Baada ya kung'ara kimataifa, mshambuliaji nyota wa Tanzania, Selemani Mwalimu (Gomez), anayekipiga katika Klabu ya Wydad Athletic Casablanca ya Morocco, ameendelea kuwa chachu ya matumaini kwa vijana waliocheza naye michuano ya Bi Mkubwa Ramadhan Cup msimu wa 2024/25.
Akizungumzia safari ya Gomez katika soka, mfanyabiashara maarufu na mdau wa maendeleo wa Wilaya ya Hai, mkoani Kilimanjaro, Shaban Mwanga, amesema mafanikio ya Mwalimu yamefungua ukurasa mpya wa hamasa kwa wachezaji wanaoshiriki mashindano hayo.
Mwalimu, aliyesajiliwa na Wydad AC akitokea Singida Big Star na Fountain Gate, alionyesha makali yake kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya kuhamia Morocco. Michuano ya Bi Mkubwa Ramadhan Cup, inayodhaminiwa na Shaban Mwanga, imetajwa kuwa moja ya ngazi muhimu katika kukuza vipaji vya soka nchini.
"Namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kubariki kazi yangu ya kuibua vipaji nchini na kuwawezesha vijana kutimiza ndoto zao. Pamoja na changamoto tunazopitia, hatutakata tamaa kusaidia vijana wa Hai na jamii kwa ujumla," alisema Mwanga.
Mwalimu sasa anatarajiwa kuwa sehemu ya kikosi cha Wydad AC kitakachoshiriki Kombe la Dunia la Vilabu, kinachotarajiwa kufanyika Marekani kuanzia Juni 15 hadi Julai 13 mwaka huu.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED