BAADHI ya abiria walionusurika katika ajali ya boti ya mizigo MV. Sea Falcon iliyolazimisha kubeba zaidi ya abiria 30 kutoka Kirumba, mkoani Mwanza kwenda kisiwani Goziba, mkoani Kagera, wamesema boti ilianza kuzama saa 12 jioni, wakapata msaada saa nne usiku.
Ajali ya boti hiyo iliyosajili MTZ 012212 ilitokea juzi katika Ziwa Victoria, Km mbili kutoka Mwalo wa Bwiru, wilayani Ilemela, mkoani Mwanza.
Wakisimulia kwa nyakati tofauti jana wakati wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mwanza (Sekou Toure), manusura hao walisema walikunywa mafuta ya petroli yaliyokuwa yakimwagika kutoka mapipa waliyoshikilia kujiokoa.
Mfanyabiashara na Mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam, Noris Mwene, alisema kuwa baada ya kuanza safari umbali wa zaidi ya Km moja, boti hiyo ilianza kuingiza maji ndani na kuanza kuzama majira ya saa 12 jioni.
"Baada ya kuanza kujaa maji, nahodha pamoja na msaidizi wake walituambia wanahitaji kurejesha boti hiyo nchikavu kwani kuna kitu ambacho walikisahau lakini baadaye wakashauriana waendelee na safari licha ya kuonekana boti inaendelea kujaa maji,"alisema.
Aliendelea kusimulia kuwa baada ya muda mfupi, boti hiyo ilianza kuzama; wakamwaga mafuta yaliyokuwa kwenye mapipa ili kuwasaidia kuelea kutokana na kukosa msaada.
"Hali hiyo iliendelea hivyo mpaka majira ya saa nne usiku, walifika baadhi ya wavuvi na kutusaidia.
"Awali walikuja baadhi ya wavuvi wakakuta tunaendelea kuelea, tulipowaomba msaada walichukua tu mizigo yetu, yakiwamo mapipa ya mafuta pamoja na fedha tulizokuwa nazo kisha kuondoka bila kutupatia msaada wa aina yoyote huku mapipa yale ya mafuta yakiendelea kutupiga usoni na kunywa petroli iliyokuwa ndani ya mapipa hayo," alisema.
Alisema kuwa yey alikuwa wa kwanza kupata msaada majira ya saa tatu na nusu usiku, akisaidiwa na vijana waliokuwa na mitumbwi midogo.
"Nilipofika nchikavu nilianza kuwatafutia msaada na kumpata mwenyekiti wa eneo hilo aliyenisaidia kupata mawasiliano ya Jeshi la Polisi pamoja na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji waliofika majira ya saa nne na kuanza kushirikiana na wavuvi wengine walikuwa wakiendelea kuokoa watu," alisimulia.
Lucia Kubagwa, mfanyabiashara na Mkazi wa Nyarugusu, mkoani Geita alisema walifika bandarini Kirumba na kukuta tayari boti ya abiria imeondoka, hivyo wakaambiwa kuwa hata hiyo ilikuwa inaelekea huko na kuwa inabeba abiria. Waliaminishwa kuwa zaidi ya abiria 40 wanaweza kuingia katika boti hiyo.
"Tulipiga kelele sana bila msaada, tukaanza kumwaga mafuta ya petroli na kuelea katika mapipa hayo huku tukinywa mafuta yaliyokuwamo ambayo mpaka sasa ninajihisi tumbo na kifua vinauma kutokana na mafuta hayo niliyokunywa," alisema Lucia.
Akizungumza katika eneo la tukio, shuhuda wa tukio hilo ambaye pia ni mmiliki wa eneo la mwalo walikokuwa wakipokewa majeruhi hao, Joseph Masole, alisema ajali hiyo ilitokea Km mbili kutoka nchikavu ambako baada ya mmoja wa abiria kufika nchikavu walianza kushirikiana naye kupeleka mitumbwi ili kutoa msaada wa uokoaji.
"Alifika anasema tupo watu kama 60 tunahitaji msaada, nikatuma mitumbwi ikaenda kuokoa watu na wakati huo tukiendelea na kuomba msaada kutoka vyombo vya ulinzi na usalama. Magari ya wagonjwa yaliletwa kwa ajili ya kuwapokea wote waliokuwa wakiokolewa," alisema Masole.
Akizungumza hospitalini huko, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Mwanza (Sekou Toure), Bahati Msaki alisema usiku wa kuamkia jana alipokea mwili wa mtoto wa kiume Kharidi Rajabu (6) na Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Goziba, wilayani Muleba.
Pia alisema walipokea majeruhi 28. Kati yao, 22 wanaume na wanane wanawake ambako hadi kufikia jana majeruhi 14 walikuwa wameruhusiwa huku wengine 14 wakiendelea kupatiwa matibabu.
Jeshi la Polisi mkoani Mwanza kupitia Kamanda wa Polisi Mkoa huo, DCP Wilbrod Mutafungwa, lilithibitisha kuwakamata watu watatu, akiwamo mmiliki wa boti hiyo, Amon Lutabanzibwa kutokana na kulazimisha kutumia boti hiyo kubeba abiria bila kuwa na kibali cha kufanya kazi hiyo kutoka Shirika la Uwakala wa Meli nchini (TASAC).
Kamanda Mutafungwa alitaja wengine waliokamatwa kutokana na ajali hiyo kuwa ni pamoja na Robert Kabota (31), nahodha wa boti hiyo na Salum Shaban (59), msimamizi wa boti hiyo ambao wote wanaendelea kuhojiwa kuhusu ukiukwaji sheria za usafirishaji majini.
"Walionusurika ni watu 30 kati ya 32 kwa idadi tuliyonayo ambako pamoja na mtoto huyo aliyefariki dunia na mtu mwingine ambaye hajajulikana jina na alikuwapo katika ajali hiyo, bado tunamtafuta," alisema DCP Mutafungwa.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda alisema serikali itagharamia matibabu ya majeruhi wote na kuwataka ndugu wa baadhi ya watu ambao hawajapatikana kuendelea kuwa wavumilivu wakati vyombo vya usalama vikiendelea kufuatilia.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED