umekuwa ukibadilika kwa jinsi muda unavyokwenda. Kwa miaka ya nyuma, mapambano makubwa yalikuwa ni dhidi ya magonjwa yanayoambukiza lakini kwa sasa changamoto kubwa ni kwenye magonjwa yasiyoambukiza. Ukiangalia pia magonjwa yanayowakabili watoto ni tofauti na magonjwa yanayowakabili watu wazima.

Ameongeza kuwa hapa nchini kwetu vile vile kunashuhudiwa mabadiliko ya aina ya magonjwa, ongezeko la idadi ya wazee wanaohitaji huduma za afya, ajali, usugu wa vijidudu vya magonjwa dhidi ya madawa, magonjwa ya afya ya akili na magonjwa yanayotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Magonjwa yote haya yanaendelea kutuathiri kwa kiasi kikubwa na wakati huo huo hali za wananchi na mazingira pia yamebadilika. Hivyo basi, ni muhimu kujiuliza nafasi ya sayansi katika kukabiliana na changamoto hizi.

Katika kongamano hilo tafiti za kisayansi 80 zitawasilishwa kwa njia ya maongezi (Oral Presentations) na 107 kwa njia ya mabango (posters). 

Tafiti zitakazowasilishwa zimeainishwa katika mada ndogo ndogo zifuatazo: Magonjwa Yasiyo ya Kuambukiza, Afya ya Akili, Upasuaji na Lishe, Magonjwa ya Kuambukiza na Usugu wa Vimelea dhidi ya Dawa Afya ya Mama, Mtoto mchanga, Mtoto na Vijana rika Utunzaji na afya ya Kinywa, Jicho, Sikio, Pua na Koo. Viamuzi vya kijamii kwa afya (Afya moja) Utafiti wa mifumo ya afya Tiba mbadala na asili, uvumbuzi wa dawa na maendeleo ya chanjo Masuala mtambuka; maadili na taaluma, akili ya bandia, teknolojia na afya ya kazini

Amesema kuwa kongamano hilo linatarajiwa kuvutia wajumbe zaidi ya 400 kutoka nchini na nje ya nchi. Baadhi ya matokeo ya tafiti zitakazowasilishwa katika Kongamano hili ni pamoja na:

Aidha amesema upatikanaji wa huduma za wodi maalum za kulaza watoto wachanga ni 48% Asilimia 15 ya wagonjwa wa VVU wana kiwango cha juu cha sukari (Hyperglycaemia). Unywaji wa pombe na shinikizo la juu la damu linachangia wagonjwa hawa kuwa na kiwango cha juu cha sukari mwilini.

Utafiti uliofanyika Kinondoni, umeonyesha 54.5% ya wanawake wanatumia vipodozi vya kujichubua. Wengi wao ni wale wanafanya mapokezi.

Mijadala mingine itahusisha ufanisi wa kugharimia mifumo ya afya nchini (health system financing) ambapo watafiti watawasilisha jinsi gani nchi yetu itaweza kuutekeleza mfumo huu ili kuleta tija kwa wanachi wote.

Mifumo bora ya kuishi ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza (Healthy living and Healthy aging).

Pia amwashukuru na kuwatambua wadau watakaoshiriki ikiwa ni pamoja na ambao walituma tafiti zao na Kamati ya maandalizi ya Kongamano la kisayansi.

Amewakaribisha wadau wote kuhudhuria, kushiriki na kuchangia matokeo ya tafiti katika Kongamano la kumi na mbili la Kisayansi la Chuo Kikuu Cha Afya na Sayansi Shirikishi, Muhimbili kikamilifu ili kuleta mabadiliko chanya kibingwa na Kibabeli katika sekta ya afya.