WATU watatu, wamejeruhiwa katika ajali ya barabarani iliyohusisha magari matatu, likiwemo basi la abiria lenye namba za usajili T.804 DCE mali ya Kampuni ya Kapricon lililokuwa likiendeshwa na Mussa Alphan (39), Mkazi wa Arusha, iligonga gari ndogo yenye namba za usajili T.130 AET aina ya Mark II, likiendeshwa na dereva Eliud Godfrey (28) mkazi wa Ilomba.
Kisha gari hilo, kugongana uso kwa uso na gari T355 DLN basi la abiria kampuni ya Premier ikiendeshwa na David Anthony (30) mkazi wa Mwanza na kusababisha majeraha kwa watu na uharibifu wa magari hayo.
Kwa mujibu wa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Wilbert Siwa ni kwamba ajali hiyo imetokea mapema leo Oktoba 07, 2024 majira ya saa 11:15 asubuhi katika eneo la Mbeya Pazuri kata ya Ilomba barabara kuu ya Mbeya- Iringa.
Amewataja majeruhi hao kuwa ni Raymond Mfaume (35) agenti wa basi la Kapricon mkazi wa Uyole jijini Mbeya, Janeth Mwanga (42) mkazi wa Jiji la Dar es Salaam na David Anthony (30) dereva wa basi la Premier mkazi wa Mwanza.
Amesema majeruhi wote walikimbizwa katika Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Mbeya kwa ajili ya matibabu, huku Mfaume akiruhusiwa kurudi nyumbani baada ya afya yake kutengamaa.
“Chanzo cha ajali ni dereva wa gari dogo kuingia barabara kuu, gari lake likiwa linasukumwa bila kuchukua tahadhari, tumemkamata na upelelezi ukikamilisha atafikishwa mahakamani,” amesema Siwa.
Kufuatia ajali hiyo, Kamanda Siwa, ametoa wito kwa madereva kuwa makini kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani ikiwemo michoro na alama zake ili kuepukana na ajali zinazoweka kuepukika.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED