"Wana-CUF njooni ACT Wazalendo, CUF inasubiri kuzikwa" -Ado

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:31 PM Sep 16 2024
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu akizungumza na wa wazee wa Kibiti.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu akizungumza na wa wazee wa Kibiti.

Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amewataka wanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) kuhamia ACT kwa madai kuwa chama hicho kimepoteza dira na kinasubiri 'kuzikwa' rasmi.

Kauli hiyo aliitoa jana Septemba 15,2024  katika Kata ya Ruaruke, Jimbo la Kibiti kwenye mkutano wa hadhara katika ziara ya viongozi wa chama hicho katika mikoa 22 majimbo 125 ya Tanzania Bara.  

Alisema: "Ndugu zangu Wana-Kibiti, ninafahamu kuwa wanamageuzi wengi wa Kusini na Pwani mlikiamini na kukipenda Chama cha CUF. Mliamini kuwa ajenda ya ukombozi, hasa wa kiuchumi kwa maeneo ya Kusini na Pwani itabebwa na CUF"-Ado

"Hali ya sasa, nyinyi nyote ni mashahidi, CUF imepoteza dira na inasubiri kuzikwa rasmi. Kwa yeyote ambaye aliiamini ile 'haki sawa kwa wote' na 'ngangari' bila shaka anajionea kwa macho kuwa CUF haina uwezo huo tena" Ado

"Baada ya marehemu Maalim Seif Sharif Hamad kujiunga na ACT Wazalendo, Wana-CUF wemgi 'walishusha tanga' kumfuata. Hatua hii, si tu kwamba ilikipa nguvu chama chetu, lakini pia ilibadili kabisa ramani ya kisiasa nchini. Upesi upesi, ACT Wazalendo kimekua kwa kasi sana" Ado

"Tunajua kuna Wana-CUF wengi ambao mmekata tamaa na mageuzi baada ya kilichotekea mwaka 2019. Tunajua baadhi mmepunguza harakati na kujikita kwenye shughuli binafsi. Tunajua pia mpo ambao mna matumaini pengine CUF itafufuka. Binafsi sioni hilo likitokea" Ado

"Rai yangu kwenu wapiganaji mliobaki CUF hapa Kibiti na Tanzania kwa ujumla, karibuni sana ACT Wazalendo tuendeleze mapambano. ACT Wazalendo ndio jahazi sahihi kwenu" Ado

"Tutawapokea wote kwa mikono miwili na kwa pamoja tutaendeleza sera zilezile za haki sawa kwa wote ili kujenga 'Taifa la Wote kwa Maslahi ya Wote' na 'Zanzibar Mpya, Zanzibar Moja Mamlaka Kamili"- Ado

1