HALMASHAURI ya Manispaa ya Shinyanga, imejipanga kuimarisha hali ya usafi wa mazingira, ili kulinda tuzo ya usafi ambayo ilishinda kutoka Wizara ya Afya.
Hayo yamebainishwa jana, kwenye Kikao cha Baraza la Madiwani cha Robo ya Pili, wakati wa uwasilishwaji wa taarifa ya Kamati ya Mipango Miji na Mazingira.
Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Revocatus Lutunda, alibainisha hayo wakati akijibu swali alililoulizwa na Diwani wa Kizumbi, Rubeni Kitinya, juu ya uimarishaji wa usafi wa mazingira katika manispaa hiyo.
Amesema, ili kuendelea kulinda hadhi ya manispaa hiyo kuwa mji safi na kulinda tuzo, wameweka mikakati madhubuti ya kuendelea kuimarisha hali ya usafi zaidi, pamoja na kukumbusha wananchi kufanya usafi katika maeneo yao.
“Suala la usafi kwa kweli katika mji wetu tumelegalega hali siyo nzuri, lakini tumeweka mikakati ya kuimarisha usafi zaidi, kukumbusha wananchi kufanya usafi, pamoja na kutenga siku maalumu ya kuwa tunafanya usafi, ili kuendelea kulinda heshima ya tuzo yetu ya usafi wa mazingira,” amesema Lutunda.
Meya wa Manispaa ya Shinyanga, Elias Masumbuko, naye amesisitiza suala la usafi kwenye mji huo na kwamba, uchafukwa sasa umeanza kuoneka na jitihada zinahitajika, ili kuendelea kulinda heshima yao ya kupata tuzo ya ushindi wa usafi wa mazingira ngazi ya miji.
Amewalalamikia pia mawakala wa kukusanya uchafu, kuwa wameshindwa kufanya kazi zao vizuri, huku wakati wa kupeleka taka dampo, baadhi huagushwa hovyo barabarani na kusababisha mji kuonekana mchafu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED