MKUU Wilaya ya Kigoma, Salum Kalli, aliyekuwa Mgeni rasmi katika mahafali ya kufunga mafunzo ya awali ya operation” ya kujitolea ya miaka 60 ya Jeshi la Kujenga Taifa kutoka 821KJ Bulombora kiliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma, amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kuwa makini na matumizi ya simu janja katika mitandao ya kijamii.
Amesema kutokana na ukuaji wa teknolojia ya simu janja zimekuwa chanzo cha kujifunza na kufahamu mambo mbalimbali yanayoendelea katika dunia na kuwataka wahitimu hao wasikubali kuvurugwa nazo bali wazitumie katika kujifunza vitu vya msingi kwaajili ya ulinzi wa taifa.
“Vijana wengi hawana elimu ya matumizi sahihi ya simu ganja na mitandao ya kijamii ,wanatumia simu kutazama vitu visivyofaa na kurusha maudhui yanye madhara katika mitandao, nawaasa msimtumie vibaya, yeyote atakayebainika atachukulia hatua mara moja” Amesema DC Kalli.
Amesema: “Elimu na mafunzo mliyopata myatumie kulinda mipaka ya nchi, msikubali nchi yenu ilindwe na mtu mwingine, msimamie kiapo, nidhamu iwe kitu pekee katika kila kitu mnachokifanya, msimamie miongozo ya nchi ili kutimiza lengo la taifa la kuwafanya kuwa jeshi la akiba.”
Akiongea mwakilishi wa mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa nchini (JKT) Hassan Mabena ambaye pia ni mkuu a tawi la Utawala wa jeshi hilo amesema vijana waliohihitimu mafunzo ya awali wanapaswa kujikita katika misingi ya “operation” ya kujitolea ya miaka 60 ya kujenga taifa ili kutekeleza malengo ya mwasisi wa taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Mabena amewataka vijana hao kuwaelimisha wengine juu ya umuhimu wa kujiunga na JKT kutokana na mafunzo ya uzalendo na stadi mbalimbali za maisha wanazozipata zinazowaepusha vijana wengi kuingia katika makundi yanayoharibu mustakabali wa maisha yao.
Mafunzo hayo ya awali yamedumu kwa miezi minne toka mwezi Disemba 2023 hadi Aprili 2024 ambapo hatua inayofuata ni mafunzo ya miezi 20 ya stadi za kazi na stadi za maisha katika makambi tofauti kote nchini.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED