NAIBU Waziri wa Nishati, Salome Makamba amezindua rasmi mradi wa kufunga mifumo ya umeme Jua maeneo ya visiwani kwa bei ya ruzuku utakaoondoa changamoto ya upatikanaji umeme na kuhudumia visiwa 120 vya Tanzania bara.
Mradi huo wenye thamani ya Sh. bilioni nane ambao serikali itagharamikia asilimia 75 na wananchi asilimia 25 ili kuunganishwa na umeme, umezinduliwa leo Februari 21, 2026 katika kisiwa cha Bezi kilichopo Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, ambapo utatekelezwa kwa muda wa miaka miwili hadi Mei, 2027.
Mikoa itakayonufaika na mradi ni pamoja na visiwa vya mikoa ya Mwanza, Geita, Kagera, Mara, Rukwa, Lindi, Mtwara na Pwani.
Imeelezwa kuwa kwa Mkoa wa Mwanza pekee mifumo 8,410 ya umeme huo itafungwa katika visiwa 65 kwa gharama ya Sh. bilioni 4.8, vikiwemo visiwa vitatu vya Bezi, Tefu na Ukara.
Akizungumza baada ya kuzindua mradi huo, Waziri wa Salome, amesema ni muhimu kwa ustawi wa wakazi wa visiwa hivyo, kwakuwa serikali ina nia thabiti ya kuhakikisha wakazi wa maeneo hayo ambayo hayako kwenye gridi ya taifa wanapata nishati ya uhakika.

"Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi hii kwa ubora na viwango vinavyokidhi matarajio ya wananchi. Tunasisitiza mkandarasi aongeze kasi na miradi ikamilike kwa wakati," amesema Makamba.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Jones Olotu amesema lengo la serikali ni kuunga wateja wapya milioni 8.3 ifikapo mwaka 2030, na kati ya Sh. Bilioni 4.8 zinazohitajika kugharamia mradi wa visiwa 65 mkoani Mwanza, tayari serikali imeshalipa ruzuku ya Sh. Bilioni 3.3 huku kiasi kinachobaki Sh. Bilioni 1.5 kitalipwa na wananchi kama ruzuku.
Ameongeza kuwa kisiwa cha Bezi kina kaya na vibanda vya biashara 600, na kaya 300 zilikuwa zimeunganishwa na umeme wa sola, hivyo kutokana na uhitaji kuwa mkubwa wamelazimika kutafuta mkandarasi atakayefunga mifumo zaidi ya 2,000 utakaonufaisha kaya takribani 500.
Imeandikwa na Damian Maira
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED