Wanafunzi wafukuzwa kisa wazazi wapinzani

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:46 AM Dec 06 2024
Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda.

WANAFUNZI tisa katika Shule ya Msingi Izinga iliyoko Namanyere, Nkasi mkoani Rukwa, wamefukuzwa shule na wazazi kutakiwa kuwatafutia shule zingine za kuendelea na masomo yao.

Kwa mujibu wa barua zilizotolewa na mwalimu mkuu wa shule hiyo, hatua hiyo imechukuliwa kwa madai ya wazazi wao kutoa kashfa dhidi ya walimu na pia ni wafuasi wa upinzani.

Wakati wanafunzi hao wamefukuzwa, Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi imetangaza kuwarudisha huku ikitangaza kuchukua hatua za kiutawala dhidi ya mwalimu mkuu huyo baada ya uchunguzi kukamilika. 

Katika mitandao ya kijamii jana, kulisambaa barua zinazodaiwa kuandikwa na mwalimu mkuu wa shule hiyo kwenda kwa wazazi pamoja na majina ya wanafunzi hao kutoka madarasa tofauti akiwamo wa darasa la kwanza.

Sehemu ya barua hizo zenye tarehe ya juzi, inaeleza sababu kuwa ni kutokana na kashfa na kauli mbaya ambazo mzazi husika alizitoa Novemba 27, mwaka huu, wakati wa mchakato wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Barua hiyo inaeleza kwamba kutokana na vitisho na dharau dhidi ya walimu, wameona hawana uwezo wa kufundisha watoto wao na kuwataka wakatafute shule nyingine.

MSIMAMO WA SERIKALI

Akitoa ufafanuzi kuhusu sakata hilo jana, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisema kutokana na uamuzi huo aliouita wa ajabu na ulioibua hisia tofauti, serikali itachukua hatua stahiki baada ya kukamilika uchunguzi na kupokea ripoti ya timu ya wadhibiti ubora wa elimu.

Alisema kama jambo hilo litabainika kuwa la kweli, litakuwa la ajabu na la kusikitisha kwa kuwa hakuna mwongozo wala sheria kwamba mwanafunzi atengwe kwa sababu ya mlengo wa kisiasa wa baba yake.

“Ni kweli mimi nimeona hizo taarifa zinasambaa kwamba kuna watoto wamefukuzwa shule kwa sababu wazazi wao ni wanachama wa CHADEMA (Chama cha Demokrasia na Maendeleo). 

“Tunafuatilia tujue ukweli wa taarifa hizi; tayari timu ya wadhibiti ubora inaelekea kwenye shule hiyo. Kwa hiyo tutapata ukweli wa jambo hili baadaye.

“Lakini pamoja na kila kitu, ninapenda kusisitiza kwamba, shule zinaongozwa kulingana na miongozo, kulingana na sheria na taratibu ambazo zinawekwa na haiwezekani mwalimu mmoja ajitungie sheria zake mwenyewe. Vyama vya siasa vipo kwa mujibu wa sheria. Hakuna mwongozo wala sheria kwamba, mwanafunzi atengwe kwa sababu ya mlengo wa kisiasa wa baba yake,” alisema.

Waziri Prof. Mkenda alisema Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza hata mabinti waliopata mimba, ujauzito warudishwe shuleni. 

“Sembuse watoto wa wazazi ambao kwa hiari yao wamechagua chama chochote cha kisiasa kuwa wanachama na vyama hivi vimesajiliwa kisheria?” alihoji.

Prof. Mkenda alisema hakuna ubaguzi kwa mtoto yeyote Mtanzania, hivyo kila mmoja anatakiwa kusoma shule kwa kuwa serikali inajenga shule nyingi na maelekezo ya Rais Samia ni kwamba, kuhakikisha kila mtoto anasoma.

HATUA ZILIZOCHUKULIWA

Kwa mujibu wa barua iliyotolewa baadaye jana na Mkurugenzi Mtendaji wa Nkasi, Afraha Hassan, hatua ambazo wamechukua ni pamoja na kuwarejesha shuleni wanafunzi wote tisa waliosimamishwa.

“Wanafunzi wote tisa waliosimamishwa shule wamerejeshwa shuleni bila masharti yoyote. Hatua za kiutawala na uongozi dhidi ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Izinga zitachukuliwa pindi uchunguzi unaoendelea utakapokamilika,” alisema Hassan.

Kadhalika alisema serikali itahakikisha wanafunzi wa shule hiyo na nyingine katika Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi wanasoma bila kubughudhiwa wala kuingizwa katika migogoro yoyote ya kijamii na kisiasa.

Alisema baada ya kufanya mahojiano na wadau wakiwamo Ofisa Elimu Kata, Mtendaji Kata na Mwalimu Mkuu imebainika mwalimu mkuu aliwasimamisha wanafunzi hao tisa na kutaka wazazi wao wakatafute shule nyingine.

Alisema Wizara ya Elimu kupitia Mkuu wa Wilaya ya Nkasi haikuhusika kutoa maelekezo ya kusimamishwa shule wanafunzi hao.

“Uamuzi wa kuwasimamisha wanafunzi hao haukutokana na itikadi za kisiasa za wazazi wa wanafunzi hao, bali ni mtafaruku uliojitokeza kati ya Mwalimu Mkuu, walimu na wazazi kutokana na kashfa, dharau na lugha chafu zilizotolewa na wazazi dhidi ya walimu wa shule hiyo kwamba, hawana sifa ya kufundisha watoto wao,” alisema.

Hassan alisema uamuzi wa kuwasimamisha wanafunzi hao haukufuata utaratibu wa miongozo ya wizara, kwa sababu waliosimamishwa hawakuwa na kosa lolote la kinidhamu.

BARUA

Katika barua hizo zilizozagaa katika mitandao ya kijamii, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Izinga, Namanyere huko Nkasi, sehemu ya barua hizo inasomeka: “Rejea mada tajwa hapo juu. Walimu wote wa Shule ya Msingi Izinga, tumefikia maamuzi (uamuzi) ya (wa) kusimamisha shule watoto wako tajwa hapo juu (majina yamehifadhiwa) kutokana na kashfa na kauli mbaya ulizozitoa wewe mzazi siku ya tarehe 27/11/2024 wakati wa zoezi la Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

“Kutokana na vitisho ulivyovitoa kwa walimu na dharau nyingi dhidi yetu, tumeona hatuna uwezo wa kuwafundisha watoto wako tena. Hivyo wewe kama mzazi wa watoto tajwa hapo juu, watafutie watoto wako shule yenye walimu unaowaamini kuwa ndio yenye uwezo wa kuwafundisha watoto wako.”