VIJANA kote nchini wametakiwa kuchangamkia fedha za mikopo Sh. bilioni 200 ambazo zimetolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, kupitia Ofisi ya Rais Maendeleo ya Vijana, kwa ajili ya kuwakwamua kiuchumi.
Witu huo umetolewa leo Februari 21, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, wakati akizungumza na vijana wa Shinyanga, kwenye hafla ya uzinduzi wa jukwaa la vijana mkoani humo.
Nanauka amesema, Rais Samia aliahidi kutoa fedha Sh. bilioni 200 kwa ajili ya uwezeshaji wa vijana, na kwamba fedha hizo tayari ameshakabidhiwa na Waziri Mkuu, na baadhi ya vijana wameshaanza kunufaika nazo.
“Ninafuraha kuwaambia kwamba, fedha ambazo Rais Samia aliahidi kutoa kwa ajili ya vijana Sh. bilioni 200, fedha hizo tayari nimeshazipokea,” amesema Nanauka.
Amesema, fedha hizo ni kwa ajili ya vijana, na zimesambazwa katika sekta mbalimbali, ikiwamo Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Kilimo, Mawasiliano na Teknolojia ya habari, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Viwanda na Biashara, na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jinsia na makundi maalumu.
Amesema, dhamira ya Rais Samia kutoa fedha hizo, ni kuona vijana wanakuwa wabunifu, wanachapa kazi na kuinuka kiuchumi, na kwamba kupitia fedha hizo, tayari vijana kutoka Jijini Mwanza wameanza kunufaika nazo na wamepata Sh. milioni 200, na kuwataka vijana kote nchini, wasibweteke bali wachangamkie fursa ya fedha hizo bilioni 200.
Aidha, amesema masharti magumu ambayo yalikuwa kikwazo kwa vijana kunufaika na mikopo mbalimbali yameondolewa, kikiwamo kigezo cha dhamana isiyo hamishika, na pia watakuwa wakirejesha marejesho kuanzia miezi mitatu hadi sita.
Katika hatua nyingine, ametoa nasaha kwa vijana, kwamba iliwapate kufanikiwa katika maisha yao, ni lazima wawe na ndoto kwa ajili ya kesho yao, kuwa na nidhamu ya muda, pamoja na kuweka nguvu ya kutimiza malengo ya jambo lao, na wasikubali kukatishwa tamaa na mtu yoyote.
“vijana ni nguvu kazi ya taifa, na asilimia 55 ya wazalishaji ni vijana, na ndiyo maana serikali imeamua kuwekeza kwa vijana na kutenga fedha kwa ajili ya kuwawezesha, pamoja na kuwajengea ujuzi kupitia VETA na serikali imeshatoa bilioni 3, na vijana wengi wapo VETA,” amesema Nanauka.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita, amewataka vijana mkoani humo kuchangamkia fursa mbalimbali ambazo zipo, ikiwamo kufungua viwanda vidogo, ambapo kuna maeneo ya uwekezaji tayari yameshatengwa na fedha zipo za kuwawezesha, ili wajikwamue kiuchumi.
Nao baadhi ya vijana walioshiriki kwenye uzinduzi wa jukwaa hilo, wamesema wanafarijika serikali kuanzisha Wizara ya vijana, ambayo imekuwa ikiwasemea mahitaji yao, na wengine wamekuwa wanufaika wa mikopo ya asilimia 10, ambayo nne hutolewa kwa vijana.
© 2026 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED