Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limewaua kwa risasi watu wawili waliodaiwa kuwateka wanafunzi wawili wa shule ya Blessings Model School iliyoko Nyasaka, Manispaa ya Ilemela.
Kwa mujibu wa taarifa, watekaji hao, ambao majina na umri wao bado havijatambulika, waliteka wanafunzi hao mnamo Februari 5, 2025, majira ya saa 12 asubuhi, katika eneo la Kapriponti, Jijini Mwanza.
Tukio hilo lilianza baada ya mtu mmoja asiyejulikana kuomba lifti kwenye gari la shule lililokuwa limebeba wanafunzi sita.
Baada ya kupanda gari hilo, mtu huyo alimshambulia dereva kwa kumkaba shingoni kutoka nyuma, kisha kuwateka watoto wawili na kuondoka nao kwa kutumia pikipiki mbili zilizowasili muda mfupi baada ya gari kusimama.
Mara baada ya utekaji, wahalifu hao walianza kuwasiliana na uongozi wa shule kupitia ujumbe wa vitisho, wakidai fedha ili kuwaachia watoto hao.
Polisi waingilia kati
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, DCP Wilbrod Mutafungwa, amesema kuwa mnamo Februari 8, 2025, majira ya saa 6:30 mchana, siku tatu baada ya tukio, walipokea taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu uwepo wa watekaji hao katika nyumba moja iliyopo Mtaa wa Nyaburogoya, Kata ya Nyegezi.
"Baada ya kupata taarifa, askari walifika eneo la tukio na kufanikiwa kuwaokoa wanafunzi wawili waliokuwa mikononi mwa watekaji. Mmoja ni wa kike mwenye umri wa miaka minane na mwingine wa kiume mwenye umri wa miaka mitano," alisema Kamanda Mutafungwa.
Hata hivyo, alipofika katika nyumba hiyo, jeshi la polisi lilikumbana na upinzani kutoka kwa watekaji hao waliokuwa wamejihami kwa mapanga, nondo, na majambia. Polisi walilazimika kutumia risasi za moto, hatua iliyosababisha vifo vya watekaji hao papo hapo.
Watoto waliokolewa wamepelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza Sekou Toure kwa uchunguzi wa afya, huku miili ya watekaji hao ikihifadhiwa katika hospitali hiyo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED