WANANCHI wa Kigoma Mjini wameeleza matarajio yao ya kupata majibu ya changamoto zinazowakabili pamoja na kusikia maelekezo ya uongozi wa chama kufuatia ziara ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kenan Kihongosi, aliyewasili wilayani humo leo.
Akizungumza wakati wa mapokezi hayo, Mbunge wa Kigoma Mjini, Revocatus Chipando (Baba Levo), amesema ziara hiyo ni muhimu kwa wananchi wa Kigoma Mjini kwakuwa inaleta nafasi ya kukutana na kusikiliza maelekezo ya viongozi wa chama pamoja na kueleza changamoto zinazowakabili katika mji huo.
Mbunge huyo amemweleza kiongozi huyo kuwa wananchi wa Kigoma wana imani na uongozi wa chama na wanaamini baadhi ya matatizo yanayowakabili katika mji huo yana majibu sahihi kupitia viongozi wa chama.
“Nipo ndugu yako, jembe lako, nipo tayari kusimama na wewe popote kuhakikisha mji huu unakupa ile heshima ya kifalme wewe ni mfalme katika mji huu wa Kigoma Mjini na umati mkubwa umejaa hapa, ukiangalia wengi ni vijana,” amesema.
Ameongeza kuwa vijana ni nguvu kazi ya taifa na wamekuwa wakipewa kipaumbele na Rais Samia Suluhu Hassan kupitia mipango mbalimbali ya kuwainua kiuchumi.
“Dk Samia Suluhu Hassan ameweka hela nyingi sana kwa vijana lengo ni kuhakikisha vijana wanatoka kwenye fikra potovu na kuingia kwenye fikra za kuijenga nchi yao kazi yake ni kuhakikisha vijana wanapata pesa ili waachane na fikra za ovyo na kufanya kazi kwa ajili ya nchi yao ya Tanzania,” amesema.
Aidha, Kihongosi amewahimiza wananchi kujitokeza katika uwanja wa kawawa ili kero zao zisikilizwe nakupatiwa majibu.
“Ukiwa na kero yoyote njoo pale Kawawa hata kama mke wako anakupiga njoo ukawa uniambie. Wajibu wa CCM ni kutatua migogoro yote, iwe ni ardhi, kero ya maji, kero ya umeme au jambo lolote,” amesema.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED