Wizara kuchunguza tuhuma mwanafunzi kushushiwa adhabu ya kipigo na walimu

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 01:29 PM Feb 21 2026
news
Picha Mpigapicha Wetu
Wizara kuchunguza tuhuma mwanafunzi kushushiwa adhabu ya kipigo na walimu.

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imesema imepokea malalamiko mazito kuhusu tuhuma za adhabu iliyopitiliza kwa mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Indian Ocean iliyopo visiwani humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo leo, haikubaliani na tukio hilo iwapo limetokea, likielezwa kuwa ni ukiukwaji wa sheria na kanuni za utoaji wa adhabu kwa wanafunzi shuleni.

Wizara imeeleza kuwa walimu pamoja na uongozi wa shule wana wajibu wa kufuata miongozo na taratibu zilizowekwa kuhusu namna ya kutoa adhabu, na kwamba haitavumilia vitendo vinavyokiuka misingi ya haki na ustawi wa wanafunzi.

“Wizara imeanza kulifuatilia tukio hilo kwa ukaribu na hatua stahiki kwa mujibu wa sheria zitajukuliwa endapo itabainika kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu,” imesema sehemu ya taarifa hiyo.

Aidha, Wizara imetoa wito kwa walimu, wazazi na jamii kwa ujumla kushirikiana katika kulinda haki za wanafunzi na kuhakikisha nidhamu inasimamiwa kwa kuzingatia kanuni zilizopo.

Wizara imewataka wanafunzi kuendelea kuwa na nidhamu, kuwaheshimu walimu wao na kufuata maelekezo pamoja na taratibu za shule ili kujenga mazingira bora ya kujifunzia.