WAZIRI Mkuu na Makamu wa Kwanza Rais Mstaafu, Jaji Joseph Warioba, amesimulia alivyotaka kujiuzulu nafasi ya Waziri wa Sheria, wakati hayati Edward Sokoine alipokuwa Waziri Mkuu, kutokana na kutoridhika na uamuzi wa kutaka kubadili sheria.
Wakati huo, Warioba alikuwa pia Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakati wa uongozi wa Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere kabla ya kuwa Waziri Mkuu na makamu wa kwanza wa Rais mwaka 1985 hadi 1990 wakati wa serikali ya awamu ya pili iliyoongozwa na Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
Jaji Warioba alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kitabu cha ‘Edward Moringe Sokoine: Maisha na Uongozi Wake’, uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan, jijini Dar es Salaam.
Warioba katika simulizi hiyo, alitumia dakika 19 kueleza nyakati ngumu na nzuri walizofanya kazi pamoja na Sokoine, huku akimwelezea alikuwa mtu wa aina gani na umuhimu wa kitabu cha maisha ya kiongozi huyo kwa viongozi wa Kitanzania, hususani vijana.
Alisema Sokoine alichukia sana wala rushwa na wahujumu uchumi, hivyo alipoteuliwa kuwa Waziri Mkuu kwa mara ya pili (1983 hadi 1984 alipofariki dunia), alipendekeza mabadiliko ya sheria ili kupambana na watu waliojihusisha na mambo hayo.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, katika mabadiliko hayo, Sokoine alipendekeza kesi za uhujumu uchumi ziwe na mahakama zake maalum, zisikilizwe faragha, hata maneno ya kusikia kuhusu wahujumu uchumi yakubalike.
Alisema binafsi hakukubaliana na hayo kwa sababu mbalimbali ambazo alisema alizitoa kwenye Baraza la Mawaziri na mbele ya Rais Nyerere.
Jaji Warioba ambaye amewahi kuwa Jaji wa Mahakama ya Haki ya Afrika Mashariki, alisema pamoja na kutoa sababu za kupinga vipengele hivyo, hakukubaliwa kwa sababu aliyepinga alikuwa peke yake, hivyo alikubaliana na matokeo. Hata hivyo, alisema alitangaza kujiuzulu kwa sababu hakuwa tayari kusimamia vipengele hivyo akiwa waziri wenye dhamana.
“Sokoine hakupenda hilo, akaniita, akasema wewe umekuwa mstari wa mbele kupambana na rushwa. Sasa kwa kitu kidogo kama hiki unasema unaacha kazi? Nikamwabia hapana Waziri Mkuu, hili ni la muhimu zaidi,” alisimulia.
Jaji Warioba ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ya Tanzania mwaka 2012, alisema alimweleza sababu ya kujiuzulu kuwa aliamini kama utekelezaji wa sheria hiyo ungeanza ungesababisha madhara makubwa kwa kuwa inavunja misingi ya utawala bora na kuingilia haki za binadamu.
Baada ya kumpa sababu hizo, alisema Sokoine alimpeleka kwa Nyerere ambaye aliwashauri wakaondoe vipengele vya kesi kusikilizwa faragha, lakini vipengele vya utaratibu maalum na kutoruhusiwa dhamana vibaki.
Alisema baada ya kupata maelekezo kutoka kwa Nyerere, Sokoine alimwelekeza kufanya marekebisho na kesho yake ampelekee kwa ajili ya kuendelea na utaratibu, na kwamba alitekeleza na sheria ilipita Aprili, 1983.
Baada ya sheria hiyo kuanzia kutumika, alisema mambo yale yale aliyohofia kuwa yangetokea, yaliyotokea kwa sababu watu walikamatwa kwa utaratibu usio nzuri, mali kukamatwa na malalamiko ya wananchi kuwa mengi.
Alisema malalamiko yalizidi na ilitokea baada ya Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kanda ya Ziwa kukamatwa kwa tuhuma za uhujumu uchumi, ndipo wazee walikwenda kumwona Nyerere ambaye aliandika ujumbe maalum kutoa maelekezo kwa Sokoine kutoa dhamana.
Alisema Sokoine akamwandikia yeye (Warioba) barua ya kumwomba amwachie na yeye akakataa kwa kuwa sheria hairuhusu.
“Alipiga simu yeye mwenyewe (Sokoine) kuniita ofisini kwake. Nilipofika kabla sijaingia, akasema Joseph wewe ni mtu wa aina gani? Rais anatoa amri, wewe unasema hutekelezi? Basi na mimi kwa kuwa tulikuwa tunataniana nikacheka tu.
“Nikasema si uliniburuza ukanipeleka Msasani (Kwa Nyerere) na ulisikia mkuu alisema nini? Kwamba dhamana isitolewe? Na Rais alisema msivunje sheria hata ikiwa mbaya bali muibadili,” alisimulia Warioba.
Alisema baada ya mazungumzo hayo, Sokoine alimwelewa lakini alisema hawawezi kwenda kumwambia mkuu wa nchi kuwa haiwezekani bali waichukue kama maagizo ya kubadili sheria, hivyo alimwagiza kufanya mabadiliko ya sheria na alifanya hivyo na kuipeleka bungeni Juni, 1983 hivyo ilidumu kwa miezi miwili tu.
Pamoja na yote, alisema Sokoine alikuwa kiongozi mwadilifu na mchapakazi, aliyependa kuuliza maswali mengi kuhusu utendaji kazi wa watumishi pia alitoa nafasi ya kuulizwa maswali.
“Akiwa amezungukwa na Baraza la Mawaziri Vijana, Sokoine alikubali kukosolewa na ikitokea amepishana lugha na kiongozi mwenziwe, hakuwa mtu wa kuweka kinyongo. Alihakikisha wanamaliza tofauti na waliendelea na kazi kama kawaida,” alisema.
Pia alisema kiongozi huyo alikuwa anathamini mambo ya kimila hasa uongozi, akitolea mfano kipindi CCM inaanza kutengeneza kanuni za mgombea urais, alipinga mpango wa kuchaguliwa kwa kura za karatasi na kushauri wachaguliwe kwa kuangaliwa viongozi wanaowajua kwa utendaji kazi wao.
Alisema kiongozi huyo alikuwa akijifunza kwa watu wa kawaida na aliishi maisha ya kawaida ndani ya nyumba za kimasai (maboma) hata kila anapokuwa nyumbani kwake, wanakijiji walikuwa wakikusanyika na kumweleza shida zao.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED