Spika ataka serikali kuwapa ajira vijana wanaojitolea

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 12:11 PM Oct 30 2024
Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.
Picha: Mtandao
Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.

SPIKA wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, ameitaka serikali kuangalia vigezo vinavyotumika kuajiri kwa kuwa vimekuwa vikiwaumiza wanaojitolea kwa kukosa fursa ya ajira.

Dk. Tulia alisema hayo bungeni jana baada ya kumhoji Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene, kuhusu mwongozo wa watu wanaojitolea kwenye kada mbalimbali zikiwamo madaktari, manesi na walimu kama umetolewa.

Simbachawene alilieleza Bunge kuwa “Tutautoa lakini tulifika mahala tukapata changamoto hasa kwenye vigezo, hata hivyo tunashirikiana na kamati kulijadili hili kwa pamoja ili tupate mawazo zaidi kwa sababu vigezo vinatusumbua sana.”

Kutokana na majibu hayo, Spika Tulia alisema: “Mngetusaidia kama hili linahitaji mawazo mapana tungeshirikisha watu wengi zaidi, kwasababu ajira zimetolewa hivi karibuni. Kwa  mfano kuna madaktari wako kwenye hospitali kwa mkataba huo huo wa kujitolea wanalipwa nusu na hawa wamekuwa wakiwafundisha wanaokuja kupata mafunzo ya uzoefu kazini (interns).

“Halafu kwenye ajira wanaajiriwa ‘interns’ wanaachwa licha ya kwamba wote waliomba. Hivi  ni vigezo gani vinavyotumika kumwajiri huyu ‘intern’ wakati vinamwacha yule ambaye amemfundisha ‘intern’ kazini? Mtazame  hivyo vigezo maana vinawaumiza watoa huduma kule.”

Awali, katika swali la nyongeza, Mbunge wa Viti Maalum (CHADEMA), Grace Tendega,  alihoji katika mchakato wa ajira mpya za walimu 11,015 zilizotangazwa hivi karibuni kama zimezingatia wanaojitolea kwa muda mrefu.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zainab Katimba, akijibu swali hilo, alisema Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ilishatoa utaratibu wa watu waombe na kwamba watazingatiwa kwa uzoefu na kujitolea kwenye maeneo wanayofanya kazi.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Anastazia Wambura, alihoji lini serikali itapeleka walimu wa kutosha wa shule za msingi na sekondari mkoani Mtwara.

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri Katimba alisema serikali imekuwa ikiajiri walimu wa shule za msingi na sekondari kila mwaka kulingana na upatikanaji wa fedha.

“Katika kipindi cha mwaka 2020/21 hadi 2022/23, serikali iliajiri walimu 29,879 wakiwamo walimu 16,598 wa shule za msingi na walimu 13,281 wa shule za sekondari. Mkoa wa Mtwara ulipangiwa walimu 968 wakiwamo 502 wa shule za msingi na 466 wa shule za sekondari,” alisema.

Alisema Julai 20, mwaka huu, serikali ilitangaza ajira za walimu 11,015 na mchakato wa ajira ukikamilika watapangiwa vituo vya kazi.

“Mkoa wa Mtwara utapata walimu 502 wakijumuisha walimu 184 wa shule za msingi na 318 wa shule za sekondari,” alisema.