OFISA Elimu wa Wilaya ya Kusini Unguja, Mussa Nahodha Makame, amesema anashangazwa kuona baadhi ya wazazi na walezi mkoani humo kuzipa kipaumbele shughuli za harusi kuliko kufuatilia maendeleo ya elimu ya watoto wao shuleni.
Aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa Kongamano la Usawa wa Kijinsia lililoandaliwa na mradi wa kuwatengenezea mazingira rafiki ya kujisomea kwa wasichana (KFHI) ambalo limewakutanisha wazazi na walezi.
Alisema baadhi ya wazizi hawana ukaribu na watoto wao hasa wa kike katika kufuatilia maendeleo yao ya kielimu na wamejikita zaidi katika sherehe za harusi.
Makame alisema katika kufikia maendeleo ya mtoto kupata elimu lazima wazazi na walezi wawe mhimili muhimu kwa kuwa karibu na watoto wao.
"Watoto kwa kawaida wanatakiwa kuwa na usimamizi mzuri wa wazazi na walezi na walimu pia kinyume na hapo jamii inaenda kupata viongozi wa ovyo hapo baadaye," alisema.
Alisema kuwa wazazi na jamii wanawajibu wa kuwalea watoto wao bila ya kuwabagua kijinsia kwa sababu wote wanahaki sawa katika kupata elimu bila ya ubaguzi wa aina yoyote.
Alisema kuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo imeweka sheria na miongozo juu ya kuwapatia elimu watoto wote bila ya kuwabagua kwa jinsia zao hivyo wazazi wanawajibu wa kufuata miongozo hiyo.
Kadhalika, alizitaka familia kuwashirikisha watoto wa kike katika kutoa ushauri kwenye ngazi za familia ili kuwa na sauti na kusikilizwa katika kujenga familia bora.
Meneja wa mradi huo kutoka Shirika la KFHI linalofadhiliwa na KOICA, Taewan Park alisema kuwa elimu ya jinsia ni msingi wa kuijenga jamii jumuishi kwa wanawake na wanaume bila ya kujali tofauti zao.
Alisema kuwa kufanya hivyo itakuwa ni fursa nzuri ya kuwaondoshea changamoto hizo kwa kusoma kwa mafanikio na kufikia malengo ya ndoto walizojiwekea.
Ofisa Mtendaji wa Elimu Jumuiishi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, Fatma Mbaraka Hashim Hashim alisema kuwa wazazi na walezi wanatakiwa kuwa mstari wa mbele katika kuwahimiza watoto wao wa kike kusoma na siyo kuwa na haraka ya kuwaoezesha.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED