Silaa azindua mnara wa mawasiliano Kata ya Makuru, Singida

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:55 PM Oct 23 2024
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa.

Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, amezindua mnara wa mawasiliano ya simu uliojengwa katika kijiji cha Hika Kata ya Makuru, wilayani Manyoni Mkoani Singida.

Mnara huo uliojengwa na Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa ruzuku inayotolewa na Serikali kupitia Mfuko wa Mwasiliano kwa Wote (UCSAF), ni muendelezo wa juhudi za Serikali katika kuboresha upatikanaji wa huduma za mawasiliano katika maeneo ya vijijini ili kuhamasisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo hayo.

Akizungumza kwenye uzinduzi huo, Silaa amesema dhamira ya Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na  Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha kuwa maeneo ya vijijini yanafikiwa na huduma bora za mawasiliano ikiwemo mtandao wa intaneti.

Gharama ya jumla ya ujenzi wa manara huo ni sh. milioni 272 kati ya hizo UCSAF imetoa ruzuku ya sh.milioni 118 na TTCL imetoa zaidi ya sh. milioni 150. Jumla ya wananchi takribani 24,000 katika kijiji cha Hila, Londoni na Msemembo na vijiji vya jirani watanufaika na kuwepo kwa mnara huo.