Serikali yabainisha fursa kwa waandishi wa vitabu

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 04:20 PM Aug 03 2024
Waziri wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda.
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda.

SERIKALI imetenga fedha katika bodi ya maktaba ya Tanzania kwaajili ya kununua vitabu vikiwemo ambavyo vitakuwa vimeshinda kwenye tuzo ya taifa ya Mwalimu Nyerere ya uandishi bunifu ili kuhakikisha waandishi wanapoandika na kwenda kuchapisha wanapata faida.

Hayo yamebainishwa leo na Waziri wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda, mkoani Dar es Salaam wakati wa hafla ya uzinduzi wa kitabu cha A Tangled Web, akieleza kuwa kuna baadhi ya watu wanaogopa kuchapisha vitabu kwa kuhofia kupata hasara.

Amesema serikali bado inahimiza usomaji wa vitabu ndio maana imeanzisha tuzo ya Mwalimu Nyerere ya uandishi bunifu, na kwamba wameweka mkakati pia wa kununua vitakavyothibitishwa kuwa ni vizuri na kuvipeleka mashuleni.

"Tuna kamati ambayo itakuwa inatushauri vitabu ambavyo tutakuwa tunavinunua kupitia maktaba ya taifa, tungependa riwaya na hadithi za maisha kama za marais wastaafu hayati Mkapa na Mwinyi, tuone vinasomwa mashuleni.

"Hii itachechea watu sio uandhishi bunifu tu lakini kujua historoa na kuchochea watu kuwa wajasiriamali kwa kuangalia maisha ya waliopita, waandishi wanatunza historia, wanaweka kumbukumbu na utamaduni hivyo wanahitaji watunzwe na kuwapa kipaumbele," amesema Prof. Mkenda.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) Anneth Komba, amesema setikali imefanya mapitio makubwa ya mitaala ya elimu na katika mabadiliko hayo wamezindua ufundishaji na ujifunzaji wa masomo ya fasihi ya Kiswahili na 'literature' kuanzia kidato cha tatu.

Waziri wa Elimu Prof. Adolf Mkenda kushoto, Mkurugenzi wa TET Anneth Komba watatu, na Mwandishi wa kitabu cha A Tangled Web Eunice Urio kulia, wakipiga makofi baada ya kuzindua rasmi kitabu hicho. Picha Maulid Mmbaga.

Amesema masomo hayo yanatoa nafasi na fursa kwa waandishi kuandika vitabu vya kutosha ili ifike mahali watoto wasome riwaya zilizoandikwa na watanzania, huku akimpongeza Eunice kwa uthubutu huo.

"Tuna uhitaji mkubwa wa vitabu vya hadithi za watoto na mashairi, kwahiyo waandishi andikeni na mvilete taasisi ya elimu, tutavifanyia ithibati baada ya kujiridhisha vitatumika katika mashule yetu," amesema Anneth.

Mwandushi wa kitabu cha A Tangled Web, Eunice Urio, amesema kinawalenga vijana na kina mafunzo mengi ikiwemo athari ya kusema uongo na matokeo yake, kupenda mali na fedha kwa kuzitafuta kwa njia ambayo sio halali,  na kinafundisha namna ya mtu kuwa na maadili na nidhamu ya maisha.
1

Pia amesema wanakutana na changamoto nyingi ikiwemo ya rasilimali fedha, huku akitoa wito kwa serikali kuweka mazingira wezeshishi katika mnyororo wa thamani kwa waandishi wa vitabu ili kuwawezesha kufanya kazi yao iwe rahisi zaidi.

"Vitabu ndivyo vinaeleza utamaduni wetu, vinaweka kumbukumbu ya maisha yetu na zama tunazoishi, kwahiyo watu wasipoandika itafika mahali wataulizana zamani kulikuwa kunafanyika nini, ni muhimu watu waweke hizo kumbukumbu na pia ni njia ya kufundisha vizazi vijavyo na kuendeleza mila na desturi zetu," amesema Eunice.

2