Wananchi wajawa hofu ya kijiji chao kufutwa

By Kulwa Mzee , Nipashe
Published at 11:39 AM Sep 16 2024
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Ndejembi.
Picha: Mtandao
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Deogratius Ndejembi.

WANANCHI wa Kijiji cha Ngombo, Kata ya Biro, wilayani Malinyi, mkoani Morogoro wameomba serikali kuwasaidia wasihamishwe katika kijiji chao walichoishi babu zao kwa zaidi ya karne tatu baada ya kuambiwa ni wavamizi wa eneo hilo.

Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, baadhi ya wawakilishi wa kijiji hicho walidai wako katika eneo hilo kwa muda mrefu - kizazi na kizazi na wanashangaa kuambiwa wahame na mamlaka za hifadhi kutokana na uharibifu wa vyanzo vya maji.

"Kumekuwa na tetesi kuwa mamlaka zinazosimamia maeneo ya hifadhi zinawataka wanakijiji kuondoka kijijini haraka iwezekanavyo na hii inatutia wasiwasi kwa sababu kama kweli hilo lipo, basi lingekuja kwa kufuata taratibu za kisheria," alisema mmoja wa wanakijiji hao, Ananias Patitu.

Alieleza hofu yao ilivyo kubwa na kuomba serikali iwasaidie wasiondolewe katika maeneo yao kwa kuwa hawajui wapi wataishi ikiwa wataondolewa.

"Tunaiomba serikali ituonee huruma na kutuacha tuishi hapa kwa kuwa tupo tangu miaka mingi na tumerithi kijiji hiki kutoka kwa babu zetu ambao nao walirithi kwa babu zao," alisema Mzee Patitu.

Alisema kumekuwa na madai ya kuharibu chanzo cha maji cha Bwawa la Kufua Umeme la Mwalimu Nyerere kupitia shughuli mbalimbali kikiwamo kilimo na ufugaji, huku wakieleza kuwa wananchi wanaelewa umuhimu wa vyanzo hivyo na hakuna uharibifu wowote uliofanyika.

Mwakilishi mwingine wa kijiji hicho, David Mkumba alisema kuwa kwa muda wote ambao wameishi kijijini huko wamewekeza vya kutosha na kijiji chao kimekuwa miongoni mwa vijiji vinavyochangia mapato kwa serikali.

"Hiki kijiji chetu kimesajiliwa na tumefanikiwa kujenga huduma zote muhimu za kijamii kama vile shule na kituo cha huduma ya afya," alisema Mzee Mkumba.