TEC yawakutanisha vigogo CCM, CHADEMA

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 12:45 PM Sep 16 2024
TEC yawakutanisha vigogo CCM, CHADEMA
Picha:Mtandao
TEC yawakutanisha vigogo CCM, CHADEMA

BARAZA la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) limewakutanisha viongozi wa CCM na CHADEMA, likionya kuwa tunu za undugu na amani nchini zimeshambuliwa kutokana na matukio ya kutekwa, kuteswa na kuuawa kwa Watanzania yanayoendelea.

Viongozi hao ni Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu, Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, Katibu Mkuu wa CHADEMA, John Mnyika, Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu - Sera, Bunge na Uratibu, William Lukuvi.

Akiwatambulisha viongozi hao jana kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Dk. Charles Kitima, alisema walikwenda kushiriki Kilele cha Kongamano la Tano la Ekaristi Takatifu la Kitaifa.

Padri Kitime aliwaita na kuwasimamisha kwa pamoja viongozi hao jukwaani kuwatambulisha kisha aliwakumbusha kuwa wao ni ndugu, hivyo wakaishi kwa upendo, wakapeleke tunu ya injili na kusambaza upendo katika vyama vya siasa.

Alisema historia ya viongozi inaonesha kuwa walilelewa kwenye misingi ya kikatoliki, hivyo wakaienzi Ekaristi kwa kuendeleza upendo na undugu.

Akimtambulisha Lissu, Padri Kitime alikumbusha kuwa mwaka 2017 alipokwenda kumjulia hali Nairobi alikolazwa baada ya kupigwa risasi na watu ambao mpaka leo hawajulikani na kumweleza kuwa awasamehe watu hao; naye akamjibu kuwa "Niwasamehe wakati siwajui?"

Alisema kuwa Lissu pia alimweleza kuwa Mungu yupo na ameona ukuu wake.

Katibu Kitime alisema Balozi Dk. Nchimbi alisoma Shule ya Sekondari Uru Seminari yenye maadili ya kidini huku Mnyika alisoma Shule ya Sekondari Maua Seminari.

"Ninyi nyote ni ndugu, hivyo mkaishi kwa upendo, pelekeni tunu ya injili katika vyama vya siasa," Padri Kitime alitoa malekezo hayo ya kanisa.

KAULI YA TEC

Akisoma salamu za TEC, Makamu wa Rais wa baraza hilo, Askofu Eusebius Nzigilwa, alisema kuwa hivi sasa tunu za undugu na amani ya nchi  zimeshambuliwa kutokana na matukio ya kuteka, kutekwa, kuumizwa na kuuawa Watanzania yaliyotokea hivi karibuni.

Alisema Tanzania kwa miaka mingi inajulikana kama kisiwa cha amani, udugu na mahali pekee Afrika ambapo raia wake wameendelea kuishi kwa umoja, amani na undugu licha ya tofauti zao za kikabila, kiimani, kiitikadi na kiuchumi.

"Tunajiuliza nini kimepotea kwenye tunu yetu hii? Taifa letu limepotea wapi? Je, uongozi na mamlaka husika pamoja na vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimezidiwa nguvu na maarifa hata kushindwa kudhibiti hali hii?" alihoji.

Alisema TEC haiamini kama makundi hayo ya kihalifu yana nguvu kuliko vyombo vya ulinzi na usalama na kuviomba vitimize majukumu yao, ili kurudisha heshima ya taifa ya kuwa kisima cha undugu na amani.

Alitoa pole kwa ndugu wa waliouawa na wale walioumizwa katika matukio hayo na wanaungana na taaaisi na jumuiya za kimataifa kulaani.

"Tunaunga mkono wito wa viongozi na watu mbalimbali wa kufanyika uchunguzi wa kina na haraka, ili wale wote waliohusika na matukio hayo yafikishwe mbele ya sheria," alisema.

Alisema pia wanakemea vitendo hivyo vya kihalifu na kuunga mkono wito wa viongozi na watu mbalimbali wa kufanyika uchunguzi wa kina na haraka, ili waliotekeleza vitendo hivyo wafikishwe mbele ya sheria na wale ambao hawakuwajibika kwa kadili ya nafasi zao wawajibishwe.

"Uhai ni zawadi kutoka kwa Mungu, mtu ameumbwa kwa sura na mfano Mungu mwenyewe, hivyo maisha na utu wa mtu ni lazima viheshimiwe na kulindwa kwa nguvu zote," alisema.

Septemba 8, mwaka huu, mara baada ya kuripotiwa kifo cha Mjumbe wa Sekretarieti ya CHADEMA Taifa, Ali Kibao, Rais Samia Suluhu Hassan alituma salamu za pole kwa viongozi wa chama hicho, familia, ndugu, jamaa na marafiki huku akiagiza vyombo vya uchunguzi kumpelekea haraka taarifa ya kina kuhusu tukio hilo na mengine ya namna hiyo.

"Nchi yetu ni ya kidemokrasia na kila raia ana haki ya kuishi. Serikali ninayoiongoza haivumilii vitendo vya kikatili vya namna hii," alisema.

Mwili wa Kibao uliokotwa katika eneo la Ununio wilayani Kinondoni baada ya kutekwa na watu wasiojulikana ndani ya basi la Tashriff wakati akitoka Dar es Salaam kwenda Tanga. Kwa mujibu wa mashuhuda waliokuwa katika basi hilo, watu waliokuwa na bunduki na pingu. 

Mbali na Kibao, kumekuwa na matukio ya watu kutekwa, kuuawa na kujeruhiwa na watu wasiojulikana yanaripotiwa mara kwa mara, hata kutishia amani na kuwaibua wanaharakati na viongozi mbalimbali kuyakemea.

Rais wa TEC, Askofu Wolfgang Pisa, alisema amefurahishwa kuwaona viongozi hao wa vyama vya siasa wamekaa pamoja, jambo linaloonesha kuwa kuna nguvu ya kuwaweka watu pamoja katika Ekaristi.

KAULI YA BITEKO

Naibu Waziri Mkuu, Dk. Dotto Biteko, alisema maadhimisho ya Ekaristi hiyo yawakumbushe Wakristo na Watanzania wote kuishi kama ndugu kwa kuhurumiana na kutoruhusu tofauti za mitazamo ziwatenganishe na kuwagombanisha.

Alisema nchi itajengwa kwa pamoja kupitia uongozi na kusisitiza siasa za kustahimiliana na kuvumiliana, zenye lengo la kubadilisha hali za Watanzania kwa kuwaondoa katika umaskini na kuwatengenezea hali bora.

Dk. Biteko pia alitoa wito kwa Watanzania kushiriki Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa kujiandikisha katika Daftari la Wakazi kuanzia Oktoba 11 hadi 20 mwaka huu. Uchaguzi huo utafanyika Novemba 27, mwaka huu.

"Yule atakayegombea na atakayekwenda kumpigia kura mwenzake, tufanye hivyo kwa kusaidiana huku tukijua kuwa hatuna pa kwenda," alisema.

Viongozi wengine walioshiriki maadhimisho hayo ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila na Spika wa Bunge mstaafu, Anne Makinda.