Wagumba wataka kipaumbele kupandikiza mimba Muhimbili

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 10:34 AM Sep 16 2024
Wagumba wataka kipaumbele kupandikiza mimba Muhimbili
Picha;Mtandao
Wagumba wataka kipaumbele kupandikiza mimba Muhimbili

CHAMA cha Wagumba Tanzania kimewasilisha hoja katika Wizara ya Afya na Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kiwe kundi la kwanza kupata huduma ya upandikizaji mimba (IVF) iliyozinduliwa Alhamisi iliyopita katika hospitali hiyo.

Kundi hilo pia linaomba serikali na wadau wengine wa afya kuwasaidia kuchangia gharama ya upatikanaji huduma hiyo ambayo ni Dola za Marekani 5,000 (sawa Sh. 13,611,700) kutokana na wengi wao kuwa na kipato kidogo. 

Akizungumza na Nipashe mwishoni mwa wiki ikiwa ni siku chache baada ya Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango kuzindua jengo la IVF hospitalini huko, Mwenyekiti wa chama hicho, Shamila Makwenjula, alisema kundi hilo linapitia changamoto kadhaa ikiwamo katika afya ya akili. 

"Hospitalini tiba za uzazi ziko juu. Katika chama chetu kuna takribani wanachama 60, wamo pia wanaume. Serikali inapochangia gharama nyingine, basi isaidie na kundi hili. 

"Tuliuliza huduma za upandikizaji hospitali binafsi ilikuwa karibu Sh. milioni 20. Muhimbili bei imeshuka kidogo, lakini kuna mtu hata Sh. milioni moja hajawahi kuishika. 

"Ummy Mwalimu alitupokea, sasa Jenista Mhagama (Waziri wa Afya), apokee kilio chetu serikali itusaidie kwamba sisi tutachangia kiasi kidogo. Kuna wengine wana ugumba ila hawajapata matibabu sahihi, wakitibiwa watapata watoto. 

"Kuna huduma za kliniki za umma za magonjwa mengine, kama yasiyoambukiza, lakini ugumba umewekwa kando," alisema.

Mwenyekiti huyo alisema jamii ina dhana potofu ambazo wanakumbana nazo kama vile kuonekana ni watu walio na mkosi, wasio na tija, huku baadhi wakichukua uamuzi mgumu kwa kutaka kujitoa uhai au kuiba watoto.

 Bingwa wa Afya ya Akili kutoka Idara ya Afya ya Akili Hospitali ya Rufani ya Kanda ya Mbeya (MZRH), Dk. Raymond Mgeni, anasema kundi hilo hukumbwa na magonjwa ya akili kutokana na wengi wao kunyanyapaliwa.

 "Unyanyapaa wanaopata unawaletea athari za wengi kujikuta wakiwa katika msongo wa mawazo ambao unachochea sana wengine kujiua, kunywa pombe na sonona pia," anasema Dk. Mgeni.

 Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Prof. Mohamed Janabi, alisema tayari huduma hiyo imeanza na kliniki kwa kinamama 10 ili kupandikizwa, na kwamba kila siku kati ya wagonjwa 10 wanaoonwa katika kliniki ya kinamama, watatu hadi wanne wana tatizo la uzazi sawa na asilimia 30.