RAIS Samia Suluhu Hassan, jana amewaapisha mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na mabalozi, aliowateua hivi karibuni huku akimtaka Profesa Mohamed Janabi aliyemteua kuwa mshauri wa Rais katika masuala ya afya, kujiandaa kugombea nafasi iliyoachwa wazi na Hayati Faustine Ndugulie ya Ukurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kanda ya Afrika.
Ndugulile aliyekuwa mtaalamu wa afya ya umma na Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, alikuwa mmoja wa wagombea watano waliojitokeza kumrithi Dk. Matshidiso Moeti, raia wa Botswana.
Alipaswa kuapishwa Februari 2025, lakini umauti ulimchukua kabla ya kukalia kiti chake.
Akiwaapisha wateule hao Ikulu ya Tunguu, Zanzibar, Rais Samia alisema, kutokana na wadhifa wa Profesa Janabi, jina lake limependekezwa na kupelekwa katika mchakato wa kugombea nafasi hiyo.
Akizungumza na viongozi hao baada ya kuwaapisha, hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwamo Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Rais Samia alisema kutokana na kasi ya ukuaji wa sekta ya mawasiliano na teknolojia ya habari duniani, serikali imekuja na mkakati wa kidijitali wa kitaifa unaohitaji kushughulikiwa ipasavyo.
Alisema bado hajaridhishwa na kasi ya utendaji katika teknolojia ya habari na ni lazima kwenda na kasi katika hiyo, ndio maana ameitoa sekta ya habari katika Wizara ya Mawasiliano na kuipeleka katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Pia, mawasiliano ndani ya nchi na kuunganisha nje ya nchi ikiwamo minara ya simu ambayo inahitaji kazi kubwa ya kulifanya Shirika la Simu (TTCL) na Shirika la Posta kusimama yenyewe na kuwa kibiashara.
Alisema kubadilisha nafasi za mawaziri na manaibu waziri kutoka wizara moja kwenda nyingine lengo lake ni kuongeza ufanisi ndani ya serikali.
Aliwataka viongozi hao aliowaapisha kwenda kufanya kazi vizuri kwa kushirikiana na watendaji wengine katika wizara husika ili kuliletea maendeleo taifa katika kila nyanja.
Alisema amemteua Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo baada ya kupitia wasifu wake, pia ni mwanahabari na ana uzoefu mkubwa unaompa imani kuwa atafanyakazi vizuri katika sekta hiyo.
“Nenda kaikamate vizuri sekta ya habari unajua vizuri changamoto zilizopo pamoja na changamoto za wanahabari,” alisema Dk. Samia.
Kuhusu uteuzi wa Dk. Ashantu Kijaji kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, alisema amekuwa akimhamisha kutoka wizara moja kwenda nyingine na sasa ni wakati wa kuvaa suruali ya jinzi na kutoka ofisini kwenda kwa wafugaji na wavuvi kufanya kazi kwa sababu kuna kero nyingi za wafugaji kuingia katika hifadhi pamoja na mashamba ya wakulima.
Aidha alimtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Yussuf Masauni, kuimarisha Muungano ili kujijengea wadhifa mzuri wa kuendelea kubaki katika Jimbo la Kikwajuni kwa sababu linazingirwa katika nafasi ya ubunge.
Akizungumzia kuhusu nafasi za ubalozi, Rais Samia alisema aliowateua hasa wa upande wa kisiasa wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali ni ambao bado wanafanya vizuri na wapo ngangari kwa sababu baadhi ya mabalozi wamefika umri wa kustaafu na anawerejesha nchini kuunga mkono katika kampeni za uchaguzi mkuu.
Aliwataka mabalozi hao kuwa ngangari kwa sababu baadhi ya maeneo wanayokwenda kufanya kazi kuiwakilisha Tanzania hayapo tulivu na amefanya uteuzi wa mabalozi kwa kutumia vigezo ikiwamo vya uaskari.
“Tunataka mkaweke nguvu kwa sababu baadhi ya maeneo mnayokwenda sio salama kwa mfano Msumbiji na maeneo mengine na ndio maana baadhi ya mabalozi tumeachagua wapo katika kazi ya uaskari,” alisema.
Naye Makamu wa Rais aliwasihi viongozi hao, kwenda kufanya kazi kwa ushirikiano na viongozi wengine na kuheshimu mawazo ya wataalamu waliowakuta katika nafasi zao ili kuwaletea ushindi wananchi wa Tanzania kwa maisha bora zaidi.
Aliwataka mabalozi walioapishwa kwenda kufanya vyema kwenye diplomasia ya uchumi ili jitihada za Rais Samia kupitia falfasa ya 4R itekelezwe kikamilifu.
Alisema viongozi hao wana kazi kubwa ya kuhakikisha wanayoyataka Watanzania yanatekelezwa kikamilifu kuendana na Ilani ya CCM na watakapoingia katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 wanafanya kazi ambayo Rais na Watanzania wote wanaitarajia.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED