MKUTANO wa pamoja wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), wamekubaliana hatua muhimu 13 kuchukuliwa, ikiwamo kusitishwa kwa mapigano mara moja katika eneo la Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mkutano huo wa dharura, uliofanyika leo, Februari 8, mwaka huu, jijini Dar es Salaam, umeongozwa kwa pamoja na Mwenyekiti wa EAC na Rais wa Kenya, Wiliam Ruto na Mwenyekiti wa SADC na Rais wa Zimbabwe, Dk. Emmerson Mnangagwa.
Mkutano huo, uliohudhuriwa na marais kutoka jumuiya hizo, masuala mengine waliyokubaliana ni kurejesha huduma muhimu na njia za usambazaji wa chakula na bidhaa nyingine, ili kuhakikisha msaada wa kibinadamu haukwami.
Mengine ni utatuzi wa mzozo na amani kupitia mchakato wa Luanda na Nairobi, huku mkutano huo wa pamoja ukizingatia ripoti ya mkutano wa mawaziri wa EAC na SADC, kuhusu hali ya usalama Mashariki mwa DRC na kusisitiza ushirikiano ya kisiasa na kidiplomasia ndiyo suluhisho endelevu zaidi la mzozo eneo hilo.
Pia, mkutano huo wa pamoja umeagiza Wakuu wa Majeshi ya Ulinzi ya katika nchi za EAC na SADC, kukutana ndani ya siku tano na kutoa maelekezo; kwanza kusitisha mapigano mara moja na bila masharti na kusitisha uhasama; utoaji wa usaidizi wa kibinadamu ikijumuisha kuwarejesha nyumbani marehemu na kuwahamisha waliojeruhiwa;
Lingine ni kuendeleza mpango wa kuweka usalama kwa eneo Goma na maeneo ya jirani; ufunguzi wa njia kuu za usambazaji misaada ikijumuisha Goma-Sake Bukavu; Goma-Kibumba-Rumangabo-Kalengera Rutshuru-Bunagana; na Goma-Kiwanja-Rwindi-Kanyabayonga-Lubero pamoja na Ziwa Kivu kati ya Goma na Bukavu.
Kadhalika makubaliano ni kufunguliwa tena mara moja kwa Uwanja wa Ndege wa Goma na kushauri kuhusu afua zingine zinazohusiana na uwezeshaji.
Mkutano wa pamoja ulikumbusha tena jukumu muhimu la mchakato wa Luanda na Nairobi na kuagiza kwamba, mambo hayo mawili yaunganishwe na kuwa Mchakato wa Luanda/Nairobi.
Mkutano pia uliazimia zaidi kuimarisha michakato hiyo miwili, ili kuongeza utimilifu na kuwapa mamlaka wenyeviti wenza, kwa kushauriana na Umoja wa Afrika (AU).
Pamoja na marais wa Kenya na Zimbabwe, mkutano huo pia umehudhiriwa na mwenyeji Tanzania, Rais Samia Suluhu Hassan; Rais Félix Tshisekedi wa DRC; Cyril Ramaphosa, Rais wa Afrika Kusini.
Wengine ni, Hassan Sheikh Mohamoud, Rais wa Somalia; Paul Kagame, Rais wa Rwanda; Yoweri Museveni, Rais wa Uganda; Hakainde Hichilema, Rais wa Zambia.Viongozi wengine waliohudhuria ni wawakilishi marais kutoka Burundi; Malawi; Angola; Sudan Kusini; Madagascar pamoja na Mwenyekiti wa Tume ya AU, Faki Mahamat na Katibu Mkuu SADC, Elias Magosi Katibu Mkuu EAC, Veronica Nduva.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED