YST kutoa tuzo kwa wanafunzi waliofanya vizuri gunduzi za kisayansi Septemba 19

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 04:33 PM Sep 16 2024
Mwenyekiti wa Bodi ya YST,(katikati) Prof.Yunus Mgaya akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) kuelekea siku ya utoaji tuzo kwa wanasayansi chipukizi waliofanya vizuri kwenye gunduzi zao.
Picha: Elizaberth Zaya
Mwenyekiti wa Bodi ya YST,(katikati) Prof.Yunus Mgaya akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) kuelekea siku ya utoaji tuzo kwa wanasayansi chipukizi waliofanya vizuri kwenye gunduzi zao.

TAASISI ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST), inatarajia kutoa tuzo kwa wanafunzi ambao wamechaguliwa baada ya kuwa na gunduzi nzuri za kisayansi zinazolenga kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii.

YST inatarajia kutoa tuzo kwa wanafunzi hao Septemba 19 mwaka huu jijini Dar es Salaam kutoka katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bodi ya YST, Yunus Mgaya, amesema wanafunzi hao wamepatikana baada ya kufanyiwa mchujo ulioshirikisha kazi 1,055 kutoka kwa wanafunzi wa mikoa mbalimbali ya pande zote za muungano.

“Idadi ya wanafunzi waliowasilisha maombi kuonyesha gunduzi zao mwaka huu ilikuwa kubwa, maombi 1,055 yalipokelewa na kati ya hayo, wanafunzi wenye gunduzi 394 walishiriki katika mafunzo ya sayansi na mwisho wa mafunzo, gunduzi 191 zilitengenezwa na kukamilika na 45 zilizoonekana kuwa bora zaidi na zilichaguliwa kushirikii na kuonyeshwa katika maonesho ya kitaifa Septemba 19,” amesema Prof.Mgaya.

Amesema gunduzi za mwaka huu, zimejikita katika masuala mbalimbali ikiwamo uhifadhi salama wa mazao ya kilimo, afya ya binadamu, mifumo ya umwagiliaji, utunzaji wa mazingira, upatikanaji wa nishati ya umeme, usalama wa chakula na utatuzi wa changamoto kidijitali.

Amesema jumla ya wanafunzi 90 na walimu 45 watapata fursa ya kushiriki na kuonesha kazi zao katika maonesho hayo ya kitaifa jijini Dar es Salaam.

Mwakilishi wa mdhamini  mkuu wa maonesho hayo kwa miaka 14 mfulilizo ya YST kutoka Karimjee Foundation, Caren Rowland, amesema wamekuwa wakitoa ufadhili huo ili kuwajengea uwezo na msingi thabiti wa elimu ya sayansi vijana wa Kitanzania  ili kukuza ujuzi wao na kuwasaidia kuchangia katika maendeleo ya taifa lao.

Mwanzilishi mwenza wa YST, Dk. Gozberth Kamugisha akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani.

“Kupitia ushirikiano huu Karimjee Foundation inajivunia kuwa sehemu muhimu ya maendeleo ya sayansi nchini Tanzania. Ni fahari kuona mafanikio makubwa kwenye miradi ya kijamii tunayoisaidia  ikiwamo huu wa YST, ambao umetoa jukwaa kwa wanasayansi chipukizi ambao wengi ni wanafunzi, kuimarisha elimu ya sayansi nchini,”amesema Caren.

Amesema Karimjee Foundation inaamini kuwa uwekezaji katika sayansi ni njia bora ya kukuza ujuzi kwa vijana, kusaidia maendeleo ya jamii na taifa pamoja na kujenga mustakabali bora wa Tanzania.

“Kwa juhudi hizo, Foundation inathibitisha dhamira yake ya kuendelea kulea kizazi kijacho na kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya elimu na uchumi wa Tanzania. Jitihada zinazofanywa na YST katika kuchochea ukuaji wa sayansi, ubunifu na teknolojia kwa vijana wa nchi hii ni mfano wa kuigwa kwa sababu inasaidia kukuza sayansi na kuongeza hamasa kwa wanasayansi kuimarisha zaidi ujuzi na maarifa,”amesema Caren.

Amesema katika kila maonesho, Karimjee Foundation imekuwa ikitoa ufadhili wa masomo kwa washindi kila mwaka na kwamba mpaka sasa imewapatia ufadhili wa masomo wanafunzi 45 ambao wengine ni wa kuendelea na elimu ya juu na mwaka huu itaongeza ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wengine wanne watakaoshinda.