Waliombaka ‘binti wa Dovya’ jela maisha, faini milioni 1/-

By Paul Mabeja ,, Renatha Msungu , Nipashe
Published at 11:04 AM Oct 01 2024
Watuhumiwa wa kesi ya ubakaji  na ulawiti kwa kundi  wakitoka katika Mahakama Jumuishi ya Utoaji Haki  Dodoma jana, baada ya kuhukumiwa  kifungo cha maisha jela na kulipa faini ya Sh. milioni moja kwa kila mmoja. Hukumu hiyo ilitolewa jana na Mahakama
PICHA: IBRAHIM JOSEPH
Watuhumiwa wa kesi ya ubakaji na ulawiti kwa kundi wakitoka katika Mahakama Jumuishi ya Utoaji Haki Dodoma jana, baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha jela na kulipa faini ya Sh. milioni moja kwa kila mmoja. Hukumu hiyo ilitolewa jana na Mahakama

WASHTAKIWA wanne wa kesi ya kubaka kwa kundi na kumwingilia kinyume cha maumbile binti mkazi wa Yombo Dovya, Dar es Salaam, wamehukumiwa kifungo cha maisha na faini ya Sh. milioni moja kwa kila mmoja.

Washtakiwa hao walihukumiwa adhabu hiyo baada ya kukutwa na hatia na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma. 

Waliokumbwa na hukumu hiyo ni askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), mwenye namba  MT (Mlinzi wa Taifa) 140105 Clinton Damas, maarufu kama Nyundo, Askari Magereza C.1693 Praygod Mushi, Nickson Jackson ‘Machuche’ na Amin Lema, anayejulikana pia kwa jina la Kindamba. 

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma, Zabibu Mpangule. 

Akizungumza nje ya mahakama, baada ya hukumu hiyo, Mkurugenzi Msaidizi Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Renatus Mkude, alisema kesi hiyo ilikuwa ikiendeshwa katika mahakama ya kificho (falagha) kutokana na aina ya makosa ili kulinda utu wa mwathirika. 

Mkude alisema mahakama hiyo imewakuta watuhumiwa wote wanne na hatia baada ya upande wa Jamuhuri kuwasilisha mashahidi 18 na vielelezo 12 huku washtakiwa wakijitetea wenyewe.

 "Kama tulivyowaomba wananchi wawe watulivu ili mahakama itoe hukumu na leo (jana) hukumu hiyo imetolewa baada ya washtakiwa kukutwa na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha na kulipa faini ya Sh. milioni moja kila moja na adhabu zote zinaenda kwa pamoja," alisema Mkude. 

Alisema kutokana na hukumu hiyo, upande ambao utakuwa haujaridhika, unaruhusiwa kukata rufani kwa ajili ya kutafuta haki. 

Wakili wa Utetezi, Godfrey Wasonga, alisema wanaheshimu uamuzi wa mahakama lakini hawajaridhika na hukumu iliyotolewa kutokana na kasoro mbalimbali zilizokuwamo, ikiwamo nakala ya mashtaka (charge sheet).

 Alisema walikuwa na shaka na uhalali wa nakala ya mashtaka kutokana kuwa na upungufu. 

Wasonga alisema upungufu huo ni pamoja na wao kutokutajiwa eneo lililofanyika tukio lakini cha kushangaza hawajatajiwa muda wa  vitendo hivyo vya kikatili vilivyofanyika.  

Alisema inakuwaje binti alisema amewatambua washtakiwa hao, ilihali ilikuwa usiku na anadai alipigwa vibao na washtakiwa. 

Pia alisema pia binti naye alipaswa kushtakiwa kwa sababu anasema alitongozwa na mtu mmoja aitwaye Kiboi na wakaelewa lakini cha kushangaza mtu huyo hajafikishwa mahakamani. 

Alisema kosa hilo hata binti naye alipaswa kushtakiwa na kuendelea kusisitiza wateja wao bado wana nafasi ya kukata rufani ili kutafuta haki yao. 

Kesi hiyo ilifikishwa katika mahakama hiyo Agosti 19, mwaka huu, na kuanza kusikilizwa mfululizo hadi jana iliposomwa hukumu hiyo.