Ulega agawa madume ya ng’ombe kwa wafugaji

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 11:23 AM Sep 17 2024
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, akikabidhi madume ya ng’ombe kwa vikundi vya wafugaji.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, akikabidhi madume ya ng’ombe kwa vikundi vya wafugaji.

WAZIRI wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, amekabidhi madume bora ya ng’ombe wa nyama 20 kwa vikundi vya wafugaji wa kijiji cha Msomera ili wasaidie kuzalisha kizazi chenye uwezo wa kutoa nyama nyingi zaidi ya wale wa asili walioko nchini.

Waziri Ulega alikabidhi madume bora ya ng’ombe wa nyama kwa vikundi vya wafugaji katika hafla fupi iliyofanyika katika kijiji cha Msomera, wilayani Handeni, mkoani Tanga, mwishoni mwa wiki.

“Tukio hili ni kutimiza mpango wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi wa kuleta mabadiliko kwenye sekta ya mifugo kupitia kuboresha mbari za mifugo kwa njia ya uhimilishaji na kuwapatia wafugaji madume bora,” alisema.

Alisema Tanzania inakadiriwa kuwa na jumla ya ng’ombe milioni 36.6 na kati ya hao, asilimia 97 ni wa asili.  Sehemu kubwa ya uzalishaji wa nyama na maziwa hapa nchini inategemea zaidi ng’ombe wa asili. 

“Ng’ombe wetu wa asili wana uwezo wa kustahimili magonjwa na hali ya mazingira ya maeneo mengi ya Tanzania. Hata hivyo pamoja na sifa hizo, ng’ombe hawa wana uzalishaji mdogo wa nyama na maziwa. Ili kuongeza uzalishaji wa nyama na maziwa, mbinu mojawapo ni kuzalisha mifugo chotara na kuboresha mazingira ya utunzaji ikiwamo lishe. Ng’ombe wa asili wana uwezo wa kuzalisha nyama kilo 80 hadi 120, lakini wakiboreshwa wanakuwa na uwezo wa kuzalisha kilo 150 hadi 200,” alifafanua.

Aidha, alisema kutokana na juhudi za Dk. Rais Samia Suluhu Hassan za kutafuta masoko ya nje, soko la bidhaa ikiwamo nyama kutoka Tanzania limeongezeka kwa haraka. Mfano mauzo ya nyama nje ya nchi yameongezeka kutoka tani 10,415 mwaka 2021/2022 zenye thamani ya USD milioni 42.5 hadi tani 14,701.10 zenye thamani ya USD milioni 61.4 katika mwaka wa fedha 2022/2023. 

“Ili soko liwe endelevu na linalozingatia ubora wa nyama wizara inachukua hatua za kuboresha mifugo, lishe, upatikanaji wa maji na afya ya mifugo ili kuongeza uzalishaji na ubora wa nyama ikiwamo kuhakikisha kuwa wafugaji wanapata mbegu bora.”

 Alibainisha kuwa katika mwaka wa fedha wa 2023/2024 wizara imenunua madume 200 aina ya Boran yenye thamani ya Sh. milioni 511.2 na Kijiji cha Wafugaji cha Msomera kimepatiwa madume 20. 

Vilevile, alisema kuwa katika mwaka 2024/2025 wizara imepanga kununua madume 66 ya nyama aina ya Brahman kutoka nje ya nchi yenye thamani ya Sh. milioni 990 ambayo yatakopeshwa kwa wafugaji kwa mkopo wa miaka miwili bila riba kupitia Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB). Utaratibu wa kuwakopesha wafugaji unafanyika ili zoezi hili liwe endelevu kwa fedha hizo kununulia madume mengine.

Pia, Waziri Ulega alisema wizara yake inawahamasisha wafugaji wote nchini kuachana na ufugaji wa mazoea na kufuga kibiashara. Moja ya hatua muhimu ya kuelekea kufuga kibiashara ni kuwa na mbegu bora za mifugo zenye uwezo wa kuzalisha mazao mengi. Serikali inatoa madume haya ili yawe hamasa kwa wafugaji kuendelea kununua mbegu bora baada ya kuona matokeo mazuri ya ndama wanaotokana na madume haya. 

Alisema serikali inaendelea kuhakikisha kuwa Kijiji cha Msomera kinakuwa kijiji cha mfano cha wafugaji. Pia itahakikisha kuwa mahitaji yote muhimu kwa ajili ya mifugo yakiwamo majosho, minada, vituo vya kukusanyia maziwa, machinjio, malisho na maji vinakuwapo Msomera.