Utafiti wafanywa athari za mikaratusi katika mazingira

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 02:58 PM May 01 2024
Miti ya mikaratusi.
PICHA: MAKTABA
Miti ya mikaratusi.

SERIKALI kupitia Taasisi ya Utafiti wa Misitu Tanzania (TAFORI) inaendelea na utafiti wa kina wa miti aina ya mikaratusi kuhusu athari zake kimazingira na kuja na taarifa ya kitaalamu pamoja na ushauri, Bunge lilielezwa jana mjini hapa.

 Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Khamis Hamza Khamis,  amesema hayo alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Hai (CCM), Saashisha Mafuwe.

Katika swali hilo, Mafuwe ametaka kujua tamko la serikali kuhusu kuteketeza miti ya mikaratusi nchini baada ya utafiti kuonyesha kuwa inaharibu mazingira.

Akijibu swali hilo, Khamis  amesema baada ya utafiti kukamilika, Ofisi ya Makamu wa Rais na Wizara ya Maliasili na Utalii zitatoa elimu kwa wananchi kuhusu miti hiyo.

Amesema kuna zaidi ya aina 500 za miti ya mikaratusi duniani na Tanzania kupitia TAFORI, imeruhusu aina 25 za miti hiyo ili kupata fursa mbalimbali zitokanazo na mikaratusi hasa kwenye viwanda vya mazao yaliyosindikwa.

 ”Serikali kupitia Wizara ya Maji, Maliasili na Utalii pamoja na sisi Mazingira tumegundua iko miti inayokunywa maji na inapunguza au kuchangia vyanzo vya maji kupotea. Pia tumegundua ziko aina tofauti kwa mfano ziko zaidi ya 20 na zinatumia maji, hivyo tuko katika mpango wa kuzifanyia utafiti,” amesema.

Hata hivyo, amewahimiza wananchi kuendelea kupanda miti kwa wingi wakati serikali inaendelea kufanya tafiti kuhusu miti ya mikaratusi kubaini athari za kimazingira.