Walioingiza ndugu zao kama wanufaika TASAF wachunguzwe

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 01:09 PM Apr 17 2024
NAIBU Spika wa Bunge, Mussa Zungu.
PICHA: MAKTABA
NAIBU Spika wa Bunge, Mussa Zungu.

NAIBU Spika wa Bunge, Mussa Zungu, ameiagiza serikali kupeleka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kwaajili ya kuchunguza uwepo wa watu walioingiza ndugu zao kama wanufaika wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) jijini Dar es Salaam.

Zungu ameyasema hayo leo Aprili 17, 2024 bungeni baada ya Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, kujibu maswali ya nyongeza ya Mbunge ya Ulyankulu, Rehema Magilla aliyehoji kuwa Serikali ina mpango wa kuongeza kiwango inachotoa kwa kaya masikini kutoka Sh 20,000 ili watu hao waweze kujikimu kulingana na hali ya Uchumi?.

Akaongeza kuhoji tena, Je serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wale wote waliorukwa kipindi cha utambuzi wanaingizwa kwenye mpango wa kusaidia kaya masikini?

Akijibu maswali hayo, Ridhiwani amesema nia ya serikali ni kuona malipo ya wanufaika yanakuwa makubwa lakini mpango huo umekuwa ukitekelezwa na serikali kwa kushirikiana na wahisani ambao huingiza zaidi ya asilimia 60 kwenye mfuko huo, huku lengo likiwa ni kusaidia kutatua tatizo la umasikini uliokithiri.

“Maboresho yanayofanyika ni sehemu ya kuona mfuko unapanuliwa au fedha zinaongezeka zaidi ili kufikia malengo ambayo Bunge lako na wananchi wangetamani tufikie” amesema Ridhiwani.

Amesema Serikali inaendelea kufanya mazungumzo na wahisani kwa lengo la kuona fedha hizo zinzongezeka ili ikiwezekana zitoke 20,000 hadi kufikia 100,000.