Waganga Tiba Asili kukutana Chalinze, kutoa huduma za kitabibu bure

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 04:06 PM Sep 06 2024
 Dk.Riziki Malela, Mganga Mshauri wa Umoja wa Waganga Afrika Mashariki.
Picha: Pilly Kigome
Dk.Riziki Malela, Mganga Mshauri wa Umoja wa Waganga Afrika Mashariki.

WAGANGA Watafiti wa Tiba Asili wapatao 250 kutoka Afrika wanakutana nchini Tanzania kutembelea Mzimu wa Afrika uliopo Chalinze mkoani Pwani na kutoa huduma za kitabibu bure kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na magonjwa sugu.

Hayo yamebainishwa na Dk.Riziki Malela Mganga Mshauri wa Umoja wa Waganga Afrika Mashariki alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari mkoani Dar es Salaam.

Dk. Malela amesema maadhimisho hayo ya mwaka mmoja yatakutanisha waganga hao kwa siku tatu kuanzia  Septemba 6 yanayotarajiwa kukutanisha waganga kutoka Afrika kutoka Tanzania, Nigeria, Rwanda, Burundi, AfrikaKusini, Ethiopia,Kenya,Uganda watakutana Chalinze kwaajili ya kuboresha huduma za kimatibabu.

Amebainisha kuwa mkusanyiko huo umekuja kutembelea mzimu wa Afrika waliouzindua mwaka jana 2023 uliopo Chalinze ikiwa na pamoja kukutana na kubadilishana ujuzi wa kitabibu kwa waganga hao

“Tunakwenda kuidhihirishia dunia kwamba tiba asili zipo na Tanzania ndio waasisi wa tiba zote za asili zilizopo ulimwenguni kwa sasa, pia tunawaasa watanzania wasidharau tiba asili na mizimu waachane na waganga wa kishirikina” amesema Malela

Nae Mwenyekiti Kitaifa Shirika la Waganga wa Mitishamba na Utafiti Kenya, Ali Suleiman amesema wamekuja Tanzania kwa ajili kujifunza na kubadilishana ujuzi wa matibabu kutoka kwa wenzao ikiwemo na kujifunza kazi zinazofanywa na Mzimu katika kusaidia jamii katika tiba za mwanadamu.

1

Amesema mzimu huo umendaliwa kwajili ya kuwasaidia watibabu Afrika kuwaongezea nguvu kwa ajili ya yale magonjwa ambayo ni sugu na mazito katika kuwasaidia kuwatibia wagonjwa ikiwemo na kufanya maombi kutokana na changamoto zinazowakumba katika kazi zao.

Aidha aliziomba serikali zote Afrika iwaunge mkono katika kuwabaini na kuwasaka waganga wapotoshaji wanaoiaminisha jamii kuwa ni waganga kumbe ni matapeli wanafanya uharifu kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kwa kuiteketeza jamii kwa vitendo viovu.

Masudi Mkali Mganga wa tiba asili kutoka Urambo Tabora amesema maadhimisho hayo ya mwaka mmoja ya mzimu wa Afrika wanataka waanze kuwasaidia watanzania wenye changamoto mbalimbali za kiafya wajitokeze ili waweze kupata matibabu na kumaliza changamoto zao kupitia mzimuhuo.

“Tutatoa huduma za kuwahudumia wagonjwa wote bure huku tukiwa na malengo kuwaaminisha watanzania na Waafrika waone umuhimu wa kudumisha mila na desturi pamoja na kuwaaminisha matibabu ya mitishamba inaponya” amesema Mkali