SERIKALI imesema taasisi za vyuo vikuu, zina mchango mkubwa katika utekelezaji wa vipaumbele vya Haki na Usawa wa Kiuchumi, kupitia Programu ya Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa (GEF).
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu, ameyasema hayo leo, jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi mkutano kuhusu GEF, uliowahusisha makamu wakuu wa vyuo vikuu nchini.
Mkutano huo ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia masuala ya Wanawake (UN Women), kwa kushirikiana na wizara hiyo, umehudhuriwa pia na Mshauru wa Rais na Mwenyekiti wa Kamati ya Ushauri ya Taifa GEF, Angellah Kairuki.
Mdemu akieleza kuhusu GEF, amesema malengo ni kutimiza azma ya nchi kufikia usawa wa kijinsia miongoni mwa jamii na mwendelezo wa utekelezaji wa Azimio la Ulingo wa Beijing la Mwaka 1995.
“Azimio lilitoa maeneo 12 ya utekelezaji na kila nchi ilipaswa kuchagua maeneo yake ya vipaumbele kwa ajili ya utekelezaji, ili kufikia usawa wa kijinsia. Hivyo, Tanzania kama nchi ilichagua maeneo matano ya utekelezaji.
“Maeneo hayo ni; uwezeshaji wanawake kiuchumi; kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto; kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi; elimu, mafunzo na ajira na uingizaji wa masuala ya jinsia katika sera za kisekta,”amesema Mdemu.
Amesema kwamba kupitia malengo hayo, vyuo vikuu vina mchango mkubwa katika utekelezaji kwa sababu huko ndiko wanakowalea na kuwakuza vijana na pia hizo ni taasisi kitovu cha tafiti mbalimbali ambazo ni muhimu katika kupanga mipango na kuandaa sera jumuishi.
“Naamini kwa ushirikiano wa pamoja tutaweza kutekeleza ahadi za nchi kwenye Jukwaa hilo sambamba na kumuwezesha Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Tanzania ambaye ni kinara wa Jukwaa hilo kuendelea kung’ara.”
Naibu Mwakilishi wa UN Women nchini, Katherine Gifford, amesema kwamba: “Tunayofuraha kuwa hapa leo kuzungumza na wasomi wanavyoweza kuendesha, kuainisha ahadi za GEF Tanzania.
Tunatazamia kubadilishana uzoefu na mitazamo kuhusu jukumu muhimu la vyuo vikuu na taasisi za kitaaluma katika kuendeleza ajenda hii ya kimataifa,” amesema Katherine.
Amesema UN Women inatambua umuhimu wa wasomi katika kushughulikia uwapo wa usawa wa kijinsia akisema zina uwezo wa kushawishi sera, kuunda kanuni za kijamii na kuwaandaa viongozi wajao kwa maarifa na zana za kukuza usawa wa kijinsia.
“Tunaposonga mbele tunahitaji kujenga uhusiano thabiti kati ya wasomi na washikadau katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na serikali na viwanda.
Kwa kufanya hivyo, tunaweza kuhakikisha utafiti unaofanyika ndani ya vyuo vikuu, unatafsiriwa duniani kwa usawa wa kijinsia,” amesema.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Dodoma (UDOM), Prof, Wineaster Saria, amesema kwamba mkutano huo umeongeza uzoefu katika masuala ya kijinsia hasa kuyazungumzia kuanzia ngazi ya chini hadi vyuo vikuu.
“Kazi kubwa niliyoiona na ya msingi ni vyuo vya hapa nchini, kujifunza kutoka kwa wenzetu wa vyuo vya Kenya, kupitia utafiti wao namna wanavyotekeleza masuala haya ili jinsi zote kuwa na fursa sawa,” amesema Prof. Saria.
Amesema ili kukuza usawa wa kijinsia malezi yenye mrengo huo ni muhimu kuanzia ngazi ya nyumbani na hatimaye taasisi za elimu ya juu kutilia mkazo masuala hayo.
Profesa Judith Waudo kutoka Chuo Kikuu Nairobi, kilichopo nchini Kenya, amesema ni wakati wa wanazuaoni kufikisha matokeo ya tafiti wanazozifanya kwa umma kwa lugha rahisi kufikisha ujumbe na kuleta matokeo chanya.
“Mara nyingi tunafanya tafiti na kuzifungia hii maana yake tunazungumza wenyewe kwa wenyewe, bila kujali kuhusu wananchi. Tumejitahidi kufikisha ujumbe kwa umma kupitia miradi tunayofanya kutoka chuoni,” amesema Prof. Waudo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED