JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata watuhumiwa watatu akiwemo Miraji Issa (29) Mkazi wa Tandale kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya raia wa China aliyefahamika kama Liu Qianhu Jiangxi (48), mfanyakazi wa kampuni ya Hope Recycling.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, marehemu aliuawa katika tukio la kihalifu lililofanyika Septemba 28, mwaka huu, baada ya watuhumiwa kuruka ukuta na kuingia kwenye yadi ya kampuni iliyoko katika Bonde la Msimbazi Ilala ambako marehemu alikuwepo ndani yake.
Amesema baada ya mauaji hayo kutekelezwa watuhumiwa waliiba baadhi ya vitu vya kampuni ya PTC investiment na kutokomea, akieleza kuwa Jeshi la Polisi lilifanya upelelezi wa kina na kufanikisha kuwakamatwa watuhumiwa hao wote watatu.
“Baada ya watuhumiwa kuhojiwa kwa kina vitu vile vilivyoibiwa vimepatikana, na mashauri yao yatafikishwa kwenye ofisi ya mashtaka na baada ya uchambuzi wa kisheria watafikishwa mahakamani kwa kadri ofisi ya mashtaka itakavyoona inafaa,” amesema Muliro.
Ameongeza kwa kutoa wito kwa wananchi kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa mbalimbali zenye viashiria na matishio ya kihalifu, na kwamba hata ikitokea bahati mbaya kuna tukio limetokea watoe ushirikiano wa taarifa ili wahusika wakamatwe na kufikishwa kwenye vyombo vya kisheria.
Aidha, amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam halitakuwa na huruma kwa watuhumiwa wowote wa makosa ambayo yatakuwa yanapagwa au yanataka kutendeka, na kwamba kwa kushirikiana na wananchi watahakikisha watuhumiwa hawapati fursa na wanashughulikiwa vikali, haraka na kwa mujibu wa sheria.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED