ZAIDI ya wanafunzi 8,000 wa shule za Msingi katika Wilaya za Rufiji na Kibiti mkoani Pwani wamekosa masomo kutokana mafuriko yaliyotokana na mvua kubwa zinazoendelea kunyesha.
Ofisa Elimu Mkoa wa Pwani, Sara Mlaki, ameyasema hayo kwenye ziara ya kujionea athari za mvua hizo katika shule na makazi katika wilaya za Rufiji na Kibiti ikiwamo kuharibu miuondombinu ya elimu.
Amesema shule 11 za msingi zenye wanafunzi 7,264 wakiwemo wasichana 3,657 na wavulana 3,607 wameathirika na mafuriko wilayani Rufiji.
Aidha nyumba 58 za walimu pia zimeathiriwa na kupoteza samani na mali zilizokuwemo ndani ya nyumba hizo.
Amesema katika wilaya ya Kibiti wanafunzi 824 katika shule saba za msingi zimeathirika huku tatu zikifungwa kutokana na adha hiyo huku sekondari ya Mtanga Delta ikiathirika pia.
“Athari za mvua ni kubwa zimeaharibu miundombinu ya shule na wanafunzi kukosa sehemu za kusoma, mkoa umefanya jitihada kuhakikisha wanakuwa salama na kuanisha shule ambazo haziathirika na mafuriko ili zipokee wanafunzi kuendelea na masomo,”amesema Sara.
Akizungumzia maafa hayo, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolph Mkenda, alisema tayari serikali imeweka utaratibu kwa wanafunzi wote waliokumbwa na mafuriko hayo kusoma kwenye shule maalum ambazo zimetengwa.
Mkenda amesema mwanafunzi yeyote asibaki nyumbani kwa sababu ya mafuriko na badala yake wazazi wawapeleke kwenye shule ambazo zimeanishwa na viongozi wa maeneo hayo.
Kuhusu miundombinu alisema tayari serikali imetenga fedha kwa ajili ya kujenga mabweni, vyoo, madarasa, vifaa vya kufundishia na chakula kuwawezesha wanafunzi kusoma kwa utulivu.
Amesema tayari wizara imetoa baadhi ya vifaa vikiwamo vitabu vya kiada na ziada, madaftari na penseli na kalamu kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Muhoro na Katundu ambazo ni miongoni mwa shule zinazopokea wanafunzi walioathirika na mafuriko.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof.Carolyne Nombo, alisema wanaendelea kufanya tathmini za athari za mafuriko katika sekta ya elimu lakini amepongeza jitihada za walimu kuendelea kuwepo kwenye vituo vya kazi na kufundisha licha ya mafuriko.
Akifafanua kwa wanafunzi wa madarasa yenye mitihani alisema serikali imeweka utaratibu wa kuhakikisha wote wanatambulika na kurudi shule.
Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amesema timu ya wataalam imeweka kambi kuhakikisha wananchi wote waliokumbwa na mafuriko wanahamishiwa kwenye makambi maalum ikiwemo ya Nyamwage ambayo imewekwa kwa ajili ya kutoa huduma zote muhimu.
Mwalimu mkuu wa Shule ya Sekondari, Gladness Swai alisema shule yake imejipanga kupokea wanafunzi kutoka maeneo mbalimbali lakini tatizo ni uhaba wa miundombinu ya madarasa, vyoo na mabweni kwa ajili ya wanafunzi.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED