Samia: Watu wanadai katiba yao

By Romana Mallya , Nipashe
Published at 08:03 AM Apr 05 2024
news
Picha: Ikulu
Rais Samia Suluhu Hassan.

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema watu wanadai katiba yao, akielekeza Wizara ya Katiba na Sheria kufanyia kazi suala hilo.

Mkuu wa Nchi alitoa kauli hiyo jana Ikulu, jijini Dar es Salaam katika hotuba yake baada ya kuapisha viongozi mbalimbali aliowateua hivi karibuni.

Akitoa maelekezo mahsusi kwa Naibu Waziri mpya wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, Rais Samia alisema, “Wewe (Sagini) ni mzoefu serikalini. Nenda kasaidie katika katiba na sheria. Kipindi hiki tulichonacho watu wanadai katiba yao, nenda kasaidiane na waziri, ninaimani utafanya vizuri."

Baada ya kuwapo mvutano wa muda mrefu katika serikali, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na vyama vya upinzani, hatimaye Juni 2022, chama tawala kilitangaza kuridhia kufufua mchakato wa Katiba Mpya uliokwama tangu mwaka 2015, yaani miaka 10 iliyopita.

Mnamo Juni 22, 2022, aliyekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, alitangaza chama hicho kimekubali kufufua mchakato wa Katiba Mpya, wakiwa na angalizo kwamba uzingatie maslahi ya taifa.

"CCM tunasisitiza umuhimu wa kuwapo Katiba Mpya kwa kuzingatia mazingira ya sasa na kuona namna bora ya kufufua, kukwamua na kukamilisha mchakato wa Katiba Mpya kwa maslahi mapana ya taifa na maendeleo kwa ujumla," alisema Shaka ambaye sasa ni Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, mkoani Morogoro. 

Wakati wa mkutano wa mwaka jana wa Bunge la Bajeti, serikali ilitangaza kuongeza takriban Sh. bilioni tisa katika bajeti ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka 2023/24, ili kukwamua mchakato wa Katiba mpya uliokwama Aprili 2, 2015, kwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kutangaza kuahirisha kura ya maoni ya Katiba Inayopendekezwa iliyokuwa ifanyike Aprili 30, mwaka huo.

Katika hotuba yake jana, Rais Samia alitoa maagizo kwa viongozi wateule, akichambua kila mmoja, kibarua kilichoko mbele yake na matokeo anayotaka.

Rais pia aliagiza hoja zote za ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) alizokabidhiwa Machi 28, mwaka huu, zifanyiwe kazi mara moja ili Bunge linapozijadili ripoti hizo, hoja ziwe zimeshajibiwa.

Alitaja sababu za mabadiliko hayo aliyoyaita ya kawaida ni kuimarisha ufanisi katika kutoa huduma kwa wananchi.

Rais Samia alielekeza viongozi hao wakafanye kazi ya kuunganisha watu na kutatua migogoro iliyoko katika maeneo walikoteuliwa na si kwenda kuitengeneza.

WENYE MIGOGORO 

Akitoa maelekezo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulevamu), Degratius Ndejembi, Rais Samia alimweleza kuwa wameamua kumpandisha kutoka Naibu waziri kuwa Waziri kamili kutokana aliyofanya maeneo mbalimbali.

“Umesaidia vizuri mawaziri uliofanya nao kazi na tumeona na wewe ukashike hapo. Na ni matumaini yangu utakwenda kufanya vizuri. Ninadhani utakwenda kufanya yote, mbali ya kusimamia taasisi mbalimbali, una watu wenye ulemavu na vijana.

“Na vijana ndio wanafanya nusu (ya watu) ndani ya nchi, wanatarajia makubwa kutoka kwako. Wizara inasimamia sera na mipango ya makundi haya, kazi yako nenda karatibu sekta zote zinazohusika na vijana,” aliagiza.

Rais alisema kazi kubwa ya waziri huyo mpya ni kuhakikisha vijana wanapata mafunzo na kupata maeneo ya kufanya kazi, ajira na kujiajiri.

Alionya viongozi wa wizara hiyo kuwa hataki kusikia wanagongana kwa kuwa ni vijana na watendaji watakaokuwa na migogoro wataondoka wote.

RIPOTI ZA CAG

Rais Samia pia alimtaka Waziri Ndejembi na mawaziri wengine kushughulikia yale yote yaliyoainishwa ndani ya Ripoti ya CAG kwa Mwaka 2022/23, yasimamiwe na kufanyiwa kazi na hoja zijibiwe mara moja ili Bunge litakapozijadili, ziwe zimejibiwa tayari.

“Na mkijibu kwa haraka tutajua yapi yamejibiwa na yapi bado na hatua gani zichukuliwe. Wote mkasimamie hayo,” Rais Samia aliagiza.

Kuhusu uteuzi wa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Zaibabu Katimba, Rais alisema kuwa pamoja na 'upya wake serikalini', ni mbunge mzuri mwenye uzoefu ndani ya Bunge na anayejua yanayoulizwa kwa serikali, hivyo akafanye kazi.

“Nimekuweka TAMISEMI, wizara pana yenye mambo mengi na wewe ni mdogo, ninajua utakwenda haraka na waziri wako (Mohamed Mchengerwa) ni mzuri sana. Timu ya TAMISEMI sasa hivi ni nzuri sana, nenda kashirikiane mfanye kazi. Suala kubwa ni asilimia 10 kwa vijana, Ndejembi atakuja kukaa kooni,” alisema.

TRAFIKI BARABARANI

Akitoa maelekezo kwa Naibu Waziri mpya wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Daniel Sillo, Rais Samia alimweleza kuwa yale aliyokuwa akiwaambia akiwa mwenyekiti wa kamati ya Bunge anakwenda kuyaona katika wizara hiyo.

“Fedha inayoingizwa itoshe na mambo yaende. Upo field (eneo la kazi) sasa haupo katika kiti cha theory (nadharia). Kamsaidie waziri, wizara hii ina mambo mengi mno na sasa tunaibadili, tunataka iende kieletroniki.

“Tunataka vituo vyako vya polisi vilivyoko Rorya vitoe taarifa siku hiyohiyo matukio yakitokea na Mkuu wa Jeshi apokee ripoti.

"Usalama barabarani tunataka kuondoa trafiki, tunataka kuondoa rushwa, tuweke kamera na mambo mengine, ambayo yatafanya kazi automatically (moja kwa moja) kusiwe na (askari wa) usalama barabarani.

“Pia weee nenda, wee subiri, wee ahaa...! Kuna mambo mengi miradi mikubwa inasubiri ukifika huko waziri atakuongoza,” alisema.

JAMII NAMBA

Rais Samia, akizungumzia uteuzi wa Maryprisca Mahundi, alisema, “Nimefanya makusudi kumbadilisha, ni mwanasheria, ambaye sasa ni Naibu Waziri wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, anakwenda kumsaidia Waziri Nape (Nnauye).

“Kuna mambo mazuri jana (juzi) umeona (uzinduzi wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi), nenda kasimamie, kuna mikataba mikubwa wanaingia, kasaidie kuweka jicho la kisheria.

“Nilitoa agizo Watanzania wote kila mtu awe na namba yake, wenyewe wameipa jina ‘Jamii Namba’, nenda kasimamie hii tujuane humu ndani nani ni nani, haiwezekani mtu mmoja ana identities (vitambulisho) tatu".

UBAMBIKIAJI BILI

Kwa Naibu Waziri wa Wizara ya Maji, Kundo Mathew,  Rais alimtaka kuhakikisha maji yanafika kwa wananchi kwa kuwa CCM imewataka ifikapo mwakani, wawe wameyasambaza kwa asilimia 95 mijini na asilimia 85 vijijini ambapo wanaamini watazidi asilimia hizo.

“Nenda mkasimamie vijijini ifike asilimia 87 tuliyojiwekea, isipofika mniambie wapi mmezubaa. Kuna miradi lazima imalizike.

“Bili za maji ni kilio cha wananchi, tumelia sana na kubambikwa bili za maji, mkaenda kwenye mita, bado kuna kilio, fanyeni kama TANESCO (Shirika la Umeme Tanzania). Tafuteni mita ambazo watalipa namna wanavyotumia.

"Nimesikia mmewahi kuziagiza na zimepimwa zina matatizo madogo karekebisheni mzifunge kwa wananchi na zitawafundisha matumizi ya maji,” alisema.

MOTO WA MAKONDA

Rais Samia alipongeza utendaji wa Paul Makonda katika siku 162 akiwa Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, akibainisha kuwa amefanya kazi kubwa ndani ya chama kwa kukichemsha kwa kutoa uvivu uliokuwa kwa kila mmoja.

“Umekichemsha chama. Tumeamka vizuri sana. Tumekupeleka Arusha, unajua nini kipo Arusha. Unajua matumaini yangu Arusha. Mimi nina matumaini nawe. Utafanya kile ambacho mimi ninatamani ukafanye," Rais alielekeza.

Rais Samia alimweleza Mkuu huyo mpya wa Mkoa wa Arusha kwamba utalii jijini Arusha umekua, wageni ni wengi, malazi hayatoshi, hivyo kumtaka akasimamie suala hilo kwa kushirikiana na wawekezaji.

“Arusha ni mji mkubwa sana na ni Makao Makuu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na taasisi kubwa za kiulimwengu zipo pale. Nenda kasimamie vizuri mkoa uwe na jina zuri,” aliagiza.

Kuhusu Mkuu mpya wa Mkoa wa Mara, Kanali  Evans Mtambi, Rais alisema mkoa huo kutokana na wasifu wake, ameona huyo ndiye anaweza kufanya yote ikiwamo kuinua mikoa ya Mara na Kagera kwa kushirikiana na mwenzake walioko ukanda hao.

Alisema kuna kilimo mkoani Mara ambacho hawakipendi, lakini ni kizuri kwa biashara, hivyo akakisimamie kwa sheria, kwa kuwa kuna watu wa serikali wanakisindikiza kwa magari yao baada ya kuvunwa kwenda nchi jirani.

Pia alimtaka akasimamie mpaka na hifadhi zilizoko huko, pia kukuza utalii.

Kuhusu Naibu Katibu Mkuu, Rais Samia aliwataka wakafanye kazi vizuri, huku akimtaja Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Suleiman Serera, kuwa ni kijana mdogo na ataweka jicho la karibu kwake kwa kumfuatilia na kumshauri ili akue vizuri.

MAHAKAMANI

Rais Samia pia alitaka Sylvester Kainda, Jaji Mahakama Kuu ya Tanzania, akasimamie haki kwa wale wanaostahili kuzipata na wasio na haki asiwape.

Katika hafla hiyo, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, alisema, "Suala la mazingira linamgusa kila mmoja, niwaombe sana mazingira ya nchi yameharibika, tuna wajibu wa kuyarejesha ili nchi iendelee kustawi."

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alisema Rais ana imani na viongozi hao alioteua hivi karibuni, hivyo wafike kwa wananchi kusikiliza na kuwapa huduma kwa kutatua kero zao na kutimiza malengo.

Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alisema, “Bahati nzuri mmepata imani hii katika kipindi ambacho Bunge la Bajeti linaendelea, hivyo hakutakuwa na muda mrefu wa kujifunza kwa ninyi tunaowatarajia kuja bungeni kujibu hoja za wabunge."

Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Juma, alisema watendaji wa mahakama walioapishwa wataongeza nguvu ya kutenda haki mahakamani.

“Wale wanaopeleka changamoto zao za kisheria kwako Mheshimwa Rais, ninaomba wawe wanapeleka kwa Msajili wa Mahakama, ndiye anayeshikilia injini ya mahakama na ndiye anajua inakoelekea,” alisema.

Uteuzi wa wakuu wa mikoa na mawaziri ulitangazwa usiku wa kuamkia Jumapili ya Pasaka, uteuzi wa Prof. Joyce Ndalichako katika nafasi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri ukitenguliwa.