Watishia kurudisha kadi za CCM kisa mgogoro wa mpaka

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:30 PM Apr 02 2024
Kadi za uanachama CCM.
PICHA: MAKTABA
Kadi za uanachama CCM.

MGOGORO wa mpaka kati ya wilaya za Kilindi na Kiteto, umewagawa makada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku baadhi yao wakidaiwa kutishia kurejesha kadi za chama wakipinga alama mpya za mpaka.

Zaidi ya wanachama 6,000 walioko katika eneo la pembezoni unakopita mpaka huo wanapinga uamuzi huo wa serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari mmoja wa wananchi hao, Ramadhan Juma, mkazi wa Kijiji cha Nkama, Kata ya Bokwa, Wilaya ya Kilindi mkoani Tanga, amesema wanachama 6,319 tayari wamejiorodhesha kurejesha kadi hizo kama serikali haitafanya marekebisho.

Amesema kata nyingine inayopinga mpaka huo mpya ni Mvungwe.

Kwa mujibu wa kada huyo, aliyejitambulisha kama mratibu wa zoezi hilo, alisema wanapinga kuanzishwa vijiji vipya vya wafugaji wa jamii ya kimasai vya Lolela na Losoiti vilivyopo wilayani Kiteto.

"Wanachama wanataka kurejesha kadi zao kwa kuwa wanaona kama serikali umekosea kushughulikia mgogoro huo kwa kufuata matakwa ya wakazi wa Wilaya ya Kiteto, ambao wengi wao ni jamii ya wafugaji kwa kuzalisha mpaka huo mpya unaowapa maeneo waliyokuwa wakiyatumia yawe malisho.

Diwani wa Kata ya Bokwa, Idrisa Mgaza, amesema kilichokosekana hapo ni wananchi kukosa elimu waliyopaswa kupewa kabla ya alama hizo kuwekwa. 
 
Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya ya Kilindi, Mohamed Kumbi, amewashauri wanachama hao kutorejesha kadi zao, kwa kuwa kufanya hivyo kutawadhoofisha katika kufuatilia madai yao ngazi za juu.
 
Mkuu wa Wilaya ya Kilindi, Hashim Mgandilwa, alipoulizwa kuhusiana na malalamiko hayo amesema serikali imeshautatua na ulitangazwa kwenye Gazeti la Serikali la Novemba 17 mwaka jana baada ya kusainiwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
 
“Ndiyo kuna mpaka mpya umewekwa. Kwani tatizo ni nini mwandishi? alihoji Mgandilwa alipokuwa akizungumza kupitia simu yake ya mkononi....Unajua GN 853 ndiyo imefuta mipaka yote iliyokuwepo awali."

Mkuu huyo wa Wilaya, alisisitiza hao wanaolalamika ni watu wasiopenda kufuata mabadiliko hayo.